[Latest Updates]: Biteko akamata tani saba za madini ya vito yaliyofichwa ndani

Tarehe : July 13, 2018, 4:34 a.m.
left

Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko amekamata madini  ya vito aina ya Rhodilite yenye uzito wa takribani tani saba yaliyokuwa yamefichwa nyumbani kwa mchimbaji wa madini hayo, Juvenal Mnene ambaye ni mmiliki wa kampuni ya J. J. Mnene & Partners na kuamuru kukabidhiwa Serikalini pamoja na mmiliki huyo kufikishwa mahakamani.

Sehemu ya madini ya vito aina ya Rhodilite yaliyokamatwa nyumbani kwa mchimbaji Juvenal Mnene katika mtaa wa Magoweko kwenye halmashauri ya mji wa Gairo mkoani Morogoro.[/caption]

Naibu Waziri Biteko amekamata madini hayo katika ziara yake aliyoifanya katika wilaya ya Gairo mkoani Morogoro lengo likiwa ni kukagua shughuli za wachimbaji wadogo  wa madini ya vito na ujenzi na kutatua changamoto mbalimbali.

Katika ziara hiyo, Biteko aliambatana na watendaji kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini, Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Gairo, Madiwani na Mwakilishi wa Mbunge wa Gairo.

Mara baada ya kuwasili katika mgodi wa mchimbaji huyo uliopo eneo la Rubeho, Bitteko alibaini kuwa  mchimbaji huyo alikuwa amelipa mrabaha wa shilingi 400,000 tu tangu mwaka 2013 ndipo akataka kupewa taarifa ya uzalishaji  na kiasi cha malipo yaliyolipwa serikalini ikiwa ni pamoja na kodi mbalimbali ambapo alielezwa na mmiliki wa mgodi huo Juvenal Mnene kuwa  taarifa ya uzalishaji wa madini hayo na vielelezo vya malipo yaliyofanyika serikalini ipo nyumbani.

Naibu Waziri Biteko pamoja na msafara wake alielekea nyumbani kwa mmiliki wa mgodi huo, ambapo alishuhudia madini ya vito aina ya Rhodilite yakiwa yamerundikwa kwenye chumba kimoja na kufungwa kwa kufuli bila kuwekwa lakiri (seal) ya serikali kinyume na sheria ya madini inavyotaka.

“Huu ni utoroshwaji wa madini kwasababu haiwezekani madini yahifadhiwe ndani ya chumba bila serikali kufahamu na kuweka lakiri, na kama serikali hatuwezi kukubali kuona madini yakitoroshwa nje ya nchi na wachimbaji wa madini wasio waaminifu,” alisema Biteko.

Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe (kushoto) akielezea shughuli za uchimbaji madini katika wilaya yake kwa Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (katikati) kwenye ziara yake katika eneo la Rubeho wilayani Gairo mkoani Morogoro tarehe 11 Julai, 2018.[/caption]

Katika hatua nyingine, Biteko alibaini mchimbaji huyo alikuwa na mtambo wa kuchenjua madini hayo  nyumbani kwake kwa nyuma bila kuwa na leseni ya uchenjuaji madini kama sheria ya madini inavyotaka.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya tukio hilo, Naibu Waziri Biteko alimwagiza Mkuu wa Polisi Wilaya ya Gairo, Musa Mwakasula kwa kushirikiana na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Morogoro kukamata madini hayo kuyapima ili kujua kiasi chake halisi na kisha kumfikisha mtuhumiwa katika vyombo vya sheria.

Aliongeza kuwa Wizara ya Madini itawachukulia hatua kali za kisheria watu wote waliohusika na mchakato mzima wa kuficha madini hayo.

“Haiwezekani kabisa juzi juzi  tumekamata madini yenye uzito wa tani 75 jijini Dar es Salaam, ni lazima tuhakikishe tunalinda rasilimali za madini kwa nguvu zote ili ziwe na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi,” alisisitiza Biteko.

Wakati huo huo, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kichangani kilichopo wilayani Gairo mkoani Morogoro, Naibu Waziri Biteko alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli kupitia Wizara ya Madini imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa sekta ya madini inakuwa na mchango mkubwa wa uchumi wa nchi kwa kuboresha sheria za madini.

Alifafanua kuwa, Wizara ya Madini ipo katika mchakato wa kurasimisha  wachimbaji wadogo kwa kuwapatia leseni  mara baada ya taratibu kukamilika ili kuondokana na umaskini kutokana na kujiajiri.

Mchimbaji madini aliyekamatwa akiwa amehifadhi madini aina ya Rhodilite yenye uzito wa takribani tani saba nyumbani kwake, Juvenal Mnene (katikati) akionyesha nyaraka mbalimbali kwa Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko.

Alisema kuwa, awali rasilimali za madini zilichukuliwa kama umiliki wa wawekezaji wa nje ya nchi lakini mara baada ya maboresho ya Sheria ya Madini wananchi sasa wana haki zote za umiliki wa rasilimali za madini.

Akizungumzia suala la bei elekezi kwenye madini ya ujenzi, Biteko alisema Serikali ipo katika mpango wa kukaa na wanunuzi wa madini hayo hasa wenye viwanda vya kutengeneza marumaru( tiles) na kukubaliana bei ambayo itafanywa kuwa bei elekezi ya madini hayo ili wananchi wanufaike.

Katika hatua nyingine, Biteko aliwataka wachimbaji hao kulipa kodi mbalimbali na kufuata kanuni na sheria za uchimbaji madini.

Wakati huo huo akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe alieleza changamoto mbalimbali katika uchimbaji madini katika wilaya yake kuwa ni pamoja na wachimbaji wadogo wa madini kutokuwa na leseni kwa kisingizio wameshawasilisha maombi yao kwenye ofisi za madini, kutokuwepo kwa utaratibu mzuri wa uchimbaji madini na kutokuwepo kwa sehemu za kuhifadhia madini.

Aliendelea kusema  changamoto nyingine kuwa ni pamoja na ukosefu wa mitaji hususan kwa wachimbaji wadogo wa madini na upatikanaji wa soko la uhakika la madini hayo.

Imeandaliwa na:

Greyson Mwase, Morogoro

Afisa Habari,

Wizara ya Madini,

Kikuyu Avenue,

P.O Box 422,

40474 Dodoma,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,

BaruaPepe: info@madini.go.tz,                                             

Tovuti: madini.go.tz

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals