Tarehe : June 28, 2025, 2:43 p.m.
Ni baada ya Tume ya Madini kukusanya zaidi ya Shilingi Trilioni Moja kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ikiwa ni asilimia 106.3 ya lengo
Yajipanga kuvuka lengo la Shilingi Trilioni 1.2 kwa mwaka wa fedha 2025/2026
DODOMA
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet R. Lekashingo amesema kuwa siri ya kukusanya Shilingi Trilioni 1.063 ikiwa ni asilimia 106.3 ya lengo la Shilingi Trilioni Moja katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 ni pamoja na uongozi imara na ubunifu kwenye ukusanyaji wa maduhuli.
Dkt. Lekashingo amesema hayo leo Juni 29, 2025 jijini Dodoma kwenye ufunguzi wa kikao cha menejimenti ya Tume ya Madini kilichoshirikisha Kamishna wa Tume ya Madini, Dkt. Theresia Numbi, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, Wakurugenzi, Mameneja na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa.
Amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 Tume ya Madini iliweka mikakati ya ukusanyaji wa maduhuli ikiwa ni pamoja na kuongeza ubunifu kwenye ukusanyaji wa maduhuli kwenye maeneo ya uchimbaji wa madini, uchenjuaji na biashara ya madini kupitia masoko ya madini 43 na vituo vya ununuzi wa madini 109 ambayo utekelezaji wake umepelekea mafanikio makubwa kwenye ukusanyaji wa maduhuli.
Ameendelea kusema kuwa mikakati mingine iliyofanikisha ukusanyaji wa maduhuli ni pamoja na kudhibiti utoroshaji wa madini.
Wakati huohuo, Dkt. Lakashingo amempongeza Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo kwa uongozi imara pamoja na imani aliyoijenga kwa viongozi waliopo chini yake hali iliyopelekea kufanya kazi kwa kujiamini huku wakizingatia Sheria ya Madini na Kanuni zake.
Pia amewataka viongozi hao kuendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha Tume inaendelea kuvuka lengo la kukusanya Shilingi Trilioni 1.2 katika kipindi cha mwaka ujao wa fedha 2025/2026.
Wakati huohuo akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo ameongeza kuwa ili kuongeza kasi ya ukusanyaji wa maduhuli katika mwaka ujao wa fedha, Tume imepanga kufanya maboresho ya mazingira ya kazi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa katika Mikoa ya Kimadini ya Rukwa, Songwe na Mahenge na kuendelea kununua viwanja kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa.
“Ninawaasa Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuendelea kuweka na kutekeleza mikakati mipya ya ukusanyaji wa maduhuli kwa ubunifu, lengo kuhakikisha Sekta ya Madini inaendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa,” amesisitiza Mhandisi Lwamo.
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.