Tarehe : Feb. 6, 2026, 3:18 p.m.
TAARIFA KWA UMMA
TANZANIA KUIMARISHA NAFASI YAKE KATIKA SEKTA YA MADINI KUPITIA MKUTANO WA MINING INDABA 2026
Februari 6, 2026 – Dodoma
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, anatarajiwa kuongoza Ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano wa Kimataifa wa Mining Indaba 2026 utakaofanyika jijini Cape Town, Afrika Kusini, kuanzia tarehe 8 hadi 12 Februari 2026.
Ujumbe huo utajumuisha wataalamu kutoka Wizara ya Madini na Taasisi zake, Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA), pamoja na wadau wa Sekta binafsi wakiwemo Chemba ya Madini Tanzania (TCM), Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Tanzania (FEMATA), Umoja wa Vijana Wachimbaji Tanzania (TYM), Chama cha Wachimbaji Madini Wanawake Tanzania (TAWOMA), Kampuni za uchimbaji madini, taasisi za fedha, watoa huduma migodini na wadau wengine katika mnyororo wa thamani wa madini.
Ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa Mining Indaba 2026 ni sehemu ya mkakati wa Taifa wa kujiweka kama mshirika muhimu katika mnyororo wa kimataifa wa uzalishaji wa madini, hususan katika kipindi ambacho Afrika, ikiwemo Tanzania, inaendelea kutambuliwa kama mhimili muhimu wa uzalishaji wa madini yanayohitajika kwa nishati safi na maendeleo ya viwanda duniani.
Katika mkutano huo, Mhe. Mavunde anatarajiwa kushiriki Kikao cha Mawaziri wa Madini kilichoandaliwa na Waziri wa Rasilimali za Madini na Petroli wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Gwede Mantashe, pamoja na kushiriki mijadala ya ngazi ya juu itakayowakutanisha mawaziri, wakurugenzi wakuu wa kampuni kubwa za madini duniani, wawekezaji na taasisi za fedha. Mijadala hiyo itajikita katika ubunifu wa kisera, maendeleo ya sekta ya madini, mazingira ya uwekezaji, uhamasishaji wa mitaji na fursa katika madini muhimu na madini mkakati barani Afrika.
Aidha, Mhe. Mavunde atafanya mikutano ya kimkakati na wadau muhimu wakiwemo wawekezaji kutoka Marekani, Umoja wa nchi za Ulaya na Canada kwa lengo la kuvutia uwekezaji mpya na kuimarisha ushirikiano uliopo. Vilevile, wawekezaji waliowekeza nchini wanatarajiwa kufanya vikao na Waziri pamoja na kushiriki vikao katika mkutano huo.
Kadhalika, wadau kutoka vyama vitakavyoshiriki mkutano huo wanatarajiwa kushiriki vikao na wadau mbalimbali kwa lengo la kutafuta washirika wa kufanya nao kazi na kujitangaza.
Mkutano wa mwaka 2026 utaongozwa na kaulimbiu “Tuna Nguvu: Maendeleo Kupitia Ushirikiano” inayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, Sekta binafsi na taasisi za maendeleo katika kujenga sekta ya madini endelevu, shindani na yenye tija kwa maendeleo ya Afrika.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini; Wizara ya Madini
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.