Tarehe : Feb. 6, 2026, 3:08 p.m.
Waziri Mavunde kushiriki kikao cha Mawaziri, kukutana na Wadau muhimu kutoka Marekani, Umoja wa Ulaya, Canada
Vyama vya Wachimbaji kutafuta washirika wa kibiashara
Na Wizara ya Madini, Dodoma
Tanzania inaendelea kujiimarisha kimkakati katika Sekta ya Madini kimataifa kufuatia ushiriki wake katika Mkutano wa Kimataifa wa Mining Indaba 2026 unaotarajiwa kufanyika jijini Cape Town, Afrika Kusini, kuanzia Februari 8 hadi 12, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Madini Februari 6, 2026, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, anatarajiwa kuongoza Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo utakaowakutanisha viongozi wa Serikali, Wawekezaji, Kampuni kubwa za madini na Taasisi za fedha kutoka mataifa mbalimbali duniani na wadau wengine.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa ushiriki wa Tanzania katika mkutano wa Mining Indaba 2026 ni sehemu ya mkakati wa Taifa wa kujiweka kama mshirika muhimu katika mnyororo wa kimataifa wa uzalishaji wa madini, hususan katika kipindi ambacho bara la Afrika, ikiwemo Tanzania, linaendelea kutambuliwa kama mhimili muhimu wa uzalishaji wa madini yanayohitajika kwa ajili ya nishati safi na maendeleo ya viwanda duniani.
Katika mkutano huo, Mhe. Mavunde anatarajiwa kushiriki Kikao cha Mawaziri wa Madini kilichoandaliwa na Waziri wa Rasilimali za Madini na Petroli wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Gwede Mantashe, pamoja na kushiriki mijadala ya ngazi ya juu itakayowakutanisha mawaziri wa madini, wakurugenzi wakuu wa kampuni kubwa za madini duniani, wawekezaji na taasisi za fedha.
“Mijadala hiyo itajikita katika masuala ya ubunifu wa kisera, mikakati ya maendeleo ya sekta ya madini, uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji, uhamasishaji wa mitaji, pamoja na fursa zilizopo katika madini muhimu na madini mkakati barani Afrika,” imesema taarifa hiyo.
Aidha, Waziri wa Madini anatarajiwa kufanya mikutano ya kimkakati na vikao vya pembeni na wadau muhimu wakiwemo wawekezaji kutoka Marekani, Umoja wa nchi za Ulaya na mataifa mengine kwa lengo la kuvutia uwekezaji mpya, kuimarisha ushirikiano na wawekezaji waliopo pamoja na kujenga mahusiano ya kibiashara.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa wadau watakaoambatana na Mhe. Mavunde wanatarajiwa kushiriki vikao mbalimbali na wadau wa kimataifa kwa lengo la kutafuta washirika wa kibiashara, kubadilishana uzoefu na kujitangaza katika masoko ya kimataifa.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo utajumuisha wataalamu kutoka Wizara ya Madini na taasisi zake, Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA), pamoja na wadau wa sekta binafsi wakiwemo Chemba ya Madini Tanzania (TCM), Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Tanzania (FEMATA), Umoja wa Vijana Wachimbaji Tanzania (TYM), Chama cha Wachimbaji Madini Wanawake Tanzania (TAWOMA), kampuni za uchimbaji madini, taasisi za fedha, watoa huduma migodini, wafanyabiashara na wadau wengine katika mnyororo wa thamani wa madini.
Kupitia jukwaa hilo, Tanzania inatarajia kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini huku ikisisitiza dhamira ya Serikali ya kuongeza thamani ya madini ndani ya nchi na kuhakikisha sekta ya madini inachangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi, uanzishaji wa ajira na maendeleo ya wananchi.
Mkutano wa Mining Indaba 2026 utaongozwa na kaulimbiu isemayo “Tuna Nguvu: Maendeleo Kupitia Ushirikiano”, inayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na taasisi za maendeleo katika kujenga sekta ya madini endelevu, shindani na yenye tija kwa maendeleo ya Afrika.
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.