Na Tito Mselem, Tanga

Waziri wa Madini Doto Biteko ametembelea Machimbo ya Tanga Stone yaliyopo katika Kata ya Doda wilayani Mkinga mkoa wa Tanga kwa lengo la kukagua maendeleo na kusikiliza changamoto za wachimbaji hao.

Katika ziara hiyo, Waziri Biteko aliambatana na Viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Yona Maki, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dastan Kitandula ambaye pia ni Mbunge wa Mkinga Kitandula na viongozi wengine.

Wachimbaji katika eneo hilo ambapo shughuli za uchimbaji madini hayo zilianza miaka 25 iliyopita wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa miundombinu ya barabara, masoko ya madini hayo, ukosefu wa nishati ya umeme pamoja na ukosefu wa mitaji.

Akizungungumza na wachimbaji hao, Waziri Biteko aliwataka kuwa wavumilivu katika kipindi hiki ambapo serikali inaangalia namna ya kutatua changamoto zao.

Baadhi ya Madini ya Tanga Stone yakiwa yamekusanywa

Kwa upande wa changamoto ya Barabara, Waziri Biteko alipokea taarifa ya upembuzi yakinifu wa barabara ambapo inatarajiwa kuanza kutengenezwa mara baada ya kukamilika kwa upembuzi unaofanywa na Wataalamu wa Mamlaka ya Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).

Pia, Biteko alitoa ahadi kwa wachimbaji hao ya kuwatafutia masoko ya madini hayo ili yalete tija kwa wachimbaji na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mkinga Dastan Kitandula alimpongeza Waziri Biteko kwa kukubali kutembelea Machimbo hayo ya Tanga stone na kumuomba kupatiwa wataalamu watakao toa mafunzo kwa wachimbaji hao ili wanufaike zaidi na asilimali zao.