Tarehe : Aug. 29, 2024, 12:36 p.m.
Agosti 29, 2024 – Dodoma
Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Chemba ya Migodi Tanzania (TCM) inautaarifu Umma na Wadau wa Madini ndani na nje ya nchi kuwa, Tanzania inaandaa Mkutano wa 6 wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini utakaofanyika kuanzia tarehe 19 hadi 21 Novemba, 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar Es Salaam.
Katika mkutano huo unaofanyika kila mwaka, Tanzania itaendelea kuutumia kuzinadi fursa zake za uwekezaji zilizopo katika mnyororo mzima wa shughuli za madini nchini zikihusisha usambazaji wa bidhaa na utoaji huduma migodini, uongezaji thamani madini, utafiti na uchimbaji madini chini ya kaulimbiu ‘’Uongezaji Thamani Madini kwa Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii’’.
Kaulimbiu ya mwaka 2024, inasisitiza kuhusu umuhimu wa uongezaji thamani ambao unaleta faida za kiuchumi na kijamii kwa maendeleo endelevu kupitia shughuli za uongezaji thamani. Ikumbukwe kwamba, uongezaji thamani madini husaidia kupandisha thamani ya madini yanayozalishwa kabla ya kusafirishwa nje, kuchochea uanzishwaji wa viwanda, kuongeza zaidi mapato kwa Serikali na wawekezaji, kutanua wigo wa ajira na kuifungamanisha Sekta ya Madini na nyingine za kiuchumi.
Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani iliyojaaliwa utajiri wa madini ya aina mbalimbali yakiwemo ya vito, yakihusisha madini adimu ya tanzanite, rubi yenye ubora zaidi ya Winza, Spinel yenye thamani ya Mahenge pamoja na madini ya viwandani na nishati. Katika zama hizi ambapo mahitaji ya madini duniani yanaongezeka ikiwemo madini muhimu na mkakati, Tanzania inajipambanua kama nchi mzalishaji mkubwa ili kuvutia uwekezaji katika shughuli za uongezaji thamani madini, utafiti na uchimbaji wa madini.
Kutokana na utajiri huo, Tanzania iko katika nafasi ya kipekee ya kukidhi mahitaji hayo, ikitoa fursa bora za uwekezaji katika shughuli za uongezaji thamani madini, uchimbaji madini, na shughuli nyingine katika mnyororo wa thamani wa madini. Mkutano huu unatarajiwa kuwakutanisha wadau mbalimbali wa kimataifa wa madini wakimwemo wawekezaji, viongozi wa sekta, watafiti, na wawakilishi wa serikali kujadili masuala muhimu yanayohusu uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini.
Aidha, Washiriki watapata taarifa za moja kwa moja kuhusu Sera ya Madini za Tanzania, Sheria, vivutio vya uwekezaji, ikiwemo dhamira ya Serikali kuweka mazingira rafiki na wezeshi ya uwekezaji kwa uchimbaji endelevu. Aidha, mkutano huo utakwenda sambamba na mijadala mbalimbali kuhusu Sekta ya Madini, mikutano ya kibiashara, kujenga mahusiano ya kibishara pamoja na Hafla ya Usiku wa Madini ambayo Wizara huitumia kutoa tuzo kwa wawekezaji mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kutambua jitihada zao kwa maendeleo ya kiuchumi Tanzania. Tukio hilo huenda sambamba na maonesho ya bidhaa za mapambo ya vito ili kuonesha fursa zilizopo katika sekta ndogo ya madini ya vito na kuhamasisha matumizi ya bidhaa za vito zinazozalishwa nchini.
Kwa taarifa zaidi kuhusu kushiriki katika mkutano huo, kudhamini na kushiriki katika maonesho, tafadhali tembelea tovuti https://conference.madini.go.tz au wasiliana na Bw. Erick Peter Ketagory kupitia barua pepe erick.ketagory@madini.go.tz au +255714278620/757432409. Ungana na wabobezi katika Sekta ya Madini, fahamu kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo nchini kwa mustakabali wa uchimbaji wa Madini Tanzania na duniani.
Karibu Tanzania, the Home of Tanzanite.
Imetolewa na:
Mhe. Anthony Mavunde
Waziri wa Madini.
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.