Na Tito Mselem, Musoma

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo amekabidhiwa Jengo la Kituo cha Umahiri Musoma lenye thamani ya shilingi bilioni 1.2 ambalo linalenga katika kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo.

Kituo hicho kilijengwa na Mkandarasi SUMAJKT na kukabidhiwa kwa Wizara ya Madini kupitia Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo ambaye naye alilikabidhi jengo hilo kwa Tume ya Madini Septemba 7, 2019.

Jengo la kituo cha umahiri lililopo Musoma.

Kituo cha Umahiri Musoma ni kimoja kati ya vituo Saba vya umahiri n pamoja na  Jengo moja la Taaluma lililopo Chuo cha Madini Dodoma (MRI) yaliyojengwa kwa jumla  ya shilingi  bilioni 11.9 na SUMA JKT kupitia mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP).  Vituo hivyo vimejengwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Kagera, Musoma, Bariadi, Chunya, Mpanda, Handeni Tanga na Songea.

Akizungumza kwenye makabidhiano hayo Naibu Waziri Nyongo ameipongeza SUMA JKT kwa kazi nzuri waliyoifanya ya ujenzi wa jengo hilo ambalo limekamilika kwa wakati.

Naibu Waziri Nyongo alisema lengo kuu la kuanzisha vituo hivyo ni kuwasadia wachimbaji wadogo kufanya shughuli za madini kwa tija kwa kuwapatia elimu ya uchimbaji katika vituo hivyo.

“Faida ya ujenzi huu ni kutoa mafunzo ya kitaalamu yanayohusu Madini, kutoa mafunzo ya utafiti wa madini, ikiwa ni pamoja na kuonesha mikanda ya Madini ilipo na muelekeo wake, uchimbaji wa madini wenye tija na salama, uchenjuaji wenye kuleta uvunaji mkubwa wa madini na hivyo kuwapatia faida kubwa wachimbaji”, alisema Nyongo.

Inaelezwa kuwa baada ya mafunzo ya uchimbaji bora wenye tija kutolewa kwenye vituo hivi, wachimbaji watavuna madini kwa zaidi ya asilimia 80 ukilinganisha na hapo awali ambapo wachimbaji wengi wanavuna dhahabu kwa asilimia 30 tu.

Aidha, imeelezwa kuwa, vituo hivyo vya umahiri vitakuwa na mafunzo ya namna ya kuomba leseni kwa njia ya mtandao na kutakuwa na usagaji wa mawe na kupima sampuli mbalimbali za madini.

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo mbele katikati akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi wa Serikali, Wizara ya Madini pamoja na Wachimbaji wadogo wa Mkoa wa Mara

Aidha, Naibu Waziri Nyongo ametoa rai kwa wachimbaji wadogo wa Mkoa wa Mara kukitumia kituo hicho cha umahiri ili viwaletee tija na faidsa katika shughuli za uzalishaji madini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vicent Naano ameipongeza Wizara ya Madini kwa Kujenga kituo cha umahiri katika Mkoa wa Mara maana kitawasaidia sana wachimbaji kufanya kazi kwa uhakika na sio kubahatisha.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) Veronica Francis alisema kuwa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) ilifanya utafiti wa kijiolojia na kubaini maeneo saba nchini kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya umahiri.

“Utafiti umebaini kuwepo kwa kiwango kikubwa cha dhahabu katika eneo la Buhemba yenye takribani wakia 10,737 zenye viwango vya 0.7g/t ndiyo sababu kituo hiki kikajengwa hapa Musoma ili kiwasaidie wachimbaji wadogo kupata mafunzo ya namna bora ya uchimbaji madini,” alisema Veronica.