[Latest Updates]: Wachimbaji Wanawake, Vijana Undeni Vikundi - Dkt. Kiruswa.

Tarehe : Aug. 29, 2023, 8:39 a.m.
left

 

#Awataka kujiunga na FEMATA ili kunufaika na Benki inayoanzishwa.

Dodoma.

Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amewataka wanawake na vijana wanaojishughulisha na uchimbaji wa madini katika wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara kujiunga kwenye vikundi na kusajiliwa katika Halmashauri husika na kwamba kufanya hivyo itakuwa rahisi kuwahudumia na kuwasaidia kupatiwa leseni za uchimbaji na mikopo kutoka Halmashauri husika na hata mabenki.

Dkt. Kiruswa amesema hayo, Agosti 29, 2023 Bungeni, jijini Dodoma wakati akijibu swali namba 12 la Mbunge wa jimbo la Lulindi, Mhe. Issa Ally Mchungahela aliyeuliza swali kuhusu namna gani Serikali itawasaidia Wanawake na Vijana wa Kata za Mitesa na Nanjota wanaojihusisha na uchimbaji Madini Lulindi.

Akijibu swali hilo, Dkt. Kiruswa amesema kuwa Mkoa wa Mtwara umebarikiwa kuwa na madini mbalimbali yakiwemo Madini ya Ujenzi ambayo huchimbwa zaidi na wananchi hasa Wanawake na Vijana. Aidha, Tume ya Madini, imetoa leseni za uchimbaji Madini ya Ujenzi na Chumvi kwa vikundi 11 vya wanawake na vijana. 

Amevitaja vikundi hivyo kuwa ni pamoja na Mtazamo Group, Wazawa Camp, Mwambani Group, Wasikivu, Songambele Group, Tusaidiane, Nguvu Kazi Youth Group katika Halmashauri ya Mji wa Masasi; Kikundi cha Kiumante kilichopo katika Manispaa ya Mtwara – Mikindani; Vikundi vya Makonde Salt Group, Mapinduzi na Umoja wa Vijana vilivyopo katika Halmashauri ya Mtwara Vijijini.

“Ili kuweza kuwasaidia wanawake na vijana wanaojishughulisha na uchimbaji wa madini katika Kata za Mitesa na Nanjota, tunawashauri Wanawake na Vijana wajiunge kwenye vikundi na kusajiliwa katika Halmashauri husika. Kufanya hivyo itakuwa rahisi kuwahudumia na kuwasaidia kupatiwa leseni za uchimbaji na mikopo kutoka Halmashauri husika na hata mabenki.” amesema Dkt. Kiruswa.

Dkt. Kiruswa amesema kuwa Wizara ya Madini itaendelea kutoa elimu kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha kujiunga katika vikundi ili kuweza kupatiwa huduma kwa ufanisi na kwa haraka zaidi.

Aidha, akijibu swali la nyongeza la Mhe. Mchungahela, Dkt. Kiruswa amesema kuwa ni kweli changamoto kubwa ya vijana, wanawake na watu mbalimbali wanaojihusha na uchimbaji wa madini ni ukosefu wa mitaji.

Aidha, ameongeza kuwa katika kutanzua changamoto hiyo Wizara ya Madini kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) wameweka wakfu kuwa walezi wa Wachimbaji Wadogo na katika hatua za awali za kuwasaidia wamewapa elimu kuhusu namna ya kufanya uchimbaji wa Madini kwa tija pamoja na kufahamu Sheria ya Madini.

“Lakini pia kuingia katika makubaliano na taasisi za kifedha hapa nchini ikiwemo NMB, CRDB na Benki ya Tanzania ili waweze kuwakopesha wale ambao wamekidhi vigezo” amesema Dkt. Kiruswa.

Pia, amesema kuwa, wachimbaji hao wanapaswa kujiunga na Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) ambao sasahivi wako kwenye mchakato wa kuanzisha benki yao ili waweze kufanya shughuli zao kwa urahisi zaidi na ufanisi.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals