[Latest Updates]: Biteko asisitiza sekta za kiserikali kupunguza urasimu, kuondoa rushwa

Tarehe : Jan. 8, 2019, 12:41 p.m.
left

  • Ni baada ya kubaini ucheleweshaji wa utoaji vibali vya uwekezaji sekta ya madini

Na Nuru Mwasampeta, Geita

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato kutoa kibali kwa wamiliki wa Kiwanda cha Kuchenjua Dhahabu kinacho milikiwa na kampuni ya Pedalu ili waweze kupewa leseni na kuendelea na shughuli ya kuchenjua madini hayo.

Biteko aliyasema hayo wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la kiwanda cha kuchenjua dhahabu kinachomilikiwa na kampuni ya wazawa ya Pedalu, katika kijiji cha Lumasa mjini Chato, iliyofanyika Desemba 2, 2019.

Alisema kuwa, kibali kingine kinapaswa kutolewa na Mkemia Mkuu wa Serikali na kubainisha kuwa, baada ya hafla hiyo atawasiliana naye ili awezeshe upatikanaji wa kibali hicho kwa lengo la kuiwezesha wizara ya madini kuendelea na mchakato wa kuandaa leseni itakayowaruhusu wawekezaji hao wazawa kuendelea na kazi ya uchenjuaji wa madini.

“Jamani, Rais anataka viwanda, isitokee mtu hapa katikati anaweka urasimu na kuchelewesha azma ya Rais wetu, nchi hii tunaondoa urasimu tunataka kuondoa na rushwa,” alisisitiza Biteko.

Aidha, alibainisha kuwa, miongoni mwa masuala yanayowakimbiza wawekezaji nchini ni mawili tu, rushwa na urasimu na wala si sheria, na kusema kuwa, vitu hivyo ni kikwazo kikubwa katika kutimiza azma ya Serikali ya Tanzania ya Viwanda.

Aliwapongeza wawekezaji katika kiwanda cha Pedalu kwa kufanya uwekezaji huo mkubwa kwani anaamini madini yatakayopatikana kutoka katika kiwanda hicho yataiwezesha serikali kupata  kodi stahiki. Pia, Biteko aliwaomba wawekezaji hao wazawa kujenga viwanda vingine kama hivyo katika maeneo tofauti na kuahidi kupeleka wadau wenye  nia ya kujifunza ili waweze kupata ujuzi wa namna ya kuwekeza ili kukuza sekta ya madini kwa pamoja.

Aidha, alimtaka Kaimu Afisa Madini Mkoa wa Geita, Pius Bajunana kuwalea vema wawekezaji na kuwataka watendaji wa Serikali kuwaendea wawekezaji hao kwa sura ya kirafiki badala ya kufuatilia masuala ya ulipwaji wa tozo mbalimbali kwa ukali. Alisema ili wawe huru kushirikiana na Serikali katika masuala yote yanayohusu utekelezaji wa majukumu yao, suala la urasimu linatakiwa kuondolewa ili kushirikiana vizuri katika kukuza uchumi wa nchi.

Halikadhalika, Biteko alisisitiza kwa kuwataka watendaji wa serikali waliohudhuria hafla hiyo na wengine kuwasidia wawekezaji wazawa ili waweze kukuza viwanda vyao na kuongeza kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya mabadiliko katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kwa lengo la kuwanufaisha watanzania hivyo, hawana budi kumuunga mkono.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Biteko aliwataka wachimbaji wadogo wa madini kufanya kazi kwa uaminifu huku wakijua kuwa Serikali ipo pamoja nao na kuwataka kuutumia vizuri wakati huu ambao imeazimia kukuza sekta ya uchimbaji mdogo wa madini ili wakati neema hiyo itakapopotea wasije wakajilaumu.

“Ametokea Rais anayewapenda watu hao, wanyonge, anatamani awasaidie waweze kukuza uchumi wao, wajibu wao ni kumuunga mkono Rais wetu, pamoja na kumwombea kwani kazi anayoifanya ni ngumu. Rais ametutuma tuwafikie wachimbaji wadogo kwani anataka ninyi wachimbaji wadogo mgeuke kuwa wachangiaji wakubwa kwenye uchumi wa taifa,” aliongeza Naibu Waziri Biteko.

Alisema Rais Dkt. John Magufuli ametoa Jumla ya Dola za Marekani Milioni tatu laki saba mia tatu elfu mia sita na sitini sawa na shilingi bilioni nane na nusu za kitanzania kwa ajili ya kufanya utafiti ili kuwasaidia wachimbaji wadogo. “ Rais wenu anawapenda, na sisi ametutuma kuja kuwasaidia wachimbaji wadogo ili mtoke kwenye wimbi la umaskini na uchimbaji wa kubahatisha,” alisema Biteko

Aliongeza kwamba, hivi sasa wizara imeanza kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo, katika maeneo mbalimbali ikiwemo Bukombe Kyerwa Kona Z, Mpanda, Tanga na maeneo mengine nchini, kwa la kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata elimu ya uchimbaji wenye tija.

Aidha, Biteko aliwataka wachimbaji wadogo kuachana na biashara ya ujanjaujanja na kuwataka kutenda haki na kuachana na majungu badala yake wafanye kazi kwa upendo na ushirikiano.

Alibainisha kuwa, wapo wachimbaji wadogo zaidi ya milioni nne nchini lakini cha kushangaza wanachangia asilimia 4 pekee katika uchumi wa taifa. Alisema wachimbaji wadogo walio wengi hawalipi kodi, na ni mabingwa wa kutorosha madini. “Mnakwepa kodi lakini mna waibia watanzania wenzenu,” alisema. 

Kwa upande wake Waziri wa Nishati na Mbunge wa jimbo la Chato, Dkt. Medard Kalemani alisema wizara yake iko katika mchakato wa kuwaunganishia umeme wa uhakika wachimbaji wadogo nchini kote ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya Tano ya kuiwezesha sekta hiyo kuwa na uzalishaji wenye tija.

Wakati huohuo, uongozi wa kiwanda cha Pedalu ulikiri kuwa, uamuzi wa kujenga kiwanda hicho ni matokeo ya matakwa ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwataka wachimbaji wa madini kuyaongezea thamani madini nchini badala ya kuyasafirisha yakiwa ghafi jambo ambalo linainyima serikali mapato zaidi

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals