[Latest News]: MUHTASARI WA HOTUBA YA MHESHIMIWA ANTHONY PETER MAVUNDE (MB.), WAZIRI WA MADINI AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2026/2027

Tarehe : April 27, 2026, 3:22 p.m.
left

 

  1. UTANGULIZI

 

  1. Mheshimiwa Spika, baada ya kupokea taarifa iliyowasilishwa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini iliyochambua bajeti ya Wizara ya Madini, naomba kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu sasa likubali kupokea, kujadili na kupitisha Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 pamoja na Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Kawaida na Maendeleo ya Wizara ya Madini na Taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.

 

  1. Mheshimiwa Spika, naomba hotuba yangu yenye kurasa 137 iingizwe kwenye kumbukumbu rasmi za Bunge (Hansard) kama ilivyowasilishwa kwenye Ofisi za Bunge.

 

  1. Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuendelea kuijalia nchi yetu amani na baraka na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushiriki Mkutano huu wa Tatu (3). Tunamuomba aendelee kutujalia rehema, hekima, busara na umoja katika kujadili hotuba za Wizara mbalimbali ikiwemo Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 kwa nia ya kuendeleza Taifa letu na kuboresha ustawi na maendeleo ya Watanzania.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee nachukua fursa hii kumpongeza kwa dhati ya moyo wangu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake wenye maono mapana, mahiri, weledi na dhamira thabiti ya kuwaletea watanzania maendeleo jumuishi. Kwa wakati wote Mheshimiwa Rais ameendelea kuhimiza amani, uwajibikaji, utawala bora, umoja na mshikamano wa Kitaifa.

 

  1. Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kuimarisha na kulinda muungano, kusimamia masuala ya mazingira na usimamizi bora wa rasilimali zetu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

 

  1. Mheshimiwa Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuendelea kuiongoza Zanzibar vizuri. Hakika kiongozi huyu amekuwa nguzo imara katika kudumisha muungano. Vilevile, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais na kuthibitishwa na Bunge kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuendelea kuisimamia vyema Serikali.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee nitumie fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini na kunipa dhamana ya kusimamia Sekta ya Madini. Ni ahadi yangu kwake na kwa Bunge lako Tukufu pamoja na watanzania kwamba nitaendelea kuitumikia nafasi hii kwa uadilifu, uaminifu na kwa uwezo wangu wote ili kuendeleza sekta hii muhimu.

 

  1. Mheshimiwa Spika, napongeza hotuba iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu inayotoa mwelekeo wa utekelezaji wa kazi za Serikali ambayo imeonesha mafanikio ya uendeshaji wa shughuli za Serikali katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2025/2026, utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 pamoja na mwelekeo wa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.

 

  1. Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza wewe binafsi kwa kuaminiwa na kuchaguliwa na Waheshimiwa Wabunge kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kutokana na uzoefu na umahiri wako katika shughuli za Bunge tunaamini utalifanya Bunge kuendelea kuwa chombo imara, madhubuti na chenye kuaminika.

 

  1. Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Daniel Baran Sillo (Mb.) kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge letu Tukufu. Aidha, niwapongeze Wenyeviti wa Bunge kwa kuendelea kushirikiana nawe katika kuliongoza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa weledi mkubwa. Ni matarajio yetu kuwa chini ya uongozi wako, Bunge litaendelea kufanya maamuzi sahihi na yenye manufaa kwa maendeleo ya Taifa letu na kufanya liendelee kuheshimika ndani na nje ya nchi yetu.

 

  1. Mheshimiwa Spika, naomba niwapongeze sana Mheshimiwa CPA. Subira Khamis Mgalu (Mb.), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini pamoja na Mheshimiwa CPA. Simon Songe Lusengekile (Mb.), Makamu Mwenyekiti wa Kamati kwa kuteuliwa kuiongoza Kamati hii. Aidha, nawapongeza wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa kuteuliwa kutekeleza majukumu ya Kamati. Wizara inaishukuru Kamati kwa ushauri wake makini ambao imekuwa ikiutoa katika kuhakikisha kuwa sekta hii inakuwa na tija kwa Taifa na kuwanufaisha watanzania. Vilevile, ninaishukuru Kamati kwa kujadili kwa kina Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fungu 100, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 na kuyapitisha kwa kauli moja.

 

  1.  Mheshimiwa Spika, vilevile, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge la 13 kwa kuwa sehemu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Niombe ushirikiano wao katika kuendeleza sekta hii muhimu katika kujenga uchumi imara na maendeleo endelevu ya Taifa letu.

 

  1. Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wote kwa kuteuliwa kuongoza Wizara mbalimbali. Pia, niwapongeze viongozi wote waandamizi wa Serikali walioaminiwa na kuteuliwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushika nyadhifa mbalimbali, nawatakia utendaji mwema katika kutekeleza majukumu yao.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa, nitumie fursa hii kuwashukuru kwa dhati kabisa wapiga kura wangu wote wa Jimbo la Mtumba kwa kuniamini na kunichagua. Naamini mtaendelea kushirikiana nami katika kutekeleza majukumu yangu kama mwakilishi wenu katika Bunge hili Tukufu. Nawaahidi kuendelea kuwatumikia kwa nguvu zangu zote na kwa kipaji nilichojaliwa na Mwenyezi Mungu katika kuleta maendeleo ya jimbo na Taifa kwa ujumla.

 

  1. Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Steven Lemomo Kiruswa (Mb.), kwa kuteuliwa tena na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Naibu Waziri wa Madini. Aidha, namshukuru kwa dhati kabisa kwa ushirikiano anaonipatia katika kutekeleza majukumu ya Wizara. Hakika amekuwa ni msaada mkubwa kwangu katika kuhakikisha sekta hii inatimiza malengo yake. 

 

  1. Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru Eng. Yahya Ismail Samamba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini kwa kuratibu na kusimamia utendaji wa Wizara. Pia, nampongeza Bw. Msafiri Lameck Mbibo, Naibu Katibu Mkuu kwa kuendelea kumpatia ushirikiano Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini. Vilevile, nimshukuru Dkt. AbdulRahman Shabani Mwanga, Kamishna wa Madini kwa kutekeleza majukumu yake vizuri. Halikadhalika, nichukue fursa hii kuishukuru Menejimenti ya Wizara pamoja na wafanyakazi wote kwa ushirikiano na utendaji kazi mzuri katika kutekeleza majukumu yao.

 

  1. Mheshimiwa Spika, nawashukuru Wenyeviti wa Bodi kwa ushauri na utendaji kazi kwa ufanisi katika kusimamia Sekta ya Madini. Viongozi hao ni: Dkt. Janeth Lekashingo, Mwenyekiti wa Tume ya Madini; Bi. Yokbeth Myumbilwa, Mwenyekiti wa Bodi ya GST; IGP Mstaafu Mheshimiwa Balozi Simon Sirro, Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO; Mheshimiwa Balozi Wilson Masilingi, Mwenyekiti wa Kamati ya TEITI; Makamishna wa Tume ya Madini; na Wajumbe wa Bodi hizo.
  2. Mheshimiwa Spika, nawapongeza Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini: Eng. Ramadhani Lwamo (Katibu Mtendaji, Tume ya Madini); Eng. Ally Samaje (Mtendaji Mkuu, GST); Dkt. Venance Mwasse (Mkurugenzi Mkuu, STAMICO); Bi. Mariam Mgaya (Katibu Mtendaji, TEITI); na Eng. Ally Maganga (Mratibu wa Kituo cha Jemolojia Tanzania) kwa kuzisimamia kwa makini na weledi taasisi wanazoziongoza. Aidha, natoa shukrani zangu za dhati kwa Maafisa Madini Wakazi (RMO’s) na Maafisa Migodi Wakazi (MRO’s) kwa utekelezaji fanisi wa majukumu yao.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa naishukuru kwa moyo wa dhati familia yangu, mke wangu mpendwa Jacquelyne Moses Lupasa na watoto wangu Atarah na Allan kwa kunipa ushirikiano mkubwa na utulivu katika kusimamia majukumu yangu ya ubunge na uwaziri na kukubali kubeba baadhi ya majukumu ya familia.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa niungane na watanzania wenzangu kutoa pole kwa wananchi wa Jimbo la Peramiho kwa kuondokewa na aliyekuwa Mbunge wao Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama. Pia, nitoe pole kwa Wananchi wa Dar es Salaam kwa kuondokewa na Mheshimiwa Halima Idd Nassor aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum. Halikadhalika, nitoe pole kwa Wananchi wa jimbo la Isimani kwa kuondokewa na aliyekuwa Mbunge wao na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi. Mwenyezi Mungu awarehemu marehemu na awape faraja familia na wananchi waliokuwa wakiongozwa nao.

 

 

  1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa pole kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watanzania wote kutokana na vifo, majeraha, upotevu na  uharibifu wa mali na miundombinu kufuatia majanga mbalimbali yaliyosababishwa na mvua nyingi, ajali za barabarani, majini, moto na migodini.

 

  1. Mheshimiwa Spika, napenda niendelee kumpongeza Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini. Kwa mujibu wa utafiti wa taasisi ya Fraser ya Canada uliyofanyika mwaka 2025, Tanzania ilishika nafasi ya 4 Afrika na ya 34 duniani katika kiashiria cha kuvutia uwekezaji (Investment Attractiveness Index). Aidha, Tanzania ilipata alama 68.04 mwaka 2025 ikilionganishwa na alama 62.75 mwaka 2024. Vilevile, Tanzania ipo nafasi ya 15 duniani kwa hazina ya rasilimali madini ikiwa na alama 75.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ripoti ya Uwekezaji Tanzania ya Mwaka 2025, Sekta ya Madini imeendelea kuongoza kwa kuvutia Uwekezaji wa Mtaji wa Nje nchini (FDI stock), ambapo mwaka 2024 mtaji wa uwekezaji ulifikia dola bilioni 9.79 kutoka dola bilioni 9.15 mwaka 2023 na dola bilioni 8.64 mwaka 2022. Ongezeko hili ni matunda ya uhamasishaji wa uwekezaji, mazingira wezeshi kwa wawekezaji, upanuzi wa miradi iliyopo, uwekezaji wa faida zinazozalishwa ndani ya sekta na uunganishaji wa mitaji.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Tanzania imepiga hatua kubwa na ya kihistoria katika kuendeleza madini muhimu na madini mkakati kwa kuingia makubaliano ya kutekeleza miradi ya niobium, nikeli, kinywe na dhahabu katika maeneo mbalimbali nchini. Mathalani, tarehe 24 Machi 2026, Serikali ilisaini mkataba wa kuendeleza mradi wa uchimbaji wa madini ya niobium wa Panda Hill uliopo Mkoa wa Mbeya.

 

  1. Mheshimiwa Spika, mradi wa Panda Hill unatarajiwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa Afrika na kuiweka Tanzania katika nafasi ya wazalishaji wakubwa wanne duniani. Mradi huu unatarajia kuzalisha ajira 1,600 za moja kwa moja na 6,336 zisizo za moja kwa moja na ununuzi wa ndani wa takriban dola za Marekani bilioni 1.77 pamoja na uwajibikaji kwa jamii (CSR). Aidha, Serikali inatarajia kupata mapato ya takribani shilingi trilioni 2 kutokana na mrabaha, kodi na tozo, gawio la hisa za Serikali asilimia 16 zisizohafifishwa.

 

  1. Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa salamu za shukrani, pongezi, pole na baadhi ya mafanikio ya Sekta ya Madini, naomba sasa nijielekeze katika maeneo mahsusi ya hotuba yangu kama ifuatavyo:

 

  1. MWENENDO WA BIASHARA YA MADINI DUNIANI

 

  1. Mheshimiwa Spika, mwenendo wa biashara ya madini duniani umeendelea kubadilika kutokana na mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa na mahitaji ya soko. Mathalani, katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, bei ya dhahabu iliongezeka hadi kufikia wastani wa dola 4,190.47 kwa wakia kutoka dola 2,655.80 kwa kipindi kama hicho mwaka 2024/25. Ongezeko hili limechangiwa na mahitaji makubwa ya dhahabu kama hifadhi salama ya thamani ya fedha duniani.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine, bei ya almasi ilishuka kwa asilimia 5.39 kutoka wastani wa dola za Marekani 168.95 kwa karati katika kipindi cha kuanzia Julai 2024 hadi Machi 2025 na kufikia wastani wa dola za Marekani 159.84 katika kipindi kama hicho mwaka 2025/2026. Kushuka huko kwa bei kumetokana na uwepo wa almasi ya viwandani (synthetic diamond) zilizosababisha kupungua kwa uhitaji wa almasi asilia hususani katika masoko makubwa duniani yakiwemo ya China na Marekani. Aidha, bei ya makaa ya mawe imeshuka na kufikia wastani wa dola za Marekani 26.69 kwa tani katika kipindi cha kuanzia Julai 2025 hadi Machi 2026 ikilinganishwa na wastani wa dola za Marekani 40.75 kwa tani kwa kipindi kama hicho mwaka 2024/2025 sawa na upungufu wa asilimia 34.50. Upungufu huu wa bei unatoka na kupungua kwa mahitaji ya makaa ya mawe katika soko la dunia.

 

  1. Mheshimiwa Spika, mwenendo wa biashara ya madini ya Tanzanite duniani umeendelea kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa masoko ya uhakika kutokana na vikwazo vya kibiashara duniani na uwepo wa vito vya kutengeneza viwandani. Hali hiyo imesababisha kushuka kwa bei kutoka wastani wa dola za Marekani 2,433.96 kwa kilogramu katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025 na kufikia dola za Marekani 2,270.44 kwa kilogramu katika kipindi kama hicho mwaka 2025/2026 sawa na asilimia 6.72.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mahitaji ya madini mkakati na muhimu kama lithium, cobalt, nickel na rare earth elements yameendelea kuongezeka kutokana na matumizi yake katika teknolojia za kisasa na nishati safi. Hali hii inaipa Tanzania fursa ya kuongeza thamani ya madini haya ndani ya nchi ili kukuza mapato, ajira na mchango katika uchumi wa Taifa.

 

  1. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2025/2026

 

  1. Makadirio ya Mapato na Matumizi

 

  1. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2025/2026 Bunge lako Tukufu liliidhinisha jumla ya shilingi bilioni 224.98 kwa Wizara ya Madini, ambapo shilingi bilioni 100.38 zilitengwa kwa matumizi ya kawaida ikijumuisha shilingi bilioni 76.11 za matumizi mengineyo na shilingi bilioni 24.27 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa wizara na taasisi zake. Aidha, shilingi bilioni 124.60 zilitengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ikijumuisha shilingi bilioni 71.51 fedha za ndani na shilingi bilioni 53.09 fedha za nje.

 

  1. Fedha Zilizopokelewa na Kutumika

 

  1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026 Wizara imepokea jumla ya shilingi bilioni 82.90, ambapo shilingi bilioni 10.48 ni  za maendeleo zikiwa ni fedha za ndani na shilingi bilioni 72.43 za matumizi ya kawaida. Kati ya fedha za matumizi ya kawaida, shilingi bilioni 54.76 kwa ajili ya matumizi mengineyo na shilingi bilioni 17.66 kwa ajili ya mishahara ya watumishi.

 

  1. Utekelezaji wa Vipaumbele kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

 

  1. Kuimarisha Ukusanyaji wa Maduhuli

 

  1. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2025/2026, Wizara ilipangiwa kukusanya maduhuli ya shilingi trilioni 1.41 kutoka vyanzo mbalimbali. Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 1.20 zilipangwa kukusanywa na kuwasilishwa Hazina na shilingi bilioni 205.54 zilipangwa kukusanywa na kutumiwa na Taasisi zilizo chini ya Wizara. Hadi kufikia Machi 2026 shilingi trilioni 1.03 sawa na asilimia 114.94 ya lengo la makusanyo ya kipindi husika zimekusanywa na kuwasilishwa Hazina. Aidha, ili kuongeza maduhuli ya Serikali, Wizara imeimarisha usimamizi na ukaguzi kwenye maeneo ya uchimbaji, masoko ya madini, vituo vya ununuzi wa madini na mipaka ya nchi.

 

  1. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi 2026, biashara ya madini yenye thamani ya shilingi trilioni 4.90 imefanyika kupitia masoko na vituo vya ununuzi wa madini ikilinganishwa na shilingi trilioni 2.82 kwa kipindi kama hicho kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa madini nchini unaofanywa na baadhi ya wachimbaji na wafanyabiashara wa madini wasio waaminifu. Katika kipindi cha kuanzia Julai 2025 hadi Machi 2026, Wizara kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali imefanikiwa kukamata madini ya aina mbalimbali yenye thamani ya shilingi bilioni 3.31 katika matukio 55 kwenye baadhi ya mikoa ya kimadini. Aidha, madini yaliyokamatwa yalitaifishwa na Serikali na watuhumiwa walifikishwa kwenye vyombo vya Sheria. Ni rai yangu kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kuzingatia Sheria za Nchi kuhusiana na biashara ya madini.

 

  1. Mheshimiwa Spika, mapato ya fedha za kigeni yatokanayo na mauzo ya madini nje ya nchi yamekuwa yakiimarika mwaka hadi mwaka. Mwaka 2025, thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi ilikuwa dola za Marekani milioni 5,401.9 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 4,119.9 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 31.1. Aidha, mwaka 2025 thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi yalichangia asilimia 52.57 ya mauzo yote ya bidhaa za asili na zisizo za asili yaliyouzwa nje ikilinganishwa na asilimia 45.17 mwaka 2024.  Vilevile, kwa upande wa mauzo ya bidhaa zisizo za asili pekee, Sekta ya Madini ilichangia asilimia 63.73 mwaka 2025 ikilinganishwa na mchango wa asilimia 56.99 mwaka 2024. Pia, thamani ya mauzo ya dhahabu iliongezeka kutoka dola za Marekani milioni 3,419.6 mwaka 2024 na kufikia dola za Marekani milioni 4,753.9 mwaka 2025 sawa na ongezeko la asilimia 39.0.

 

  1. Kuongeza Mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa
  1. Mheshimiwa Spika, mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa umekuwa ukiimarika mwaka hadi mwaka. Mchango huo uliongezeka kutoka asilimia 9.1 mwaka 2023 na kufikia asilimia 10.1 mwaka 2024. Aidha, hadi kufikia kipindi cha robo tatu ya mwaka 2025  (Januari – Septemba) wastani wa mchango wa sekta umefikia asilimia 11.9. Mwenendo huu umechangiwa na kuongezeka kwa uwekezaji katika Sekta ya Madini.

 

  1. Kuendeleza Mnyororo wa Thamani katika Madini Muhimu na Madini Mkakati
  1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, Wizara kupitia Tume ya Madini imetoa leseni 454 za Madini Muhimu na Madini Mkakati yakiwemo madini ya kinywe (271), nickel (136), cobalt (2), lithium (6), heavy mineral sands (11) na rare earth elements (28). Utoaji wa leseni hizi unaendelea kuweka msingi thabiti wa kukuza uwekezaji katika utafutaji na uendelezaji wa madini muhimu na madini mkakati nchini.
  1. Kuhamasisha Uwekezaji na Uongezaji Thamani Madini
  1. Mheshimiwa Spika, katika kuhamasisha uwekezaji kwenye Sekta ya Madini, Wizara imeendelea kutangaza fursa na kutoa elimu kwa umma kupitia ziara za viongozi, vyombo vya habari na mikutano ya kitaifa, kikanda na kimataifa. Aidha, Wizara ilishiriki katika mikutano, makongamano na maonesho ya kimataifa nane (8) ikiwemo Future Minerals Forum Saudi Arabia, Mining Indaba Afrika Kusini, ZIMEC Zambia, mikutano ya ADPA na Maonesho ya 69 ya Vito Bangkok Thailand. Vilevile, ndani ya nchi Wizara iliandaa na kushiriki maonesho matano (5) yakiwemo Maonesho ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini Geita, Maonesho ya Sabasaba Dar es Salaam na Maonesho ya Biashara Zanzibar. Jitihada hizi zimeongeza mwamko wa uwekezaji na kuimarisha taswira ya Tanzania kimataifa.

 

  1. Mheshimiwa Spika, watanzania na wadau  wameendelea kuelimishwa  na kufahamishwa  kuhusu uwepo wa fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini ikiwemo sheria, kanuni na miongozo inayosimamia sekta. Aidha, elimu imeendelea kutolewa kupitia njia mbalimbali za mawasiliano ikiwa ni pamoja na Jarida la Mtandaoni la Madini na Uchumi, programu maalumu za urushwaji wa vipindi mubashara vilivyoelezea masuala mbalimbali yanayohusu Sekta ya Madini. Vyombo hivyo ni pamoja na TBC, Clouds Media, Crown Media, ITV, Kiss FM, Azam Media, Wasafi Media, VOA, BBC, DW, TRT, Radio France, ZBC na Morning Star.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Wizara imekamilisha uandaaji wa Mkakati wa Uongezaji Thamani Madini. Mkakati huo unatoa mwelekeo kwa Serikali wa kubadilisha Sekta ya Madini kutoka kwenye uuzaji wa madini ghafi na kuelekea kwenye kuuza madini yaliyoongezewa thamani ndani ya nchi. Lengo kuu ni kutumia rasilimali madini kama njia ya kufungamanisha Sekta ya Madini na Sekta nyingine za kiuchumi ikiwemo viwanda. Utekelezaji wa mkakati huo utachochea ongezeko la thamani ya madini yetu na kuongeza viwanda vitakavyosaidia upatikanaji wa ajira, Pato la Taifa, ubunifu, kuongeza ujuzi na kuimarisha ushindani wa bidhaa zitokanazo na madini katika masoko ya ndani na nje ya nchi kupitia mnyororo imara wa uongezaji thamani.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia shughuli za uongezaji thamani madini nchini kupitia viwanda sita (6) vya kusafisha dhahabu vilivyopo mikoa ya Dodoma (1), Shinyanga (1), Geita (2), Dar es Salaam (1) na Mwanza (1). Aidha, Wizara inaendelea kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kuyeyusha madini ya Shaba, Nikeli, Bati na Chumvi katika mikoa ya Dodoma, Shinyanga, Kagera, Mbeya, Lindi na Pwani. Sambamba na hilo, Wizara inaendelea kushirikiana na wamiliki wa viwanda vya kusafisha dhahabu ili kupata ithibati ya LBMA kwa ajili ya kuwezesha viwanda hivyo kutambulika katika masoko ya kimataifa.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuimarisha shughuli za uongezaji thamani madini ya vito na metali za thamani nchini kwa kuendelea na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa jengo pacha la ghorofa 8 katika Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) ili kuongeza uwezo wa kutoa mafunzo ya uongezaji thamani madini.

 

 

 

  1. Kuimarisha Uendeshaji wa Minada na Maonesho ya Madini ya Vito
  1. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) iliendesha mnada mmoja (1) wa ndani wa madini ya vito uliofanyika kielektroniki Jijini Arusha Mwezi Novemba 2025. Katika mnada huo madini yenye thamani ya shilingi milioni 231.25 yalinunuliwa. Hata hivyo, Wizara inaendelea kuhamasisha na kuongeza mwamko wa ushiriki wa wadau katika minada ya madini ya vito.

