Nuru Mwasampeta na Tito Mselem

Naibu Waziri wa Madini, Stansilaus Nyongo jana tarehe 28 April, 2019 amepokea ujumbe ulioongozwa na Naibu Waziri wa Maliasili wa Jamhuri ya Watu wa China waliofika kwa ajili ya kujadili maeneo ya kushirikiana katika sekta ya madini baina ya nchi hizo mbili yaani Tanzania na China.

Akizungumza wakati akifungua kikao cha majadiliano baina ya nchi hizo mbili, Nyongo aliwahakikishia wageni hao kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imeweka mazingira mazuri ya kuwekeza nchini kupitia sekta ya Madini na kuwataka kutosita kutembelea maeneo mbalimbali ili kujionea fursa zilizopo na kuwekeza nchini Tanzania.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (Mbele Kushoto) akiwa na Naibu Waziri wa Maliasili wa China Dkt, Zhong Ziran (Kulia) pamoja na wajumbe walioambatana nao katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl. JK Nyerere Jana.

Nyongo amewadhihirishia wageni hao uwepo wa sera na sheria  zisizokandamiza upande wowote baina ya wawekezaji, wananchi na Serikali na hivo kuzifanya pande zote kunufaika na rasilimali na uwekezaji unaofanyika katika sekta ya madini.

Aidha, Nyongo amebainisha kuwa ushirikiano baina ya Tanzania na China ni wa muda mrefu ikiwa ni takribani miaka 50 na kufika kwa ujumbe huo kunabainisha wazi kuwa  urafiki na ukaribu baina ya nchi hizo hauna mashaka.

Akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya mkutano huo, Nyongo alisema wataalamu kutoka China wamekuja kuunganisha nguvu ya pamoja na watanzania ili kuweza kusaidiana katika kufanya tafiti za kina katika kujua kiasi cha madini yaliyopo, namna nzuri ya kuvuna madini hayo pamoja na namna ya kuyaongezea thamani madini yaliyopo nchini kabla ya kuyasafirisha nje ya nchi.

Pia, Nyongo amebainisha kuwa China ipo tayari kuleta wataalamu katika masuala ya madini watakaojikita katika kufanya shughuli za uchimbaji wa madini.

Naibu Waziri Nyongo amebainisha kuwa ujio wa ujumbe kutoka China utasaidia kuweka makubaliano ya pamoja baina ya Taasisi ya Utafiti na Jiolojia Tanzania na Taasisi ya Jiolojia na utafiti ya nchini China katika kusimamia masuala ya utafiti wa madini katika maeneo ambayo hayajafikiwa.

Zaidi ya hayo Nyongo amewadhihirishia wageni hao uwepo wa mazingira mazuri na rafiki ya uwekezaji yanayotokana na uwepo wa sera na sheria zisizokandamiza upande wowote baina ya wawekezaji na Serikali na kuwataka kutosita kuja kuwekeza nchini.

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Utafiti na Jiolojia nchini Bi Yourghbert Myumbilwa amesema ushirikiano huo utaleta manufaa makubwa kwani uzoefu wa China katika masuala ya utafiti ni mkubwa hivyo itawawezesha watumishi wa taasisi hiyo kupata uelewa mkubwa katika kutekeleza majukumu yao.

Akizungumzia ujio wa ujumbe wake nchini, Naibu Waziri wa Maliasili wa China Dkt. Zhong Ziran amesema ni kuweza kujadili na kukubaliana juu ya maeneo ya kushirikiana baina ya Tanzania na China kupitia maliasili madini inayopatikana nchini.

Ushirikiano huu baina ya Taasisi ya Utafiti na Jiolojia nchini na Taasisi ya Utafiti wa Jiolojia nchini China ni matokeo ya kikao kilichofanyika mwezi Desemba, 2018 baina ya aliyekuwa Waziri wa Madini, Angellah Kairuki na Waziri wa Maliasili wa China kilichofanyika katika ofisi za Wizara ya Maliasili nchini China ambapo Mhe. Kairuki alishiriki kongamano la uwekezaji lililofanyika  nchini humo na kuibua fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya madini.