[Latest Updates]: Waziri Biteko Awataka Wajiolojia Kuiheshimisha Taaluma Yao

Tarehe : Oct. 7, 2022, 11:05 a.m.
left

Awahakikishia kuundwa Bodi ya Wajiolojia

Waiomba Serikali kuzifanyia kazi changamoto zao kulinda Taaluma   

Naibu Katibu Mkuu Mbibo awahakikishia ushirikiano, ahimiza uadilifu, nidhamu ya juu

Na Asteria Muhozya, Arusha

Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amewataka Wajiolojia nchini kuhakikisha wanaiheshimisha taaluma yao kwa kutoruhusu wasio waaminifu kuingilia majukumu ya kitaaluma kutokana na umuhimu wa shughuli za utafiti kwa maendeleo ya Sekta ya Madini na Taifa.

Dkt. Biteko ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Jumuiya ya Wajiolojia Tanzania (TGS) kwa mwaka 2022 unaofanyika jijini Arusha na kuwashirikisha wajiolojia wenye ubobezi wa aina mbalimbali takribani 200 kutoka wizara, taasisi na kampuni mbalimbali nchini.

Amesema jiolojia ni sayansi muhimu kutokana na ukweli kwamba ili nchi iweze kuendelea kiuchumi inahitaji kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye eneo la jiosanyasi na kwa kuzingatia Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kuwa na rasilimali za kutosha za madini hivyo, uwepo wa wanataaluma wabobezi kutaliwezesha taifa kukuza sekta ya viwanda kupitia sekta ya Madini.

Amesema kuwepo wa wajiolojia wadanganyifu kumepelekea wawekezaji wengi kupoteza fedha zao kutokana na kupatiwa taarifa zisizo sahihi hali ambayo imepelekea wawekezaji kupoteza imani ya kuwekeza kwenye sekta ya madini huku hali hiyo ikisababishwa na wajiolojia hao.

‘’ Wajiolojia ni moyo wa sekta ya Madini, hatuwezi kuchimba bila wao na badala yake tutachimba kwa kubahatisha. Kama taifa tunataka mambo yatokee kwa nguvu ya sayansi. Wajiolojia ndiyo wanaoleta fedha za uwekezaji nchini,’’ amesisitiza Dkt. Biteko.

Akizungumzia Bodi ya Wajiolojia, amesema kwamba Wizara iko katika hatua za mwisho za kukamilisha mchakato wa kuanzishwa kwa bodi hiyo na kuongeza kwamba, baada ya Serikali kukamilisha sehemu yake itatoa nafasi kwa wadau hao kutoa maoni kuhusu namna gani bodi hiyo iundwe, namna itakavyosimamiwa, masuala ya yatakayohusisha vyanzo vya fedha na kuangalia masuala ya sheria.

Ameongeza kuwa, wakati Serikali inakamalimisha mchakato wa kuundwa kwa bodi hiyo ni muhimu wajiolojia wakahakikisha wanaiendeleza taaluma ya jiolojia ili kuipatia nchi heshima ikiwemo kuwawezesha wawezekaji kupata taarifa sahihi na hivyo kuvutia uwekezaji zaidi kwenye sekta ya Madini.

Awali, akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wajiolojia Elisante Mshiu amemweleza Waziri Biteko kuhusu kuwepo kwa changamoto kadhaa katika kutekeleza shughuli za wanajiosayansi nchini ambazo kwa kiasi flani zinachangia kuifanya taaluma kutoendelea.

Amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na kuwepo kwa changamoto ya kukuza viwango au uwezo wa kufanya tafiti kwa wahitimu wapya na kupendekeza kuanzishwa kwa mfumo wa kuweka wahitimu wapya kwenye kipindi cha mpito wakiwa wanafanyakazi chini ya uangalizi au maelekezo ya wabobezi na wanaopata ujuzi stahiki wa vitendo wathibitishwe na kuruhusiwa kufanya tafiti wenyewe.

‘’Mheshimiwa mgeni rasmi, mfumo huu hutumika kwenye nchi nyingina pia kwenye taaluma mbalimbali nchini kama vile wahandisi, madaktari, wahasibu na kadhalika.

Mshiu amezitaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na matokeo ya tafiti mbalimbali kuwa ya udanganyifu na chini ya viwango. Amesema kuwa, kwa bahati mbaya mara nyingi kuna watafiti ambao kwa makusudi wanatoa matokeo ya tafiti yasiyo sahihi na mara nyingi suala hilo hufanyika kwa makusudi. Akitoa mapendekezo ya changamoto hiyo, Mshiu amesema Chama Cha Wajiosayansi kinapendekeza kuanzishwa kwa mfumo wa uhakiki wa taarifa zinazotolewa na wataalamu hususan za miradi ya uzalishaji ili kuhakikiwa kuwa zinakuwa sahihi.

‘’ Hii itafanyika kwa kuwa na Bodi ya Uhakiki wa Taarifa, na kuwa mfumo wa kuthibitisha ubora wa taarifa hizo ambapo mtafiti akibainika ametoa taarifa zenye ubora wa chini ya viwango, hupewa adhabu stahili na mwingine kunyanga’nywa usajili hadi hapo atakaooonekana amejirekebisha,’’ amesisitiza Mshiu.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amewataka wajiolojia nchini kuwa waadilifu na kuweka nidhamu ya juu wakati wa utekelezaji wa majukumu yao na kuongeza kwamba, sekta ya uziduaji inahitaji watu waadilifu.

‘’ Wizara imepewa jukumu la kusimamia sekta ya uziduaji na inahitaji uadilifu na nidhamu ya juu, sisi kama wizara tuko tayari kushirikiana kikamilifu nanyi na inatambua nafasi na kazi zinazofanywa na wajiolojia.

Naye, Rais wa Jumuiya ya Wajilojia Tanzania, Prof. Abdulkarim Mruma ameieleza hadhira hiyo kuhusu utajiri wa kijiolojia ambao nchi ya Tanzania imebarikiwa kuwa nao na kuelelezea namna bora ya kuitumia taaluma hiyo kwa maendeleo ya nchi na jamii nzima.

Sambamba na mkutano huo, zimetolewa tuzo kwa kampuni mbalimbali zilizochangia kufanyika kwa mkutano huo ikiwemo Mgodi wa Uchimbaji Dhahabu wa Geita, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Kampuni ya BarrickGold, Vilevile mkutano huo umetumika kutoa tuzo kwa wajiolojia wastaafu.

Awali, kabla ya kufanyika kwa mkutano huo, wataalamu hao walitembelea katika vivutio vya utalii kujionea na kujifunza utalii wa kijiolojia katika maeneo ya Serengeti, Ngorongoro na Olduvai Gorge.

 

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals