Na Tito Mselem, Kyerwa

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo amefungua Soko la Madini ya Bati (Tin) Wilayani Kyerwa Mkoa wa Kagera na kuwataka wafanyabiashara wa Madini hayo kuacha kuyatorosha na kuyapeleka nchi za nje zikiwemo za Rwanda, Uganda na Kongo badala yake wametakiwa kuyauza kwenye soko lililozinduliwa kwakuwa changamoto za tozo na bei zimekwisharekebishwa hali itakayopelekea kuuza na kununua kulingana na soko la dunia.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Nyongo ametoa mwezi mmoja kwa wamiliki wa leseni za uchimbaji wa Madini ya Bati (Tin) wasioendeleza leseni hizo kuziendeleza na wasiofanya hivyo watafutiwa na kupatiwa wengine wenye nia ya kuziendeleza.

Naibu Waziri Nyongo aliyasema hayo Mei 8 wakati akizindua Soko la Madini ya Bati lililoko wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera.

“Hatutakuwa na msamaha kwa mtu au kampuni yoyote itakayoshikwa ikitorosha Madini ya Tin kupeleka nje ya nchi au kufanya biashara ya Madini hayo nje ya Soko hili tunalolizindua leo, atakayeshikwa atalipa faini mara tatu ya thamani ya Madini hayo na Madini hayo yatataifishwa na Serikali,” alisisitiza Naibu Waziri Nyongo.

Naibu Waziri aliongeza kwamba, katika kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli la kufungua masoko ya Madini nchini,  tayari jumla ya masoko 13 ya Madini  yamekwishafunguliwa nchi nzima  na kueleza kuwa, bado Mikoa michache iko katika hatua za mwisho za kukamilisha  uanzishwaji wa masoko hayo.

Pia, aliwahakikishia wananchi wa Kyerwa na Kagera kwa ujumla kuwepo kwa ajira kupitia soko hilo lililozinduliwa na hivyo kuwataka kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo katika soko hilo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali, Marco Gaguti alisema ataendelea kushirikiana na Wizara ya Madini katika kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji wa Madini ya Tin ikiwemo nishati ya umeme pamoja na mitaji kwa wachimbaji wadogo ili kuwawezesha kuongeza uzalishaji.

Brigedia Jenerali, Gaguti aliongeza kuwa, hivi sasa kuna takriban wachimbaji 1234 wa Madini ya Bati katika Wilaya ya Kyerwa, lakini bado uzalishaji haujakidhi matakwa ya kuelekea kwenye uchumi wa kati ikiwemo uzalishaji wa Tin kwa kiwango kikubwa na kinachotegemewa kama malighafi kwenye viwanda kwaajili ya hatua nyingine.