Tarehe : Dec. 28, 2017, 10:33 a.m.
Serikali imeagiza kufikia Januari 10, 2018 Ukaguzi wa Usalama kwenye eneo la Machimbo ya Dhahabu ya Buhemba, Wilayani Butiama Mkoani Mara uwe umekamilika ili shughuli za uchimbaji zilizokuwa zimesimamishwa ziruhusiwe.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo alitoa agizo hilo Desemba 27, 2017 alipofanya ziara kwenye eneo hilo ili kujionea hali halisi ya machimbo husika pamoja na kuzungumza na wachimbaji waliosimamishwa kuendeleza shughuli zao hadi hapo ukaguzi utakapokamilika.
“Ninasikitika kuona shughuli za uchumi kwenye eneo hili la Buhemba zimesimama kutokana na shughuli za uchimbaji kusimamishwa baada ya kutokea ajali,” alisema.
Serikali ilisitisha shughuli za uchimbaji Madini kwenye eneo hilo la Buhemba Februari 2017 baada ya kutokea vifo vya wachimbaji Watatu na wengine wapatao 15 kujeruhiwa kutokana na kufanya shughuli zao bila kuzingatia taratibu na kanuni za uchimbaji salama.
Nyongo alisisitiza kwamba mgodi huo hautofunguliwa hadi hapo zoezi la ukaguzi litakapokamilika. “Hatuwezi kuufungua mgodi huu leo hii bila kukamilisha zoezi la ukaguzi kwahiyo kabla ya Tarehe 10 mwezi ujao, Wakaguzi wawe wamekamilisha ili mgodi uanze kazi na shughuli za uchumi zilizokuwa zikifanyika mgodini hapa zirejee,” alisema.
Alisema shughuli hiyo ya Ukaguzi inapaswa kukamilika mapema ili maduara yasiyo salama yaweze kutambulika na yazuiwe na yaliyokuwa salama yafahamike na kuendelezwa.
Aidha, alikumbushia agizo alilotoa kwa Wakaguzi wa Migodi Desemba 14, 2017 Mkoani Tabora alipotembelea kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Nsungwa Gold Mine uliopo katika Kata ya Silambo Wilaya ya Kaliua la kukagua hali ya usalama na kuwasaidia Wachimbaji kuepusha ajali wakati wa utekelezaji wa shughuli zao.
“Ninawaagiza kwa mara nyingine Wakaguzi wa Migodi kuhakikisha mnatembelea maeneo ya migodi mara kwa mara ili kuepusha ajali,” aliagiza Naibu Waziri.
Naibu Waziri Nyongo yupo Mkoani Mara kwa ziara ya siku mbili ya kukagua shughuli za uchimbaji wa madini kwenye maeneo mbalimbali yenye migodi pamoja na kuzungumza na wachimbaji ili kubaini changamoto zinazowakabili kwa ajili ya kuzitafutia ufumbuzi.
Imeandaliwa na:
Mohamed Saif,
Afisa Habari,
Wizara ya Madini,
5 Barabara ya Samora Machel,
S.L.P 2000,
11474 Dar es Salaam,
Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,
Barua Pepe: info@madini.go.tz,
Tovuti: madini.go.tz
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.