Tarehe : Sept. 22, 2025, 11:28 a.m.
Bombambili- Geita,
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amesema sekta ya madini imekuwa mhimili muhimu unaoibeba uchumi wa Kanda ya Ziwa na Taifa kwa ujumla, huku akiitaka jamii kuendelea kushiriki kikamilifu katika fursa zinazochipuka kupitia sekta hiyo.
Amesema hayo leo Septemba 22, 2025 wakati akizungumza katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bombambili – Geita, alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya Teknolojia ya Madini Geita
Waziri Mkuu Majaliwa amesema, mchango wa madini katika Pato la Taifa umekuwa ukipanda mwaka hadi mwaka, sambamba na kuimarika kwa mifumo ya usimamizi, ukusanyaji mapato na uwekezaji wa ndani na nje ya nchi.
“Mchango wa Sekta ya Madini katika maendeleo ya Taifa si wa kubeza. Kanda ya Ziwa pekee imejidhihirisha kama kitovu cha madini ya dhahabu, Mkoa wa Geita, na mikoa ya jirani na hivi sasa tunashuhudia miradi mikubwa ya madini ikisaidia upatikanaji pato, ajira, ujenzi wa miundombinu ya afya, elimu, kilimo, usafiri na uchukuzu na kuendelea kuhakikisha Watanzania wananufaika zaidi,” amesema Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa wadau wa sekta hiyo kutumia maonesho ya Geita kama jukwaa la kuonesha jinsi Sekta ya Madini inavyochangia katika mapinduzi ya kiteknolojia hapa nchini, pamoja na mbinu rafiki za uchimbaji na uhifadhi wa mazingira.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, amesema kuwa uwepo wa maonesho hayo umekuwa kichocheo cha mageuzi makubwa katika Sekta ya Madini, hususan dhahabu.
Samamba amefafanua kuwa kupitia teknolojia mpya zilizotambulishwa na wadau katika maonesho ya miaka ya nyuma, uzalishaji wa dhahabu umeongezeka kwa kasi na kufikia zaidi ya tani 62 kwa mwaka, ukilinganisha na wastani wa tani 45 miaka michache iliyopita.
“Hii ina maana kwamba teknolojia hizo zimeboresha mbinu za uchimbaji na usimamizi, kupunguza upotevu wa madini, na kuongeza tija kwa wachimbaji wadogo na wakubwa. Pia tumeona ongezeko la viwanda vya kusafisha na kuchakata madini, hali inayoongeza thamani kabla ya kuuzwa,” amesema Samamba.
Naye, Mkuu wa Mkoa Geita Mhe. Martin Shigella ameeleza kuwa Mkoa huo umeendelea kutekeleza Maagizo yaliyotolewa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akifunga maonesho hayo mwaka jana ambapo aliagiza kujengwa kwa miundombinu ya kudumu katika viwanja hivyo.
“Mpaka sasa tayari kuna majengo ya kudumu tisa yameshajengwa katika viwanja hivi vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.1 na ujenzi unaendelea” amesisitiza Shigella.
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.