[Latest Updates]: Kamati ya Bunge yatembelea Mgodi wa Buhemba na CATA Mining

Tarehe : March 22, 2018, 8:45 a.m.
left

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imetembelea na kukagua Mgodi wa Buhemba na ule wa CATA Mining Ltd iliyopo mkoani Mara ikiwa katika ziara ya kazi Machi 15 mwaka huu.

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila (kushoto) wakishiriki katika ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, katika Mgodi wa CATA Mining mkoani Mara, Machi 15 mwaka huu.[/caption]

Katika Mgodi wa Buhemba, Kamati ilielezwa kuwa, Serikali iliukabidhi Mgodi huo wa dhahabu kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) mwaka 2011 ili iuendeleze, kutoka kwa mmiliki wake wa awali ambaye ni Kampuni ya Meremeta Limited.

Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Kanali Mhandisi Sylivester Ghuliku, aliieleza Kamati kuwa Shirika limekamilisha upembuzi yakinifu katika mabaki ya dhahabu yaliyoachwa kipindi cha nyuma ambapo umebaini kuwapo takribani tani 796,400 za mabaki ya mchanga wa dhahabu yenye wastani wa kilo 852 za dhahabu.

“Aidha, upembuzi huo ulibaini kuwa mabaki hayo ya mchanga yatachenjuliwa kwa kutumia teknolojia ya Carbon in Leach (CIL). Mtambo unatarajiwa kuchakata mabaki ya mchanga wa dhahabu kiasi cha tani 246,240 kwa mwaka,” alisema.

Aliongeza kuwa, tathmini ya kiuchumi ya mradi imeonesha gharama za uwekezaji zinakadiriwa kufikia Dola milioni 3.96 na kwamba gharama za uendeshaji kwa mwaka zinakadiriwa kufikia Dola milioni 4.46 na kutarajiwa kuingiza faida inayofikia Dola milioni 3.45 kwa mwaka.

Kuhusu tathmini ya mashapo katika miamba migumu, Kamati ilielezwa kuwa taarifa za kitaalam zinaonesha kwamba wakati Kampuni ya Meremeta inafunga uzalishaji katika mgodi, kiasi cha wakia 600,000 zilisalia kwenye miamba migumu.

Akifafanua zaidi, alisema kuwa STAMICO imeamua kufanya upya tathmini ya mashapo hayo ili kujiridhisha. “Hadi sasa kiasi cha mashapo yenye wakia 441,772 kimethibitika kuwemo kwenye miamba migumu kutoka katika migodi ya wazi. Ukadiriaji wa mashapo unaendelea,” alisema.

Wajumbe mbalimbali wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakizungumza wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Migodi ya Madini ya Buhemba na CATA Mining iliyopo mkoani Mara, Machi 15 mwaka huu.[/caption]

Vilevile, ilielezwa kuwa Shirika lilifanikiwa kuchoronga shimo moja katika eneo la Nyasanero ili kutathmini mkanda mpya wa dhahabu. Tathmini kamili ya kiasi cha dhahabu kilichopo kwenye mwamba itakamilika mara baada ya kupokea majibu ya maabara.

Akieleza zaidi, alisema kuwa Januari mwaka huu, Shirika lilitangaza zabuni ya kumpata mbia wa kushirikiana naye katika kuendesha mradi kwa njia ya ushindani. Alisema, tayari Kampuni tatu zimenunua zabuni husika na kwamba uchambuzi wa zabuni hizo unaendelea.

Katika Mgodi wa CATA Mining Company Limited, Kamati ilielezwa kuwa Mgodi huo unamilikiwa kwa ubia kati ya Mtanzania, Mahuza Mumangi na Raia wa Canada Stefan Nagy kwa uwiano wa asilimia 50 kwa 50.

Akitoa taarifa kwa Kamati ya Bunge kuhusu Mgodi huo, Kamishna Msaidizi wa Madini, Ofisi ya Madini Musoma, Samwel Mayuki alisema kuwa Kampuni inamiliki leseni sita za uchimbaji mdogo katika eneo la Kataryo ambapo kuna miundombinu mbalimbali ikiwemo mitambo ya kusaga na kuchenjua madini.

“Kuanzia Julai 2016 hadi Juni 2017, Mgodi umezalisha kilo 241.3 za dhahabu zenye thamani ya Dola 8,880,240.57 sawa na wastani wa shilingi bilioni 19.5 za Tanzania. Mrabaha uliolipwa ni Dola 355,209.66 sawa na shilingi milioni 781 za Tanzania,” alisema Mayuki.

Aidha, Kamishna Mayuki aliongeza kuwa, kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Novemba 2017 Mgodi umezalisha kilo 62.4 za dhahabu zenye thamani ya Dola 2,239,659.86 sawa na shilingi bilioni 4.9 za Tanzania. Kiasi cha mrabaha na ada ya ukaguzi wa madini kilicholipwa ni Dola 134,388.56 na Dola 22,396.57 sawa na wastani wa shilingi milioni 295.7 za mrabaha na milioni 49.3 za ada ya ukaguzi.

Vilevile, alisema Mgodi umeajiri jumla ya wafanyakazi 351 ambao kati yao 318 sawa na asilimia 91 ni watanzania.

Hata hivyo, ilielezwa kuwa changamoto kubwa inayoukabili Mgodi kwa sasa ni kusimamishwa kwa shughuli za Mgodi kuanzia Juni 2017 kutokana na mgogoro baina ya wawekezaji husika na Jeshi la Wananchi wa Tanzania ambao ni wamiliki wa eneo hilo la uchimbaji.

Wajumbe mbalimbali wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakizungumza wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Migodi ya Madini ya Buhemba na CATA Mining iliyopo mkoani Mara, Machi 15 mwaka huu.[/caption]

“Hali hiyo imesababisha hasara mbalimbali ikiwemo kusimama kwa ajira za watanzania 318, kushindwa kurejesha mikopo ya Benki na hasara ya kupoteza mapato ya mamilioni ya shilingi kutokana na kusimama kwa uzalishaji.”

Kamati iliiagiza Wizara kuhakikisha inasaidia katika kushughulikia mgogoro huo ili shughuli za uzalishaji katika Mgodi zirejee mapema.

Viongozi mbalimbali wa Wizara walishiriki ziara hiyo wakiongozwa na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, ambaye aliahidi kwa niaba ya Wizara kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Kamati.

Imeandaliwa na:

Veronica Simba, Mara

Afisa Habari,

Wizara ya Madini,

Kikuyu Avenue,

P.O Box 422,

40474 Dodoma,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,

BaruaPepe: info@madini.go.tz,                                             

Tovuti: madini.go.tz

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals