[Latest Updates]: Tume ya Madini Kushirikiana na TRA Usimamizi wa Sekta ya Madini

Tarehe : March 11, 2021, 12:38 p.m.
left

Yajipanga kukusanya bilioni 600 mwaka wa fedha 2021-2022

Yaainisha mafanikio yake, masoko ya madini yaiingizia serikali bilioni 211.2 tangu kuanzishwa kwake Machi 2019

Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa Tume ya Madini kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeweka mikakati ya kushirikiana kwa pamoja kwenye Sekta ya Madini ili iwe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa Uchumi wa Nchi.

Mhandisi Samamba ameyasema hayo leo tarehe 11 Machi, 2021 katika kikao kati ya Tume ya Madini na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jijini Da es Salaam chenye lengo la kuangalia namna ya utekelezaji wa makubaliano kati ya TRA na Tume ya Madini ya utendaji kazi kwenye Sekta ya Madini ambayo yalisainiwa Septemba, 2020.

Alisema kuwa, ushirikiano kati ya Tume ya Madini na TRA utarahisisha usimamizi kwenye Sekta ya Madini hususan kwenye ukusanyaji wa maduhuli kwa kubadilishana taarifa za kodi mbalimbali zinazolipwa Serikalini.

Katika hatua nyingine akielezea mikakati ya Tume ya Madini kwenye ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka wa fedha 2021-2022, Mhandisi Samamba amesema Tume imeweka lengo la kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 600 na kuongeza kuwa lengo ni kuhakikisha mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa unakua na kufikia asilima 10 ifikapo mwaka 2025.

“Kama Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, menejimenti, maafisa madini wakazi wa mikoa na maafisa migodi wakazi tumeweka mikakati  mbalimbali ya kuhakikisha kasi ya  ukusanyaji wa maduhuli inazidi kuimarika,” alisema Mhandisi Samamba.

Katika hatua nyingine alimshukuru Waziri wa Madini, Doto Biteko, Naibu Waziri wa Madini, Profesa Shukrani Manya na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila kwa msaada kwenye utatuzi wa changamoto mbalimbali.

Wakati huo huo akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini, Venance Kasiki alisema kuwa tangu kuanzishwa masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini mapema Machi, 2019 Serikali ilipata kiasi cha shilingi bilioni 211.2 ikiwa ni kama mrabaha na kodi ya ukaguzi kupitia masoko ya madini yaliyopo kila mkoa wa Madini.

Alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa masoko ya madini nchini hali ya ukusanyaji wa maduhuli imeendelea kuimarika nchini kwa kuwa wachimbaji wadogo wa madini wameanza kuwa na uelewa wa umuhimu wa masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini.

Akielezea manufaa ya masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini vilivyoanzishwa alisema kuwa wachimbaji wadogo wa madini wanapata bei elekezi zinazoendana na soko la dunia na kufanya biashara ya madini kuwa na  faida.

“Zamani wachimbaji wadogo walikuwa wakifanya biashara ya madini kwa hasara kwa kuwa walikuwa wanadhulumiwa, lakini tangu masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini yameanzishwa, wachimbaji wadogo wameanza kuyatumia kwa kuuza madini yao kulingana na bei elekezi inayoendana na Soko la Dunia inayotolewa na Tume ya Madini na kulipa kodi mbalimbali Serikalini,” alisema Kasiki

Katika hatua nyingine, Kasiki aliongeza  manufaa mengine kuwa ni pamoja na kurahisisha ukusanyaji wa maduhuli kwa Serikali ambayo yanatumika kuendeleza Sekta nyingine.

Kikao hicho kilichoongozwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba kilihusisha watendaji kutoka Tume ya Madini, watendaji kutoka TRA wanaotoka katika Idara za walipa kodi wakubwa, walipa kodi wa kati na forodha ambacho lengo lake lilikuwa ni kujenga uelewa wa pamoja wa watendaji wa Tume ya Madini na TRA kwenye ukusanyaji wa maduhuli na kujadili changamoto mbalimbali zinazojitokeza wakati wa utekelezaji na kuzipatia ufumbuzi.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals