Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) ulio chini ya Wizara ya Madini, unatarajia kujenga jengo kubwa la kuingiza kiasi cha Wanafunzi 200  kwa wakati mmoja katika Chuo Cha Madini Dodoma.

Matukio mbalimbali yakimwonesha Waziri wa Madini Angellah Kairuki pamoja na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wakipata maelezo kuhusu namna mashine na vifaa mbalimbali vya utafiti, uchenjuaji , na utenganishi wa madini pamoja na uchimbaji bora wa madini kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira kutoka kwa wanafunzi wa Chuo cha Madini Dodoma ikiwa sehemu ya kazi mbalimbali zinazofanywa na wanafunzi hapo chuoni.

Hayo yalibainishwa  mwishoni mwa wiki na Waziri wa Madini Angellah Kairuki wakati akitolea ufafanuzi changamoto zilizowasilishwa na Serikali ya Chuo hicho wakati  wa maadhimisho ya Siku ya Madini chuoni hapo.

Alisema, ujenzi huo unatarajia kuanza mwezi Julai mwaka huu  na kuongeza kuwa wizara  kupitia wadau wake wa maendeleo itajenga viwanja vya michezo chini ya usimamizi wa Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo.

Kwa upande wake, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo hicho, Chuo Elia Mwita  alimwomba Waziri Kairuki kuwakutanisha na wadau wa sekta ya madini nchini ili kuwawezesha kupata fursa ya kuonesha ujuzi waliopata kutoka katika Chuo hicho.

Mbali na ombi hilo, Mwita aliwasilisha maombi mbalimbali ya wanafunzi  ikiwemo kutumiwa kama mabolozi pindi wanapomaliza mafunzo yao, kupatiwa fursa za udhamini wa masomo ya juu kupitia wizara, kuwapatia fedha za kujikimu  wakati wa mafunzo na kuingizwa katika Huduma ya Afya kupitia  Bima ya Afya.

Sambamba na kufanya mikutano  ya uongozi wa wanafunzi, pia Waziri Kairuki alitembelea maonesho ya kazi za wanafunzi, kugawa zawadi kwa timu zilizoshinda katika michezo mbalimbali iliyofanyika, ambapo katika siku hiyo MRI iliitambua siku hiyo kama Siku ya Madini.

Pia, Waziri Kairuki alipokea Muhtasari wa taarifa ya chuo kutoka kwa Kaimu Mkuu wa Chuo Bw. Vincent Pazzia pamoja na risala kutoka kwa Rais wa Serikali ya Chuo  hicho, Elia Mwita.

Katika maadhimisho hayo, Waziri Kairuki aliambatana na Naibu Waziri Stanslaus Nyongo, Viongozi wa Wizara na Taasisi.

Imeandaliwa na Samwel Mtuwa, Dodoma