[Latest Updates]: Dkt Macheyeki aitaka kampuni ya Neelkanth kuachana na uagizaji wa malighafi kutoka nje ya nchi

Tarehe : Feb. 22, 2019, 1:55 p.m.
left

Na Greyson Mwase, Pwani

Kamishna wa Tume ya Madini, Dkt. Athanas Macheyeki ameitaka kampuni inayojishughulisha na uzalishaji wa chumvi ya Neelkanth Salt Limited iliyopo Wilayani Mkuranga mkoani Pwani kuachana na uagizaji wa malighafi zinazotumika katika kuzalisha chumvi  kutoka nje ya nchi na badala yake ijikite kwenye matumizi ya malighafi zilizopo nchini na kusisitiza kuwa kufanya hivyo kunazorotesha soko la ndani.

Dkt. Macheyeki alitoa agizo hilo mapema leo tarehe 22 Februari, 2019 kwenye ziara yake katika kiwanda hicho ikiwa ni sehemu ya ziara ya Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula katika mkoa wa Pwani yenye lengo la kutembelea wachimbaji wa madini pamoja na kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.

Aliyasema hayo mara baada ya kuelezwa kuwa kampuni hiyo imekuwa ikiagiza  malighafi ya chumvi kwa asilimia kati ya 60 na 70 kutoka katika nchi za Namibia, India na Afrika ya Kusini.

Alisema kuwa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 pamoja na Marekebisho yake ya Mwaka 2017 inawataka wachimbaji wa madini nchini kutumia bidhaa za ndani ya nchi badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi na kuitaka kampuni hiyo kuendelea kujipanga zaidi katika kuhakikisha baadaye inaondokana na matumizi ya malighafi za kutoka nje ya nchi.

Aliendelea kusema kuwa, katika kujiandaa na matumizi ya malighafi ya chumvi kutoka ndani ya nchi, kampuni inatakiwa kutoa elimu kwa wazalishaji wa chumvi katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Kilwa ili waweze kununua chumvi iliyo bora na kuondokana na matumizi ya malighafi ya chumvi kutoka nje ya nchi na kuinua uchumi wa wazalishaji hao wa chumvi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Macheyeki aliitaka kampuni hiyo kuhakikisha inawasilisha mpango wa manunuzi ya bidhaa na huduma kutoka wananchi wanaoishi karibu na kiwanda hicho (local content plan) pamoja na kiapo cha uadilifu   Machi 15 mwaka huu  kwenye Ofisi za Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini zilizopo jijini Dodoma.

Aidha, Dkt. Macheyeki aliitaka kampuni hiyo kuwasilisha mpango wa kuongeza ujuzi kwa wafanyakazi wake ili baadaye waweze kushika nafasi za wataalam kutoka nje ya nchi kwenye Ofisi za Tume ya Madini mapema kama Sheria ya Madini inavyowataka.

Aliendelea kufafanua kuwa, Serikali inapenda kuona wawekezaji katika sekta ya madini wanafanya kazi katika mazingira mazuri ili waweze kulipa kodi mbalimbali Serikalini.

“Ndio maana tozo nyingi zilizokuwepo kwenye madini ya chumvi zimeondolewa, tunataka mzalishe kwa faida, lakini wito wangu kwenu ni kuhakikisha mnafuata Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake, Tume ya Madini ipo tayari kuwasaidia muda wowote,” alisisitiza Dkt. Macheyeki.

Awali akizungumzia changamoto za kampuni hiyo, mmoja wa wataalam kutoka kampuni hiyo, Tanmay Purohit alisema kuwa kumekuwepo na changamoto ya kukatika kwa umeme na kuongeza kuwa wameshaiomba Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuwekewa umeme katika mashamba ya chumvi yaliyopo katika eneo la Shungubweni wilayani humo na kuwekewa gesi kwa ajili ya matumizi ya kiwandani hapo.

Alisema kuwa wamekuwa wakitumia gharama kubwa ya kuendesha mitambo kwa kutumia dizeli pindi umeme unapokatika kiwandani hapo na katika mashamba ya chumvi.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals