[Latest Updates]: Bodi ya Stamico watembelea mnada wa Tanzanite

Tarehe : July 28, 2017, 9:22 a.m.
left

  • Wanunuzi wa Tanzanite kutoka Tanzania, Hongkong, China, USA, Sri-Lanka na Kenya wajitokeza.

Na Koleta Njelekela, Naisinyai, SIMANJIRO

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Balozi Alexander Muganda na Mjumbe wa Bodi hiyo, John Seka, wametembelea eneo la kijiji cha Naisinyai wilayani Simajiro, mkoa wa Manyara, unapofanyika Mnada wa Tatu wa Kimataifa wa Madini ya Tanzanite, ili kujionea jinsi mnada huo unavyoendeshwa katika ushindani mkubwa na uwazi.

Mnada huo wa Kimataifa wa Madini ya Tanzanite umeandaliwa na Serikali kupitia Wizara ya Madini na ulianza rasmi tarehe 18 na kukamilika tarehe 21 Desemba, 2017 kwa lengo la kuimarisha soko la Tanzanite kwa wanunuzi wa ndani na wanaotoka nje ya nchi.

Akizungumza baada ya kutembelea mnada huo, Balozi Muganda, ameipongeza Wizara ya Madini kwa kuendeleza minada hiyo, ambayo imesaidia kuvutia wanunuzi wakubwa wa madini kuja Tanzania kununua Tanzanite katika masoko yanayotambulika kisheria na hivyo kuchangia ukusanyaji wa kodi stahiki na kukuza Pato la Taifa.

Amesema kujitokeza kwa makampuni matatu katika kuuza Tanzanite kupitia mnada huo, yaani Kampuni ya Tanzanite One Mining Limited (TML) yenye ubia na STAMICO; Tanzanite Afrika na Classic Gems; kunaonesha ishara ya mafanikio katika kuboresha masoko halali ya madini hayo, na kuleta matumaini ya kwamba wauzaji wengi zaidi wataendelea kujitokeza katika minada ijayo.

“Nafurahi kuona namna wanunuzi wa Tanzanite wanavyweza kutathmini wao wenyewe viwango vya madini, kupanga bei watakayonunulia na kuwasilisha Zabuni kwenye sanduku la zabuni, wakati wakisubiri matokeo ya zabuni hiyo. Sisi kama wauzaji wakuu, tutaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kuimarisha Soko halali na la uhakika la Tanzanite kwa wanunuzi wa ndani na wa kutoka mataifa mbalimbali duniani,” alifafanua Balozi Muganda.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanzanite One Mining Limited (TML) , Hussein Gonga (anayetoa maelezo kushoto) akimuonesha kipande cha Tanzanite Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO, Balozi Alexander Muganda alipotembelea nyumba ya EPZ iliyoko kijiji cha Naisinyai, Simanjiro mkoani Manyara, katika Mnada wa Ttatu wa Kimataifa wa Tanzanite.[/caption]

Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya STAMICO, John Seka ameshauri wachimbaji wa madini ya Tanzanite kushiriki kwa wingi katika minada ijayo ili kuifanya iwe endelevu na yenye manufaa kwa Serikali na watanzania kwa ujumla.

“Kitendo cha Serikali kufanya minada ya aina hii ni kizuri na cha kujivunia kama nchi, kwani kinasaidia kuimarisha udhibiti madini na kukuza soko la ndani katika viwango vya bei za Kimataifa, ” alieleza Seka.

Aidha, aliitaka Menejimenti ya STAMICO kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa uzalishaji madini ya Tanzanite katika Mgodi wa TML na uendeshaji, ili kulinda maslahi mapana ya Taifa endelevu na kuufanya mgodi huo kujiendesha kwa faida na kuwa endelevu.

Akizungumza katika mnada huo, Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka amesema Serikali inakusudia kudhibiti utoroshwaji wa madini ya Tanzanite nje ya nchi kupitia minada hiyo, hatua ambayo itawawezesha wafanyabiashara wa madini hayo nchini, kuuza Tanzanite kwa bei ya ushindani inayoendana na Soko la Dunia.

“Mnunuzi atakayefanikiwa kununua madini hayo ya Tanzanite katika mnada huu, ni yule atakayetoa bei ya juu ambayo imefikia au kuvuka bei iliyopangwa na Timu ya Wathamini wa Serikali kutoka Wizara ya Madini,” alifafanua Mhandisi Mchwampaka.

Amesema Serikali inalenga kukusanya mapato zaidi kupitia minada hiyo ambapo asilimia 0.3 ya mauzo ya jumla yatakayopatikana; yatalipwa kwa Halmashauri ya Simanjiro kama Tozo ya Huduma (Service Levy); asilimia 6 italipwa Serikalini kama Mrabaha (Royalty) na asilimia moja italipwa pia kwa Serikali kama ada ya ukaguzi (inspection fee).

“STAMICO kama mbia mwenza wa TML, imekuwa ikilipwa management fee ya fedha zilizopatikana kutokana na mauzo ya Tanzanite kupitia minada hii, na hivyo kuwezesha kuimarisha mapato ya Shirika. Kimsingi minada hii imesaidia pia kuwakutanisha wauzaji wa Tanzanine nchini, na wale wanunuzi wakubwa wa Kimataifa; ili waweze kuwauzia Tanzanite moja kwa moja, bila kupitia kwa madalali ambao hununua kwa bei ya chini,” alibainisha Mhandisi Mchwampaka.

Wakizungumza katika mnada, Wakurugenzi wa TanzaniteOne, Faisal Shabhai na Hussein Gonga wameihaidi kuunga mkono juhudi za Serikali za kudhibiti utoroshaji wa madini hayo, kwa kuuza Tanzanite katika minada ya hapa nchini.

Wanunuzi 60 wamejitokeza kunua madini katika mnada huo wa Tatu wa Kimataifa wa Tanzanite, ambapo wanunuzi 44 wanatoka Tanzania na 16 wanatoka Mataifa mengine, ambayo ni Hongkong, China, USA, Sri-Lanka na Kenya.

Makundi hayo ya wanunuzi yanahusisha madalali, makampuni ya uchimbaji na watu binafsi.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals