[Latest Updates]: Vyombo vya Ulinzi Vyatakiwa Kuandaa Mtandao wa Usimamizi Madini Nchini

Tarehe : Feb. 11, 2020, 9:06 a.m.
left

  • Waziri Biteko avipongeza kwa mchango wake kwenye  Mafanikio Ukusanyaji Maduhuli

Asteria Muhozya, Greyson Mwase na Tito Mselem, Dodoma

Vyombo vya Ulinzi na Usalama vimetakiwa kuandaa Mtandao wa Kusimamia Rasilimali Madini Nchini hususan kwenye udhibiti wa Utoroshaji rasilimali hizo kutokana na mchango wa vyombo hivyo katika ukuaji na Maendeleo ya Sekta ya Madini.

Aidha, vimetakiwa kuweka mazingira salama ya wawekezaji katika sekta husika ili kuhakikisha waliopo wanaendelea kufanya shughuli zao vizuri bila kubugudhiwa huku vikitakiwa kuhakikisha mazingira salama yatakayovutia wawekezaji  wapya katika Sekta ya Madini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,  Uratibu , Bunge,  Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenister Mhagama mapema leo   Januari 25, 2020 Jijini Dodoma, wakati akifungua Semina  kuhusu Ushiriki  wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama katika Usimamizi na Udhibiti wa Rasilimali Madini.

Mhagama amesema  kuwa, mabadiliko makubwa ya Kisera, Sheria, na Taratibu yaliyofanyika katika Sekta ya Madini yamepelekea mabadiliko makubwa katika mageuzi ya Sekta ya Madini huku akimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kwa kuwezesha na kusimamia mabadiliko hayo  na  kuipongeza Wizara ya Madini kwa  usimamizi dhabiti ambao umewezesha mafanikio yanayoonekana katika sekta ikiwemo uanzishwaji wa  masoko ya madini.

Vilevile, amewataka washiriki hao kuhakikisha wanatoka na maazimio kutoka katika semina hiyo, ambayo yataendelea kuivusha Sekta ya Madini katika kufikia Malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 huku akiitaka Wizara ya Madini kuandaa semina kama hiyo kwa Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama na Taasisi nyingine za Umma ikiwemo Uhamiaji, taasisi zinazohusika na masuala ya ajira, Halmashauri za Wilaya na Majiji na wadau wengine muhimu katika sekta ya madini lengo likiwa ni kuifungamanisha sekta ya madini na sekta nyingine.

‘’ Kazi yetu ni moja tu, kuhakikisha tunafungamanisha sekta hii na sekta nyingine ili kuhakikisha sheria na taratibu zote zilizowekwa katika sekta hii zinasimamiwa na kutekelezwa kikamilifu,’’ amesema Waziri Mhagama.

Naye, Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza katika semina hiyo amesema kwamba,  Wizara iliona ipo haja ya hukakikisha wasimamizi wote wa Sekta ya Madini wanakutana  ili kuwa na uelewa unaofanana katika usimamizi wa sekta  ili kuboresha utendaji kazi na  kuongeza  manufaa zaidi kwa sekta husika.

Akielezea mafanikio yaliyopatikana mara baada ya kufanyika kwa marekebisho ya Sheria ya Madini ameeleza kuwa, ni pamoja na kuimarishwa kwa usimamizi kwenye Sekta ya Madini hali iliyopelekea kuvuka kwa lengo la makusanyo  kwa kipindi cha Nusu mwaka wa Mwaka wa Fedha 2019/20  ambapo Wizara  imekusanya kiasi cha shilingi bilioni  242 sawa na asilimia 103,   na kuongeza kuwa, yamechagizwa na ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali wa madini vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama.

Pia, Waziri Biteko amesema kuwa, mapato na uzalishaji wa madini mbalimbali ikiwemo dhahabu, almasi na tanzanite yameongeza nchini tofauti na ilivyokuwa awali na kusema kuwa, thamani ya madini ya dhahabu kwenye soko la Geita imefikia thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 238 kwa nusu mwaka tofauti na awali huku madini ya tanzanite yakiiwezesha serikali kukusanya mapato ya shilingi bilioni 2 baada ya kujengwa ukuta kuzunguka migodi ya tanzanite Mirerani kutoka makusanyo ya shilingi milioni 71 kabla ya kujengwa kwa ukuta.

Ameongeza kuwa, uzalishaji wa madini ya almasi katika Mgodi wa Mwadui Shinyanga umeongezeka kufikia karati Laki Nne ukiwa ni uzalishaji mkubwa tangu kuanzishwa kwa mgodi huo, na hivyo kuyafanya madini hayo kuwa ya pili katika uchangiaji wa makusanyo ya maduhuli ya Serikali yakiongozwa na madini ya dhahabu ambayo yanachangia kwa asilimia 86.

‘’Ndugu washiriki yapo mafanikio mengi yanayoonekana katika sekta hii, na yote yamechangiwa na championi wa mabadiliko hayo ambaye ni Rais Dkt. John Magufuli,’’ amesema Waziri Biteko.

Katika hatua nyingine, Waziri Biteko amevipongeza vyombo hivyo kutokana na mchango wao katika maendeleo ya Sekta ya Madini na kueleza kuwa, Wizara imejipanga kuhakikisha vyombo hivyo katika ngazi zote vinafikiwa  ili kupatiwa elimu  kuhusu sekta husika.

Kwa upande wake, Kamishna wa Polisi Utawala na Rasilimali Watu, Benedict Mwakulyamba akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, amemweleza Waziri Mhagama kuwa, vyombo hivyo ambavyo vinasimama kama daraja katika usimamizi wa rasilimali hivyo vitahakikisha vinasimamia rasilimali hiyo ili kukuza uchumi wa nchi na maendeleo ya taifa.

Huku akinukuu kauli ya Rais Dkt. John Magufuli kwamba ‘Tanzania si  maskini’ amesema itaungwa mkono na vyombo hivyo kwani inatoa dira  na mwelekeo wa usimamizi wa rasilimali madini katika kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa nchi inayojitegemea  kutokana na uwepo wa rasilimali madini.

Awali, akizungumza katika semina hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila amesema kuwa, semina hiyo imelenga katika kujadili na kutafakari masuala mbalimbali yanayohusu sekta hiyo ili kuboresha na kuongeza tija zaidi.

Semina hiyo ya Siku mbili inayofanyika Jijini Dodoma inavishirikisha vyombo mbalimbali vya Ulinzi na Usalama kutoka Mikoa yote nchini.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals