Tume ya Madini iliundwa kwa mujibu wa kifungu cha 21 cha Sheria ya Marekebisho Anuwai ya Sheria ya Madini Na. 7 ya Mwaka 2017. Mnamo tarehe 17 Aprili, 2018, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. John Pombe Joseph Magufuli, kulingana na Sheria tajwa, aliteua Mwenyekiti na Makamishna wa Tume ya Madini. Ili kutekeleza majukumu yake, Tume ilifanya kikao chake cha kwanza tarehe 30 Aprili, 2018 Jijini Dodoma. Pamoja na mambo mengine, Tume iliazimia mambo  yafuatayo:

i) Ofisi za Makao Makuu ya Tume ya Madini zitakuwa Jijini Dodoma katika Ofisi za Wizara ya Madini;

ii) Kuimarisha usimamizi wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na marekebisho yake ya Mwaka 2017 kwa lengo la kuhakikisha kuwa Serikali inamiliki hisa zisizopungua asilimia 16 ya mtaji wa Kampuni zinazomiliki migodi ya kati (MLs) na mikubwa (SMLs), Wazawa wanashirikishwa ipasavyo katika Miradi ya Madini na kunufaisha jamii katika maeneo ya migodi na Taifa kwa ujumla;

iii) Kuwajulisha wamiliki wote wa leseni zote za kuhodhi maeneo (Retention Licences – Jedwali Na. 1) kuwa leseni zao zimefutwa kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 ikisomwa pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2017 na Kanuni ya 21 ya Kanuni za Madini (Haki Madini), 2018 Tangazo la Serikali Na.1/2018 na kwamba maeneo ya leseni hizo yamerudishwa Serikalini bila hakikisho la kupewa tena;

>>Soma Zaidi>>