 

  1. Kuongeza Uwekezaji kwenye Tafiti za Kina za Madini
  1. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Taasis ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imefanya utafiti wa jiofizikia kwa kutumia ndege nyuki katika maeneo ya Geita, Manyara na Lindi ambapo taarifa muhimu za kina za jiolojia zilibainishwa katika maeneo hayo. Sambamba na hilo, umefanyika pia utafiti wa kina wa jiofizikia (High Resolution Airborne Geophysical Survey) katika maeneo ya leseni za STAMICO zilizoko Mkoa wa Lindi, hatua inayolenga kuongeza uelewa wa kina kuhusu rasilimali zilizopo. Utafiti huo uliofanyika umewezesha Serikali kubaini uwezekano wa matumizi ya ndege nyuki kutumika katika upatikanaji wa taarifa za kina za jiofizikia kwenye leseni ndogo za uchimbaji wa madini. Hivyo, hatua hii itasaidia kutumia teknolojia ya ndege nyuki katika kupata taarifa za kina za jiofizikia kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo.

 

  1. Mheshimiwa Spika, GST imekamilisha taratibu za kumpata mkandarasi wa kufanya utafiti wa kina wa jiofizikia katika vitalu viwili (2) vya kimkakati vilivyoko kusini-magharibi mwa nchi, vyenye ukubwa wa takribani kilomita za mraba 176,676.45 sawa na asilimia 18 ya eneo lote la nchi. Utekelezaji wa utafiti huu unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa taarifa za kina za jiofizikia kutoka asilimia 16 ya sasa hadi kufikia asilimia 34.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kutokana na kutokuwepo kwa taarifa za kina za jiofizikia kwenye baadhi ya maeneo ya nchi, Wizara imeendelea kuhamasisha kampuni mbalimbali kufanya tafiti za kina kwenye maeneo ya leseni zao kama hatua za awali za utafutaji madini. Mathalani, hivi karibuni kampuni ya Barrick imefanya utafiti wa kina wa jiofizikia kwa kutumia helikopta katika maeneo ya Msalala, Nzega, Igunga, Mbogwe na Nyang’hwale kwa ajili ya kubaini uwepo wa maeneo mapya yenye madini.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia GST imeendelea na ujenzi wa Mfumo wa Usimamizi na Usambazaji wa Taarifa za Jiosayansi na Rasilimali za Madini ambapo hadi kufikia Machi 2026 ujenzi wa mfumo huo umefikia asilimia 45. Aidha, kukamilika kwa mfumo huo kutaimarisha usimamizi na upatikanaji wa taarifa za miamba na madini yaliyopo nchini.

 

  1. Kuwarasimisha na Kuwaendeleza Wachimbaji Wadogo
  1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi, 2026 jumla ya leseni 8,878 za uchimbaji mdogo zimetolewa na Wizara kupitia Tume ya Madini. Aidha, STAMICO inaendelea kusaidia wachimbaji wadogo kwa kutoa huduma za kitaalam katika utafiti, uchimbaji, uchenjuaji na utunzaji wa mazingira. Katika kipindi husika jumla ya wachimbaji 451 wamepatiwa mafunzo kupitia vituo vya mfano vya Lwamgasa, Katente na Itumbi.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia STAMICO imetoa huduma ya uchorongaji katika maeneo mbalimbali, ambapo jumla ya mita 3,896.59 zilichorongwa kwa ajili ya utafutaji wa dhahabu. Kwa upande wa wazalishaji chumvi wadogo, ujenzi wa jengo la kiwanda cha kusafisha chumvi kilichopo Nangurukuru Wilaya ya Kilwa umekamilika, na hatua inayofuata ni kukamilisha usimikaji wa mitambo.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Tume ya Madini imefanya ufuatiliaji wa kutambua maeneo ya kugawiwa kwa wachimbaji wadogo ambapo hadi sasa jumla ya maeneo 99 yamependekezwa kwa ajili ya uchambuzi. Aidha, maeneo mawili (2) yametengwa katika Mikoa ya kimadini ya Mbogwe - Msasa (Leseni 35 zimetolewa) na Lindi - Ntaka Hill (Leseni 69 zimetolewa).

 

  1. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu na kuwezesha ushiriki wa wachimbaji wadogo katika warsha, makongamano, mikutano na majukwaa ya kitaifa na kimataifa kwa ajili ya kujifunza teknolojia mbalimbali pamoja na kutafuta fursa za biashara.  Mathalani, chini ya uratibu wa FEMATA, jumla ya wachimbaji wadogo 31 walifanya ziara ya mafunzo nchini Uturuki kuanzia tarehe 3 hadi 14 Septemba 2025.
  2. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, Wizara kupitia Tume ya Madini imesaini Hati ya Makubaliano na Benki ya CRDB kwa ajili ya upatikanaji wa mikopo kwa wachimbaji wadogo wa madini. Aidha, kikundi cha wachimbaji wadogo cha Songwe Gold Family – Saza mkoani Songwe kinatarajiwa kupata mkopo wa shilingi bilioni 50 kutoka benki ya CRDB ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano hayo. Nitumie fursa hii kuzishukuru benki za CRDB, NMB, NBC, AZANIA na KCB kwa kuendelea kuwakopesha wachimbaji wadogo. Hivyo, naomba kutoa wito kwa benki nyingine nchini kuendelea kuwaamini na kuwakopesha wachimbaji wadogo.

 

  1. Kuzijengea Uwezo Taasisi Zilizo Chini ya Wizara ya Madini

 

  1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia Julai 2025 hadi Machi 2026, Wizara na Taasisi zake zimejaza nafasi 147 kwa utaratibu wa uhamisho (55) na ajira mpya (92). Aidha, kupitia uhamisho huo, Wizara imepata watumishi (24), Tume ya Madini (17), TEITI (8) na GST (6). Vilevile, kwa upande wa ajira mpya Wizara imepata watumishi (9), STAMICO (1), Tume ya Madini (66), GST (12) na TGC (4). Kadhalika, kwa upande wa mafunzo kwa watumishi, Wizara na Taasisi zake zimewawezesha watumishi 455 kupata mafunzo. Kati ya hao watumishi 347 walipata mafunzo ya muda mfupi na 108 ya muda mrefu katika masuala mbalimbali yanayohusu Sekta ya Madini.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuhakikisha kuwa Taasisi zilizo chini yake zinatekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuzipatia vitendea kazi. Tume ya Madini imewezeshwa vifaa vya masoko na TEHAMA; STAMICO imewezeshwa kupata leseni mbili za utafiti wa madini ya nikeli na adimu (REE); GST imewezeshwa upatikanaji wa vitendea kazi kwa ajili ya utafiti wa madini ikiwemo magari manne (4); TGC imewezeshwa kuboresha miundombinu ya kutolea mafunzo, huduma za uzalishaji wa bidhaa kwa lengo la kukuza shughuli za uongezaji thamani madini nchini; na TEITI imewezeshwa kwa kupewa jengo kwa ajili ya ofisi lililopo mji wa Serikali Mtumba. Aidha, Wizara imeendelea na taratibu za kuidhinishwa kwa TGC kuwa Taasisi inayojitegemea. Hatua hii itaiwezesha TGC kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

 

  1. Utekelezaji wa Maeneo Mengine ya Wizara katika Mwaka wa Fedha 2025/2026

 

  1. Mining Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri

 

  1. Mheshimiwa Spika, Wizara imekamilisha Andiko la Mining Vision 2030 lililozingatia nguzo tano (5) ambazo ni: kuwa na taarifa za jiosayansi; kuimarisha mfumo wa kisheria na kitaasisi; kuimarisha ufungamanishaji wa Sekta ya Madini na sekta nyingine za kiuchumi na uwekezaji; kukuza uchimbaji mdogo wa madini; na kuimarisha usimamizi wa mazingira. Kwa kuzingatia nguzo hizo Sekta ya Madini itafikia malengo na matarajio ya DIRA 2050.

 

  1. Programu ya Mining for a Brighter Tomorrow – MBT

 

  1. Mheshimiwa Spika, Wizara imeanza kutekeleza Mpango wa MBT ambao ni wa miaka mitano kuanzia mwaka 2025/2026 hadi 2029/2030. Mpango huo unalenga kuongeza ushiriki wa vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum katika mnyororo wa thamani kwenye Sekta ya Madini. Aidha, Malengo Mahsusi ya Mpango wa MBT ni pamoja na kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya sekta, kujenga uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za mnyororo wa thamani wa madini, na kuimarisha ujumuishi na manufaa yatokanayo na Sekta ya Madini kwa vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum.

 

  1. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza malengo ya Mpango wa MBT, Wizara imetoa jumla ya leseni 273 za uchimbaji wa madini kwa vikundi 183 katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mara, Kagera, Shinyanga, Morogoro, Dodoma na Njombe. Aidha, Wizara ilitoa elimu kuhusu usalama, afya, utunzaji wa mazingira na usimamizi wa rasilimali fedha kwa wanufaika wa leseni zilizotolewa. Vilevile, Wizara imeendelea kuratibu ushiriki wa makundi hayo kupitia miradi mbalimbali ya uchimbaji na biashara ya madini ikiwemo mradi wa Nyamongo kwa kushirikiana na Mgodi wa dhahabu wa North Mara katika Wilaya ya Tarime, Mkoa wa Mara. Sambamba na hilo, mpango huu unatekelezwa katika maeneo ya Mirerani Mkoa wa Manyara, Mbogwe na Nyang’hwale Mkoa wa Geita. Wizara pia imeendelea kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa MBT.

