Na Issa Mtuwa Bukombe

Kazi kubwa ya kiongozi yeyote aliepewa dhamana, ana wajibu wa kuhahikisha anabadilisha maisha ya watu kwa kushugulikia matatizo na kero zao kwenye eneo alilopewa, na ndio maana Rais Magufuli kila kukicha anawaza juu ya changamoto za Watanzania na anawahiza viongozi wote kushugulikia matatizo ya Watanzania.

Akiongea na Wananchi wa vijiji mbalimbali katika kata ya Ushirombo na Bugelenga wilaya ya Bukombe katika muendelezo wa ziara yake katika mkoa wa Geita, jana Machi 2, 2019, Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko amesema “dhana” ya kushugulika na matatizo ya watanzania katika wizara yake na wananchi wa jimbo lake kwa ujumla ndiyo inayomfikisha kila mara kwenye maeneo mbalimbali nchini kushugulikia matatizo yao ikiwemo Bukombe.

Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko akizungumza na Wananchi wakiwemo Wachimbaji wadogo wa Madini katika kijiji cha Busonjo kata ya Busonjo wilaya ya Bukombe mkoa wa Geita.

Akihutubia wananchi wa Kijiji cha Mkange kata ya Bugelenga, Biteko amewambia wananchi hawanabudi kuuchukia umaskini kwa kujishugulisha na kufanya kazi kwa bidii. Amesema hata yeye wanae muona leo, ni mtu alietokana na familia maskini na ndio maana hata kipindi akisoma walikuwa wakimuita “Doto Maziwa”, kwa kuwa sehemu kubwa ya gharama za masomo yake ilitokana kwa kuuza mazima hivyo kila familia ijitume kufanya kazi kwa kutumia fursa zilizopo.

“Ndugu zangu, ngoja niwaambie ukweli, nimetembea nchi nyingi sana, kuna nchi zina watu masikini zaidi kuliko hata sisi, mi niwaombe kama wewe huna ulemavu wa kukufanya ushindwe kufanya kazi ndugu zangu tuchapeni kazi, tuibadilishe Bukombe yetu” alisema Biteko.

Biteko amewaambia wananchi kuwa hataona fahari kama matatizo ya Watanzania katika sekta ya madini na wananchi wake wa Bukombe wanaendela kuwa na changamoto na hazipatiwi majawabu. Amesema kama ambavyo ameweka mkazo katika kuondoa kila aina ya kero kwenye sekta ya madini ndivyo hivyo hivyo anahakikisha anaondoa kero za wananchi wa Bukombe katika sekta Afya, Elimu, Miundombinu, Maendeleo ya jamii, vijana, wanawake na walemavu.

Katika ziara yake Biteko amekagua shuguli mbalimbali za maendeleo ikiwemo kuweka jiwe na msingi katika majengo ya zahanati, kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa na nyumba za waalimu, kukagua madaraja na miundombinu ya barabara katika kuhakikisha ilani ya  chama cha Mapinduzi inatekelezwa.