Na Bibiana Ndumbaro, STAMICO

Ziara ya Waziri wa Madini Angellah Kairuki (Mb) aliyoifanya tarehe 05.11.2018 katika Ofisi za Makao Makuu ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), imeleta tija, baada ya Waziri kuchangia shilingi milioni 24 ili kuongezea nguvu ya kutekeleza mradi Kokoto wa Shirika hilo; uliopo eneo la Ubenazomozi, mkoani Pwani.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila (kushoto) wakisalimiana na mwenyeji wao Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Kanali Mhandisi Sylvester Ghuliku wakati wa ziara ya Waziri katika Ofisi za Makao Makuu ya Shirika zilizopo Barabara ya Umoja wa Mataifa, Upanga jijini Dar es Salaam.

Kairuki alitoa mchango huo baada ya kuguswa na tatizo la ukosefu wa mitaji ya kutekeleza miradi, kama lilivyobainishwa katika taarifa ya utendaji kazi ya Shirika hilo iliyowasilishwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Kanali Mhandisi Sylvester Ghuliku; kwenye kikao cha pamoja baina ya Waziri, Wafanyakazi na Katibu Mkuu Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila.

Fedha hizo zitaiwezesha STAMICO kufikia bajeti yake ya Shilingi milioni 54 zinazohitajika kufanya utafiti wa kijiolojia unaolenga kubaini ubora wa mwamba katika eneo la Chigongwe, ambapo awamu ya kwanza ya mradi wa kokoto wa STAMICO itatekelezwa.

Waziri Kairuki aliwataka Wafanyakazi kukuza ubunifu na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi, huku akiwataka kuwasilisha maoni yao kuhusu namna ya kuboresha utendaji kazi wa STAMICO wenye tija kwa Watanzania na Taifa kwa ujumla.

Waziri huyo wa Madini Kairuki na Katibu Mkuu wake Prof. Msanjila, waliipongeza STAMICO kwa kuweka Menejimenti mpya katika Kampuni yake tanzu ya STAMIGOLD kwani imesaidia kujiendesha kwa faida, kuimarisha ulipaji madeni na kumudu gharama za uendeshaji mgodi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Kanali Mhandisi Sylvester Ghuliku alimshukuru Waziri Kairuki kwa ziara hiyo na ushirikiano anaoutoa kwa STAMICO ili kuhakikisha Shirika linakua kwa kasi na kuleta manufaa mapana kwa Taifa na kwa maendeleo ya Watanzania.

Kanali Mhandisi Ghuliku alimhakikikishia Waziri kuwa STAMICO imedhamiria kuleta mabadiliko katika miradi yake kwa kuboresha miundo mbinu ya miradi, mifumo ya uangalizi na ufuatiliaji na kupunguza gharama za uendeshaji migodi ili kuongeza faida na tija kwa Taifa.

Akitoa neno la shukrani, Kaimu Mkurugenzi wa Fedha wa STAMICO Meja Luyodrey Masaki amesema kikao hicho cha pamoja na Mhe. Waziri kimekuwa kichocheo cha uwajibikaji kama Shirika na kwa mtu mmoja mmoja na amemuahidi kuwa STAMICO itarekebisha mapungufu yake na kutoa maoni ya maboresho Wizarani, ili kuleta tija kwa Shirika.

Baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya STAMICO na Wafanyakazi wakimsikiliza Waziri wa Madini Angellah Kairuki (hayupo pichani) alipotembelea Shirika la Madini la Taifa, tarehe 5 Novemba 2018 katika ofisi za Makao Makuu ya STAMICO zilizopo barabara ya Umoja wa Mataifa, Upanga jijini Dar es Salaam na kufanya kikao nao.

Meja Masaki alimshukuru Kairuki kwa mchango wake wa Shilingi milioni 24 ambazo zitasadia kutekeleza mradi wa kokoto wa Ubenazomozi, na hivyo kuwezesha kukidhi mahitaji ya kokoto katika miradi ya  miundombinu ya barabara, reli, bandari na viwanja vya ndege, sambamba na majengo ya biashahara, ofisi na makazi.

Mapema mwezi huu Novemba, Waziri huyo wa Madini aliitembelea STAMICO ikiwa ni ziara yake ya pili kwa mwaka 2018; iliyolenga kufuatilia utendaji kazi wa Shirika, changamoto zake, mbinu utatuzi na mwelekeo wa uendeshaji Shirika kwa kasi itakayoleta matokeo chanya nchini.