[Latest Updates]: Tanzania Yapata Mapokezi Makubwa Maonesho ya 68 ya Vito Thailand

Tarehe : Sept. 6, 2023, 3:04 p.m.
left

Naibu Katibu Mkuu Mbibo awataka Wafanyabishara, Wachimbaji kuchangamkia fursa

Na Wizara ya Madini- Bangkok

Ushiriki wa Tanzania katika Maonesho ya 68 ya Vito na Usonara katika jiji la Bangkok   nchini Thailand umewavutia Wafanyabiashara mbalimbali wa madini kutokana na wengi kutumia malighafi za madini kutoka nchini.

Akizungumza baada ya kushiriki hafla fupi ya ufunguzi wa maonesho hayo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya  Madini Msafiri Mbibo amesema  wafanyabiashara wakubwa wa madini nchini humo wakiwemo viongozi wa Serikali wameonesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali zikiwemo  biashara ya madini, uongezaji thamani madini pamoja na kubadilishana uzoefu katika shughuli hizo.

Aidha, Mbibo amesema  uwepo wa Tanzania  katika maonesho hayo ya madini yenye thamani kubwa unalenga  kujifunza pamoja na kuhamasisha urejeshwaji wa minada ya madini nchini na kuhamasisha uwepo wa masoko ya madini ambapo wafanyabiashara hao wanaweza kununua madini kupitia masoko ya madini yaliyoanzishwa katika kila mkoa nchini.

Serikali kupitia Wizara ya Madini inatarajia kurejesha tena minada ya madini nchini pamoja na Maonesho ya Kimataifa ya Vito na Usonara ya Arusha yatakayofanyika kila mwaka kulingana na kalenda  za kimataifa ya maonesho ya madini ya vito na biashara za usonara.

Aidha, hivi karibuni Serikali kupitia Tume ya Madini ilitoa taarifa kuwa, Wizara ipo kwenye mchakato wa kuwasilisha mapendekezo ya maboresho ya Sheria na Kanuni ili kuwezesha maonesho na minada ya vito kufanyika nchini ikiwemo marekebisho ya Kanuni za Eneo Tengefu la Mirerani za Mwaka 2021 ambazo zilizuia kuuzwa kwa madini ya Tanzanite nje ya Mirerani.

Kufuatia hayo, Mbibo ametoa wito kwa wauzaji, wachimbaji, waongezaji thamani madini kutumia uhusiano  mzuri  uliopo kati ya  Tanzania na Thailand ambao umekuwepo  kwa muda mrefu kuchangamkia fursa  hiyo ikiwemo kuungana na wadau  wa nchi hiyo katika masuala yanayohusu  mnyororo wa shughuli za madini.

Ameongeza kwamba, tayari Serikali ya Awamu ya Sita imefungua milango  ya biashara katika Sekta ya Madini na kuwataka wadau wa madini nchini kutumia fursa hiyo kuwapokea wawekezaji mbalimbali  ili hatimaye  kujenga uchumi imara na kuinua ustawi wa watanzania  kupitia rasilimali madini.

‘’Biashara lazima iwe na wauzaji na wanunuzi wawe tayari kupokea watu wengine na wajifunze namna ya kufanya biashara kutoka biashara ya kitaifa hadi kimataifa kwa madini ya thamani na mawe,’’ amesema Mbibo.

Akizungumza baada ya ujumbe wa Tanzania kutembelea banda la Kampuni ya  Bright Future katika maonesho hayo, Mkurugenzi wa Kampuni  hiyo Ashish Baid ambaye pia   ni Makamu wa Rais wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa Madini nchini humo  na mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite na madini  mengine, ameelezea nia yake ya dhati kupitia jukwaa hilo na kampuni yake binafsi  ya kushirikiana na Tanzania katika kuipa  thamani ya kimataifa  minada ya madini  endapo Serikali itakuwa yatari kushirikiana  nao ikiwemo katika eneo la uongezaji thamani madini.

Ameongeza kwamba, kwa kuzingatia uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Thailand na kutokana na utajiri wa rasilimali madini zilizopo nchini ikiwemo madini pekee ya Tanzanite, wananchi wa Tanzania na taifa hawana budi kunufaika ipasavyo na rasilimali hiyo na si kwa wafanyabiashara pekee  wa madini  na kuongeza,’ ’ikiwa sisi wafanyabiashara tunanufaika ni muhimu sana Kwa Tanzania kunufaika," amesema.

Naye, Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Fine Gamestone  Sukharit Sinchawla baada ya kutembelewa na ujumbe wa Tanzania   amesema amefurahishwa na uwepo wa Tanzania katika maonesho hayo na kusema ni nchi nzuri  yenye madini  mengi mazuri na yenye thamani kubwa  na kueleza kwamba ni nchi ambayo kampuni yake inatumia  madini mengi kufanya biashara yakiwemo ya Spinel  na Tanzanite.

Maonesho ya BangKok ni moja ya maonesho ya madini ya vito na usonara maarufu zaidi duniani na yamekuwepo nchini humo kwa miaka mingi. Maonesho hayo yameandaliwa na Idara ya Ukuzaji Biashara ya Kimataifa ya Thailand.

 Aidha, biashara ya madini nchini humo imetajwa kuwa ya pili katika kuchangia fedha za kigeni ikiwemo kukuza ajira .

Wadau muhimu wapatao 31 elfu kutoka maeneo mbalimbali duniani wanatarajia kutembelea maonesho hayo   kutoka  nchi 21   na  waoneshaji takribani 1,100.

Imeelezwa kuwa mwaka 2022 mauzo ya vito  na usonara nchini humo  yalifikia thamani ya Dola za Marekani milioni 800 na mwaka huu  mauzo yanatarajiwa kufikia Dola za Marekani milioni 850.

Maonesho ya BangKok ni maonesho makubwa  na ya kuaminika ambayo wafanyabiashara wachimbaji wanaweza kuyatumia kujenga uhusiano wa kibiashara, kutangaza bidhaa zao na kuuza.

Mbali na Naibu Katibu Mkuu, wengine wanaoshiriki ni wawakilishi kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC)   na Wataalam kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals