[Latest Updates]: Mgodi wa Buhemba wafunguliwa rasmi

Tarehe : March 28, 2018, 10:51 a.m.
left

Hatimaye Serikali imefungua Migodi ya Dhahabu ya Wachimbaji Wadogo iliyopo katika eneo la Buhemba Wilaya ya Butiama Mkoani Mara baada ya kujiridhisha hali ya usalama katika migodi hiyo.

Migodi hiyo imefunguliwa rasmi na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo Januari 13, 2018 na kushuhudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Annarose Nyamubi.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) akifungua rasmi migodi ya Buhemba ya wachimbaji wadogo. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima akishuhudia tukio hilo.[/caption]

Akizungumza katika tukio hilo, Nyongo alisema jumla ya migodi 10 imefunguliwa kati ya 16 baada ya kujiridhisha usalama wake.

Alifafanua kwamba eneo la Buhemba lina jumla ya Migodi ya Dhahabu 16 ambayo inamilikiwa na Wachimbaji Wadogo hata hivyo iliyokidhi vigezo vya kiusalama ni Migodi 10 pekee ambayo imeruhusiwa kuendeleza shughuli za uchimbaji.

Alisema Serikali ilisitisha shughuli za uchimbaji Madini kwenye eneo hilo la Buhemba Februari 2017 baada ya kutokea vifo vya Wachimbaji Saba na wengine wapatao 15 kujeruhiwa kutokana na kufanya shughuli zao bila kuzingatia taratibu na kanuni za uchimbaji salama.

Alibainisha kuwa Mwezi Desemba mwaka jana alifanya ziara kwenye eneo hilo ili kujionea hali halisi ya machimbo husika pamoja na kuzungumza na wachimbaji waliosimamishwa kuendeleza shughuli zao ambapo aliagiza shughuli za ukaguzi zikamilike ifikapo Mwezi huu wa Januari ili migodi ifunguliwe.

"Kama mtakumbuka nilifanya ziara hapa na niliagiza kufikia Januari 10, 2018 Ukaguzi wa Usalama kwenye eneo la Machimbo ya Dhahabu ya Buhemba uwe umekamilika ili shughuli za uchimbaji zilizokuwa zimesimamishwa ziruhusiwe; tumejiridhisha mashimo kumi ni salama na sasa tunafungua rasmi," alisema Naibu Waziri Nyongo.


Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima akizungumza wakati wa ufunguzi wa migodi ya wachimbaji wadogo ya Buhemba, Mkoani Mara.[/caption]

Alisema shughuli hiyo ya Ukaguzi kama alivyokua ameagiza ilifanyika kwa umakini na kwamba maduara Kumi (Migodi Kumi) yameruhusiwa na mengine Sita hayatoruhusiwa kuendeleza shughuli za uchimbaji.

Aliongeza kuwa baada ya kufika kwenye eneo hilo kwa mara ya kwanza alisikitishwa kuona wananchi wengi wakiwa wamekosa shughuli za kufanya kutokana na migodi hiyo kufungwa na ndiyo sababu ya kuagiza ukaguzi wake ukamilike haraka.

“Nilivyotembelea hapa Mwezi Desemba mwaka jana nilisikitishwa kuona shughuli za uchumi kwenye eneo hili la Buhemba zimesimama kutokana na shughuli za uchimbaji kusimamishwa baada ya kutokea ajali,” alisema.

Aidha, Naibu Waziri Nyongo aliwaagiza Wakaguzi wa Migodi kuhakikisha wanatembelea mara kwa mara maeneo ya migodi ili kukagua hali ya usalama pamoja na kutoa mafunzo ya uchimbaji salama kwa wachimbaji hususan wadogo lengo likiwa ni kuepusha ajali.

[ Naibu Waziri wa Madini, Stansalus Nyongo (kulia) akijiandaa kufungua rasmi Migodi ya Dhahabu ya Wachimbaji Wadogo wa Buhemba, Wilayani Butiama Mkoani Mara. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima.[/caption]

“Ninawaagiza kwa mara nyingine Wakaguzi wa Migodi kuhakikisha mnatembelea maeneo ya migodi mara kwa mara ili kuepusha ajali,” aliagiza Naibu Waziri.

Naibu Waziri Nyongo vilevile aliwaagiza wachimbaji madini kuhakikisha wanafuata sheria, kanuni na taratibu za uchimbaji ili kuepusha ajali migodini na wakati huohuo kunufaika ipasavyo na shughuli zao bila kupata usumbufu.

Aidha, Naibu Waziri alizungumzia ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali ambapo aliwaagiza wachimbaji hao kuhakikisha wanalipa kwa mujibu wa sheria na alionya kwamba mgodi utakaoshindwa kulipa inavyostahili, utafungiwa.

"Tumewafungulieni migodi yenu tukiamini kwamba nanyi mtatimiza wajibu wenu wa kulipa kodi kwa mujibu wa sheria. Mkishindwa kulipa, hatutosita kuifungia," alibainisha Nyongo.

Naibu Waziri Nyongo yupo Mkoani Mara kwa ajili ya shughuli za ukaguzi wa migodi na kuzungumza na wachimbaji wadogo.

Imeandaliwa na:

Mohamed Saif,

Afisa Habari,

Wizara ya Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,

Barua Pepe: info@madini.go.tz,                                                                               

Tovuti: madini.go.tz

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals