• Ni baada ya waziri Kairuki kubaini madudu baada ya ziara ya kushtukiza

Waziri wa Madini Mhe. Angellah Kairuki ameyafungia maduka manne ya vito na usonara yaliyopo katika Mtaa wa Indiragadhi baada ya kubaini ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za uuzwaji wa madini hayo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wa kwanza kulia akifuatiwa na Waziri wa Nishati mara baada ya kuwasili katika mtaa wa Indiragadhi kwa ziara ya ukaguzi wa maduka ya madini na usonara ili kujiridhisha endapo wafanyabiashara hao wanafuata taratibu za kufanya biashara hiyo.

Hayo yamebainika mara baada ya Kairuki kufanya ziara ya kushtukiza ya kukagua na kujiridhisha endapo wafanyabiashara hao wanafuata taratibu na shaeria za kufanya biashara ya madini Jijini Dar es Salaam na kubaini wengi wao kuzikiuka na kuisababishia Serikali kutokupata mapato halali ya mrabaha kutoka kwa wauzaji wa madini hayo.

Maduka yaliyofungiwa wakati wa ziara hiyo ni Sami Jewellers, New Gold Point, Almasi Jewellers pamoja na Queens Jewellers ambapo wafanyakazi wake hawakutaka kumtaja mmiliki wa maduka hayo yanayodaiwa kuwa ni ya mtu mmoja.

Waziri Kairuki alibainisha kutoridhishwa na wafanyabiashara wa madini hao mara baada ya kumaliza ziara yake ya siku ya kwanza na hivyo kuagiza maduka hayo kufungwa. “Baada ya kufanya ziara hii na kujionea madudu yanayoendelea nimeelekeza kufungwa kwa maduka manne kutokana na mmiliki wake kutokuzingatia utuzwaji wa kumbukumbu na kufanya biashara hii bila kuwa na leseni kutoka wizara ya Madini kama sheria zinavyoelekeza”. Alisema.

Alikazia kuwa, ili kufanya biashara hii, mfanyabiashara anapaswa kuwa na leseni mbili ambapo moja inatolewa na Wizara ya Madini na nyingine inatolewa na Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji.

Aidha, Waziri Kairuki alibaini kuwa, Wafanyabiashara hao wanakiuka au hawafuati mfumo elekezi wa utunzwaji wa kumbukumbu za mauzo na manunuzi ya madini hayo kutokana na maduka yote aliyoyatembelea kutokufuata utaratibu halali wa kutunza kumbukumbu hizo.

Waziri wa Madini Mhe. Angellah Kairuki mwenye blauzi ya mistari akimsikiliza mwalimu wa ukataji vito Farai Runyanga (kushoto kwa Waziri) kutoka nchini Zimbambwe aliyefika kwa ajili ya kuwaongezea uwezo wazawa ili kujishughulisha na kazi hiyo ya kusanifu madini nchini.

Kutokana na kutoridhishwa na ujazwaji wa kumbkumbu hizo Waziri Kairuki aliwaagiza wafanyabiashara hao kuhkikisha wanzingatia namna elekezi ya kutunza taarifa hizo ili kujiweka katika hali salama pindi itakapobainika kuwa madini wanayouziwa ni ya wizi au vinginevyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam aliyeamua kuambatana na Waziri kwenye ziara yake ya siku ya kwanza alisema amesikitishwa sana kuona katika mkoa wake bado kuna watu wanaokiuka sharia na taratibu za nchi na kueleza kuwa wasipotaka kufuata sharia kwa hiari basi sharia zenyewe zitawalazimisha wazifuate.

“Mimi kama Mkuu wa Mkoa huu najisikia vibaya kuwa na wafanyabiashara ambao wanakiuka taratibu na kuwa wajanja wajanja wakati wanafahamu msimamo wa Serikali ya awamu ya tano kuwa ni wajibu wa kila mmoja kufuata sharia na taratibu za ulipwaji wa kodi”. Alisisitiza.

Aidha, Makonda amewataka wafanyabiashara katika mkoa wake kuweka mazingira yao ya biashara vizuri ili kuepuka usumbufu watakaoupata endapo watakiuka taratibu hizo.