Na Nuru Mwasampeta,

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amewataka watumishi wa wizara kuhakikisha wanatoa huduma stahiki kwa watanzania ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Pombe Joseph Magufuli.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akiwa katika picha pamoja na makundi mbalimbali yaliyoshiriki mkutano wa wizara na hafla ya kuwaaga wastaafu kutoka Chuo Cha Madini (MRI) na Wizara ya Madini Makao Makuu

Aidha, amewataka watumishi hao, kila mmoja kulingana na majukumu yake  kujipima utendaji wake binafsi kabla ya kungoja vipimo vilivyopo kwa kuzingatia miongozo na taratibu za Utumishi wa Umma.

Naibu Waziri Nyongo, ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akifungua Mkutano wa Wafanyakazi wa Wizara kwa niaba ya Waziri wa Madini, Doto Biteko aliyekuwa katika utekelezaji wa majukumu mengine ya kitaifa.

Aidha, Nyongo amewaeleza watumishi hao kuwa wanao wajibu wa kuzingatia dhana nzima ya kuongeza ufanisi na tija katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku kwa manufaa ya Taifa na watanzania kwa ujumla.

Pamoja na rai ya kila mtumishi kujipima utendaji wake, Nyongo amewakumbusha kuzingatia matumizi ya Opras katika kutekeleza na kujipima namna kila mmoja anavyotekeleza majukumu yake. Amesema Opras ni hitaji la kisheria kila mmoja hanabudi kulizingatia.

“Wote tnafahamu kuwa ipo miongozo mbalimbali inayotumika katika utendaji wetu wa kila siku hivyo ni rai yangu kuwa tuizingatie ili kutoa huduma stahiki kwa watanzania kwa ufanisi na viwango vinavyotakiwa.” Alisisitiza .

Aidha, Nyongo alieleza wajibu wa Wizara kwa kuzingatia miongozo iliyopo ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira mazuri ya kazi yatakayowawezesha watumishi wake kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Pamoja na hilo, alikazia suala la kuwaendeleza watumishi, kuwajengea uwezo katika kazi zao pamoja na kushughulikia na kutatua changamoto zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi.

Zaidi ya hapo, Nyongo alisisitiza suala la kuimarisha mawasiliano baina ya watumishi wa wizara lakini pia mawasiliano baina ya wizara na taasisi zilizo chini ya wizara na wadau wote wa sekta ya madini ili kuongeza ufanisi hatimaye kuongeza tija katika utendaji wa wizara.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akiwa katika picha pamoja na makundi mbalimbali yaliyoshiriki mkutano wa wizara na hafla ya kuwaaga wastaafu kutoka Chuo Cha Madini (MRI) na Wizara ya Madini Makao Makuu

Kuhusu kuzingatia suala la afya za watumishi, Nyongo ameipongeza wizara kwa kuratibu mara kwa mara suala la upimaji wa afya kwa hiari kwa watumishi wake na kutoa rai kwa kila mmoja kutumia fursa hiyo na kujitokeza kupima afya zao kwa hiari.

Akihitimisha hotuba yake,  Nyongo amewasihi  watumishi wa wizara kuongeza juhudi na kuelekeza fikra zao katika kupelekea serikali ya viwanda kutokana na ukweli kwamba sekta ya madini ni mojawapo ya nguzo ya uchumi wa viwanda na kuwa itasaidia katika kuifikisha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kati ifikapo 2025.

Kutokana na uwepo wa wastaafu katika mkutano huo, Nyongo alitumia fursa hiyo kuwapongeza sana wastaafu watano walijumuika katika mkutano na hafla fupi ya kuwaaga na kuwatakia maisha mema katika hatua nyingine ya maisha.

Kwa uande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu Nsajigwa Kabigi kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila alisema mkutano huo umelenga katika kujadili masuala mbalimbali ya kiutendaji ya wizara ili kupata mwelekeo wa namna bora ya kuleta ufanisi katika kutekeleza majukumu na shughuli za kila siku za wizara pamoja na kubadilishana mawazo, kufurahi pamoja na kuwaaga wastaafu.