Na Nuru Mwasampeta -Geita

 

Waziri wa Madini, Doto Biteko amewaasa wachimbaji wadogo wa Madini wilayani Bukombe mkoani Geita kuepuka kujihusisha na shughuli za uchimbaji wa Madini bila ya kutumia vifaa vya usalama ili kujiepusha na maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu.

Waziri Biteko Alitoa kauli hiyo leo tarehe 18 July,  2019 wakati wa makabidhiano ya pikipiki nne na bajaji 2  zilizotolewa ili kutumika katika kuchukua makohozi kutoka katika makazi ya wachimbaji wadogo wa Madini na wananchi wa Bukombe na kuyawasilisha katika maabara kwa uchunguzi.

Waziri wa Madini, Doto Biteko akipeana mkono na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe Said Nkumba mara baada ya kukabidhiwa vifaa vya usafiri na kuvikabidhi kwa Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Bukombe.

Makabidhiano hayo yamefanyika katika hospitali ya wilaya ya Bukombe yakishuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Said Nkumba, waugizi,  na viongozi wengine wa chama na Serikali.

Akizungumza kabla ya makabidhiano hayo,  Waziri Biteko alisema kutokana na takwimu kuonesha kuwa maambhkizi ya kifua kikuu kwa wananchi wa Bukombe hisusani wachimbaji wadogo wa Madini kuwa wa juu, hiyo ni dhahiri kuwa watu wa Bukombe hawako salama.

Aidha, alilishukuru shirika la SHIDEFA kwa kuamua kuingilia Kati na kutafuta namna rahisi ya kuwafikia waadhirika kwa lengo la kuwasaidia na kuwawezesha kupata tiba kwa wakati.

Akikabidhi vifaa hivyo vya usafiri kwa niaba ya bodi ya wakurugenzi wa shirika binafsi la SHIDEFA, mjumbe wa shirika hilo ambaye jina lake halikufahamika alisema kutokana na adhari kubwa ya ugonjwa wa kifua kikuu kwa wachimbaji wadogo na jamii ya eneo hilo wameona ni vema kutoa vifaa hivyo vya usafiri ili vitumike katika kufuata makohozi kwenye makazi ya watu na kuyapeleka maabara ili kufanyiwa uchunguzi.

Aidha,  afisa Huyo wa SHIDEFA alifafanua kuwa Mara baada ya vipimo kuonesha namna yoyote ya maambukizi wahusika wataanzishiwa tiba na hivyo kuokoa maisha ya watu.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Said Nkumba,  amewataka wataalamu wa afya kutumia vifaa hivyo kwa umakini mkubwa  ili kuwapa moyo wafadhili wa kuendelea kutoa misaada kwa ajili ya sekta ya afya na jamii kwa ujumla.