1.0 UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba, kufuatia Taarifa iliyowasilishwa leo Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Bunge lako Tukufu sasa likubali kupokea, kujadili, na kupitisha Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu, Mpango na Bajeti ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18. Aidha, ninaomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19.

2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi  wa  rehema,  kwa  kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana tena. Aidha, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu Hotuba ya Bajeti ya Wizara yangu kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19.

3. Mheshimiwa Spika, vilevile, ninakushukuru kwa kunipa fursa hii adhimu ya kuwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu kwa mara ya kwanza Bajeti ya Wizara ya  Madini.  Kama  unavyofahamu  Wizara hii iliundwa mwezi Oktoba, 2017 baada ya kuvunjwa kwa iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini, na hivyo kufanya bajeti hii kuwa ndiyo ya kwanza ya Wizara mpya ya Madini. Wizara ya Madini inategemea sana mawazo, ushauri na maelekezo ya Bunge lako Tukufu ili kuimarisha na kukuza Wizara hii mpya.

4. Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniteua kuwa Waziri wa Madini; Wizara ambayo ni muhimu kwa uchumi wa Nchi yetu pamoja na Manaibu wangu, Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo (Mb.), na Mheshimiwa Doto Mashaka Biteko (Mb.). Tunamuahidi tutatekeleza maelekezo anayoyatoa kwa ufanisi na uadilifu na tutatekeleza majukumu  yetu  vyema  na  tutatumia ujuzi na maarifa yote tuliyopewa na Mwenyezi Mungu na tuliyojifunza kusimamia Sekta hii ipasavyo ili Taifa letu linufaike na rasilimali za madini.

5. Mheshimiwa Spika, napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uongozi wake makini katika usimamizi wa rasilimali za nchi. Sote ni mashahidi wa jinsi uongozi wake unavyogusa wananchi wa Tanzania hususan katika matumizi sahihi ya rasilimali za Taifa katika kuwaletea maendeleo.

6. Mheshimiwa Spika, pia ninawashukuru Makamu wa Rais, Mheshimiwa  Samia  Suluhu  Hassan  na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) kwa miongozo wanayonipatia katika kutekeleza majukumu yangu kikamilifu.

7. Mheshimiwa Spika, katika  suala  hili  la usimamizi wa rasilimali za nchi na hususan katika Sekta ya Madini ninayoisimamia, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais na wewe binafsi kwa kuunda Kamati ambazo zilishughulikia changamoto zilizopo katika Sekta ya Madini. Mapendekezo ya Kamati zote yamefanyiwa kazi na baadhi ya mapendekezo mengine yanaendelea kutekelezwa. Nawahakikishia kuwa, Wizara yangu itatekeleza mapendekezo yote kama yalivyotolewa na Kamati hizo.

8. Mheshimiwa Spika, vilevile, nikupongeze wewe binafsi, Mheshimiwa Job Yustino Ndugai (Mb.), Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson (Mb.), na Wenyeviti wa Bunge kwa kuendesha Bunge kwa weledi mkubwa, hekima, busara na kwa umahiri.

9. Mheshimiwa Spika, ninachukua fursa hii pia kuwashukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula (Mb.), Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Mariam Ditopile Mzuzuri (Mb.) na Wajumbe wote wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, kwa michango yao  mahsusi  wakati  wa  uchambuzi wa Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18 na Mpango na Makadirio ya Bajeti ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19. Kamati imetoa maoni mbalimbali na ushauri mzuri unaoboresha utekelezaji wa majukumu yetu na kuhakikisha Sekta ya Madini inanufaisha Taifa. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa Wizara ya Madini itafanya kazi  kwa karibu na Kamati hii kwa manufaa na maslahi ya Taifa.

10. Mheshimiwa Spika, sina  budi  kuwashukuru kwa dhati Viongozi wenzangu wa Wizara ya Madini Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo (Mb.), Naibu Waziri, Mheshimiwa Doto Mashaka Biteko (Mb.), Naibu Waziri na Profesa Simon Samwel Msanjila, Katibu Viongozi hawa na Watendaji wote wa Wizara  wananipa ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yangu na kutekeleza majukumu yao kwa kujituma, tija na ufanisi. Naahidi Bunge lako kuwa  kwa ari na kasi tuliyonayo tutahakikisha rasilimali za madini zinanufaisha Taifa na mchango wa Sekta ya Madini unaongezeka katika Pato la Taifa, maendeleo ya jamii na kupunguza umaskini nchini.

11. Mheshimiwa Spika,  napenda kutoa pole  kwa Bunge lako Tukufu, familia, ndugu, jamaa na wananchi wa jimbo la Songea Mjini kwa kuondokewa na mpendwa wao,  Mheshimiwa  Leonidas  Tutubert  Gama  (Mb.), na Jimbo la Buyungu, Kigoma kwa kuondokewa na mpendwa wao Mhe. Kasuku Samson Bilago (Mb). Aidha, naomba kuungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuwapongeza Mheshimiwa Janet Masaburi kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Mbunge, Mheshimiwa Dkt. Godwin Ole Mollel, Mbunge wa Jimbo la Siha, Mheshimiwa Stephen Lemomo Kiruswa, Mbunge wa Jimbo la Longido, Mheshimiwa Dkt. Damas Daniel Ndumbaro, Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Mheshimiwa Justin Joseph Monko, Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini na Mheshimiwa Maulid Said Mtulia,  Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, kwa kuchaguliwa na kuwa wawakilishi wa wananchi katika Majimbo hayo. Kuchaguliwa na kuteuliwa kwao ni kielelezo cha kuaminiwa na wananchi ili kuwawakilisha ipasavyo katika Bunge hili.

12. Mheshimiwa Spika, napenda kipekee kabisa kuchukua nafasi hii kumshukuru Mume wangu Mpenzi Balozi Mbelwa Kairuki pamoja na watoto wetu wapendwa kwa kunivumilia, kuniunga mkono na kuniombea kwa Mwenyezi Mungu ili niweze kutekeleza majukumu niliyopewa na Mheshimiwa Rais ya usimamizi wa sekta hii nyeti ya madini.

13. Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, naomba sasa kuwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti  ya  Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18; na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19.

>>Soma Zaidi>>