[Latest News]: Lindi, Morogoro, Songwe Kuchele!

Tarehe : April 18, 2023, 4:46 p.m.
left

Ikiwa imetimia miaka miwili tangu kusainiwa kwa Mikataba Minne ya Uchimbaji madini, leo Aprili 17, 2023 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anashuhudia tena utiaji saini wa Hati ya Makubaliano ya Mikataba Mitatu ya uchimbaji Madini Mkubwa na wa Kati baina ya Serikali na Wabia.

Makubaliano hayo yamehusisha mikataba ya Msingi na Mikataba ya Wanahisa baina ya Serikali na  kampuni za Evolution Energy Minerals Limited,  EcoGraf Limited  na Peak Rare Earth Limited zote za Australia.

Makubaliano hayo na Serikali  ni ya kuchimba madini ya kimkakati ya Graphite (Kinywe) katika wilaya ya Ruangwa eneo la Chilalo  mkoani Lindi, madini ya kinywe eneo la Epanko wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro na madini ya rare earth elements katika eneo la Ngualla wilaya ya Songwe mkoani Songwe.

Aidha, kwa mujibu wa makubaliano ni kuwa miradi ya uchimbaji itasimamiwa na Kampuni za ubia wa Serikali na Wawekezaji zitakazojulikana kama Kudu Graphite Limited kwa mradi wa Chilalo, Duma TanzGraphite kwa mradi wa Epanko na Mamba Minerals Corporation na Mamba Refinery Corporation kwa mradi wa Ngualla.
 
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Dkt. Samia Suluhu amesema miradi hiyo ni mikubwa na inatarajia kuleta tija kwa taifa na hivyo kuwataka watanzania kujipanga kufanya kazi na kutoa huduma mbalimbali katika migodi itakayoanzishwa kupitia madini hayo yanayohitajika sana kwa sasa duniani.

Dkt. Samia amesema kutokana Tanzania kubarikiwa  madini ya aina mbalimbali ikiwemo ya kimkakati ambayo yana mahitaji makubwa kwenye matumizi ya teknolojia dunia, amesema siku za usoni Tanzania inakwenda kuwa kitovu cha uzalishaji na usafishaji wa madini ya nikeli na baadaye kuvutia uwekezaji katika viwanda vya uzalishaji wa betri na magari ya umeme.

Kutokana na Baraka hizo, Dkt. Samia amewataka wasimamizi wa rasilimali hizo kutochukulia fursa hizo kwa wepesi bali kuichukulia kwa umakini wa nani taifa lishirikiane naye katika uendelezaji wa rasilimali hizo ili kuhakikisha taifa linanufaika ipasavyo.

‘‘Nimetaarifiwa kuna kiasi cha mashapo yapatayo tani Milioni 67 yenye kiwango cha wastani wa asilimia 5.4 za madini ya Kinywe (indicated and inferred) yamegundulika katika eneo la Kijiji cha Chilalo, Ruangwa ambayo yatachimbwa kwa muda wa zaidi ya miaka 18. kiasi cha mashapo yapatayo tani Milioni 63 yenye kiwango cha wastani wa asilimia 7.6 za madini ya Kinywe yamegundulika katika eneo la Kijiji Epanko, Mahenge ambayo yatachimbwa kwa muda wa zaidi ya miaka 17.5,’’ amesema.

Ameongeza kwamba, kiasi cha mashapo yapatayo tani Milioni 18.5 yenye kiwango cha asilimia 4.8 za madini ya rare earth elements yamegunduliwa katika eneo la Kijiji cha Ngwala, Songwe ambayo yatachimbwa kwa muda wa zaidi ya miaka 24. 

Aidha, amesema kutokana na miradi hiyo kugusa maisha ya watu moja kwa moja, amewataka Wakuu wa Mikoa katika maeneo miradi itapatekelezwa kusimamia vizuri ili ilinufaishe taifa na watanzania.

Aidha, amewataka wawekezaji waliosaini makubaliano kuhakikisha wanatekeleza mikataba hiyo kwa haraka na kwa mujibu wa makubaliano ili watanzania wanufaike kikamilifu na hazina hiyo ambayo nchi imebarikiwa kuwa nayo.

Dkt. Samia ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wawekazaji hao na pia kuona wanapata manufaa ya kuwekeza nchini.

Amesema kupitia miradi hiyo, Serikali itapata manufaa mbalimbali kupitia kodi, tozo, ajira, maendeleo ya miundombinu, ukuaji wa teknolojia mbalimbali, huduma kwa jamii na ununuzi wa bidhaa na huduma zinazopatikana hapa nchini. 

Awali, akizungumza katika halfa hiyo, Mwenyekiti wa Timu Maalum ya Majadiliano ya Serikali Prof. Palamagamba Kabudi amesema serikali imesaini mikataba mitatu ya madini muhimu na ya kimkakati ambayo kila mmoja serikali itakua na hisa za asilimia 16 zisizopungua thamani na wawekezaji asilimia 84 na kuitaja Tanzania kua nchi ya pekee duniani yenye aina hiyo ya mikataba.

Ameongeza kwamba, mbali na kusainiwa kwa mikataba hiyo, serikali inaendelea na majadiliano ya mikataba mingine minne ambayo itasainiwa muda wowote baada ya kukamilishwa.

Akizungumzia gharama za uwekezaji kwa kampuni hizo amesema, mradi wa graphite Chilalo una jumla ya uwekezaji wa kiasi cha Dola za Marekani milioni 100, mradi wa graphite Epanko una uwekezaji wa Dola za Marekani Milioni 127.7 na mradi wa rare earth elements Ngualla una uwekezaji   Dola za Marekani Milioni 439.

‘’Mhe. Rais, pamoja na mikataba iliyosainiwa, pia natoa nafasi za watanzania kushiriki katika nafasi za juu za utendaji kwa kampuni zote,’’ amesema.

Naye, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko akizungumza katika hafla hiyo amesema wakati dunia ikijipanga kutumia madini ya kimkakati tayari Serikali ya Tanzania imesaini mikataba ya madini hayo ambayo inatarajia kuleta nchini mtaji wa Dola za Marekani milioni 667.

‘’Mhe. Sekta hii haipigi hatua hii kimuujiza, bali ni kutokana na maelekezo yako na namna unavyoisimamia sekta ya Madini. Tulio Wizara ya madini tukisimamia kikamilifu ili yale yanayokusudiwa kutokea yatatokea na lengo la Chama Cha Mapinduzi kuzalisha ajira milioni 8 litawezekana kupitia sekta ya madini,’’ amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa, pamoja na kwamba Serikali inaendelea kuvutia uwekezaji mkubwa katika sekta ya madini bado haijawaacha wachimbaji wadogo ambao mchango wao kwenye sekta ya Madini umeendelea kukua na kusema, hivi sasa mchango wa wachimbaji wadogo kwenye mauzo yote ya madini umefikia asilimia 40 kutoka asilimia 20 ya kipindi alichoingia madarakani Rais Samia.
 

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals