Na Nuru Mwasampeta- Kahama

Waziri wa Madini, Doto Biteko awaeleza wachimbaji wadogo wa Madini, wanaokwepa  kulipa kodi na kujihusisha na utoroshaji wa madini nje ya nchi   kuwa wakati wao wa unyakuo  umekwisha kufika.

Ameyasema hayo mjini Kakola, halmashauri ya Msalala wilayani Kahama katika nyakati mbalimbali alipokuwa katika ziara ya kikazi iliyolenga kukagua na kujiridhisha kwa taarifa za ubadhirifu alizozipata kutoka kwa wenye mapenzi mema nan chi yao ya Tanznania.

Akizungumza katika hatua tofautitofauti wakati wa ziara hiyo, Biteko alibainisha kuwa wakazi 12 wa eneo hilo wamebainika kujihusisha na biashara ya madini pasipokufuata taratibu na sheria zilizowekwa aidha, wanajihusisha na kutorosha madini hayo na kuyauza nje ya nchi pasipo kulipia kodi za Serikali.

1. Wananchi wa Kakola wakinyosha mikono juu na kukiri kuwa watalipa kodi ya serikali mara baada ya kuongozwa na Waziri wa Madini, Doto Biteko alipokuwa akihitimisha hotuba yake alipofanya mkutano wa hadhara mjini Kakola wilayani Kahama Jana tarehe 17/07/2019

“Nawaambia kuwa biashara hiyo imefika mwisho na nawapa pole, na hakuna wa kuwasaidia, na jinsi tulivyokuwa tukihubiri habari za unyakuo na ninyi mtanyakuliwa”

“leo tumetembelea baadhi ya watu tuliokuwa na taarifa zao na kukutana na mambo ya kusikitisha ambayo hayavumiliki.” Biteko alisisitiza.

Mmoja miongoni mwao ndani ya wiki mbili amenunua dhahabu yenye thamani ya shilingi mil. 331,209,200/- kiasi cha kg 3.6 na ameyauza pasipo kuyalipia kodi ya serikali, ungekuwa  wewe serikali ungemfanyaje? Biteko alihoji.

Aidha, mnunuzi mwingine ndani ya wiki tatu amenunua dhahabu yenye thamani ya shilingi milioni 241,490,800/-  sawa kg 2.64 na hajalipia kodi hata shilngi moja japo akinunua kwa wachimbaji anawakata na pesa ya serikali, na badala yake zote husipeleki serikalini tukufanyaje? Saa ya unyakuo imefika tutawanyakua.

Akitoa salamu za Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Biteko alisema ametumwa na Rais kuwataka walipe kodi za serikali.

Pamoja na hayo, Biteko amebainisha mpango wa Serikali katika kurahisisha usimamizi wa mialo nchini na kubainisha kuwa mialo yote itawekwa sehemu moja na kuwa na uongozi maalum ukishirikisha uongozi wa wizara na ofisi ya mkurugenzi wa Halmashauri pamoja na uongozi wa wachimbaji wadogo wa madini.

Biteko amesema uamuzi huo umefikiwa ili kusaidia katika kutunza mazingira pamoja na kusaidia kupata taarifa sahihi za uzalishaji wa dhahabu katika mialo husika.

Pamoja na hayo serikali itaanzisha utaratibu wa kuchoma dhahabu katika eneo moja litakalochaguliwa ili kuondoa hali ya kila mmiliki wa mialo kuchoma dhahabu mahali anapojua yeye jambo ambalo linalochangia kwa kiasi kikubwa kutopatikana kwa taarifa muhimu za uzalishaji.

2. Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza na Wananchi wa Kakola wilayani Kahama alipofanya mkutano wa hadhara Jana tarehe 17/07/2019

Kwa upande wake, mwenyekiti wa viwanda vya uchenjuaji wa madini Mkoani Shinyanga Nicodemas Majabe alisema kuwa wachimbaji wadogo wamekuwa wakishawishiwa na wanunuzi na kuuza madini kinyemela kwakuwa kwa wakati huo wanakuwa hawana fedha za matumizi wawapo mgodini.

Aliendelea kusema amepanga vikosi vya kuwadhibiti  wanunuzi na kuhakikisha dhahabu haisafirishwi kwenda nchini Kenya na kwingineko na kuongeza kuwa mnunuzi atakayeruhusiwa kununua madini ni yule mwenye leseni inayomruhusu kufanya hivyokutoka Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini.

Naye Kamishna wa Madini, kutoka Tume ya Madini, Prof Abdulkarim Mruma aliwataka wachimbaji wadogo wahakikishe wanauza dhahabu zao katika masoko ya madini yaliyoanzishwa jambo litakalowasaidia kuuza dhahabu zao kwa bei iliyopo sokoni

Prof. Mruma alikiri kuwa asilimia kubwa ya wachimbaji wamekuwa wakiendelea kuwa maskini na kudharaulika kwenye jamii kutokana na kila mmoja kuuza dhahabu yake sehemu ambayo si sahihi.