 

  1. Kuwajengea Uwezo Wataalam kwenye Maeneo Muhimu katika Sekta ya Madini

 

  1. Mheshimiwa Spika, ili kukidhi mahitaji ya wataalam na uwepo wa teknolojia mahsusi katika mnyororo wa thamani wa madini nchini, Wizara imekamilisha taratibu za kuwapeleka wataalamu masomoni ndani na nje ya nchi katika fani mbalimbali zikiwemo: ukadiriaji wa mashapo (resource estimation); modeli za kifedha (financial modelling); ukaguzi na usimamizi wa rasilimali madini; uthaminishaji wa madini; ukataji wa madini ya vito; utengenezaji wa bidhaa za usonara na uongezaji thamani madini. Katika Mwaka wa Fedha 2025/2026, Wizara imepanga kuwajengea uwezo jumla ya watumishi nane (8) katika maeneo ya ukadiriaji mashapo (resource estimation), modeli za kifedha (financial modelling) na ukaguzi wa fedha (financial auditing) migodini.

 

  1. Kuboresha Usimamizi wa Shughuli za Madini Kidijitali

 

  1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, Wizara imeendelea na taratibu za kuanzisha Mfumo wa Usimamizi wa Sekta ya Madini Kidijitali utakaojulikana kama “Mineral Sector Management Information System - MSMIS”. Mfumo huu unalenga kuimarisha usimamizi, uratibu na upatikanaji wa taarifa za Sekta ya Madini kwa kutumia teknolojia za kidijitali, sambamba na jitihada za Serikali za kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma za umma. Hatua za awali zimeanza kutekelezwa ikiwa ni pamoja na kufanya uchambuzi wa mahitaji ya mfumo, kubainisha wadau watakaohusika katika utekelezaji wa mfumo na maandalizi ya nyaraka muhimu zinazohitajika.

 

  1. Mpango Mkakati wa Madini Muhimu na Madini Mkakati (Critical and Strategic Minerals Strategy)

 

  1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, Wizara imekamilisha uandaaji wa Mpango Mkakati wa Madini Muhimu na Madini Mkakati. Utekelezaji wake utaanza kutumika mara baada ya kuidhinishwa kwa orodha ya Madini Muhimu na Madini Mkakati. Mkakati huo ni moja ya nyenzo za kutekeleza Sera ya Madini iliyohuishwa pamoja na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Muda Mrefu (LTPP 2050) ili kufikia malengo ya DIRA 2050.

 

  1. Marekebisho ya Sheria ya Madini Sura 123 na Kanuni zake

 

  1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi rejewa, Wizara imefanya marekebisho ya Kanuni za Wajibu wa Wamiliki wa Leseni za Madini kwa Jamii za Mwaka 2025 na kutangazwa katika Tangazo la Serikali Na. 563 la tarehe 12 Septemba, 2025 pamoja na Tangazo la Serikali Na. 692 la tarehe 19 Desemba, 2025. Kanuni hizo ni: Kanuni ya 6 ili kuboresha muundo wa kamati ya wataalamu kwa lengo la kuongeza ufanisi; kuongeza kanuni ndogo ya 7(3) iliyolenga kupunguza gharama za utendaji wa kamati ya wataalamu na kuleta ufanisi katika utekelezaji wa miradi; Kanuni za 8 na 9 kwa kuweka ukomo wa muda wa kuwasilisha mipango; Kanuni ya 15 imefutwa na kutungwa kanuni mpya inayofafanua zaidi majukumu ya wamiliki wa leseni za madini ikiwemo kuwasilisha taarifa za fedha na miradi; na Kanuni ndogo ya 16(6) inayohusu usimamizi, ufuatiliaji na ukaguzi wa utekelezaji wa mipango ya wajibu wa wenye leseni kwa jamii imeongezwa.

 

  1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi rejewa, Wizara imetunga kanuni mpya, Kanuni za Leseni Ndogo ya Uchenjuaji wa Madini za Mwaka 2025 na kutangazwa katika Tangazo la Serikali Na. 572 la tarehe 12 Septemba, 2025. Kanuni hizi zitaboresha shughuli za Sekta ya Madini kwa kuwatambua na kutoa leseni kwa wachenjuaji wadogo.

 

  1. Utekelezaji wa Shughuli za Taasisi Zilizo Chini ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

 

  1. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuzisimamia na kuziwezesha taasisi zake tano (5) ili ziendelee kutekeleza majukumu kwa ufanisi na kuzingatia Sera, Sheria na Miongozo inayosimamia Sekta ya Madini. Taasisi hizo ni Tume ya Madini; Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST); Shirika la Madini la Taifa (STAMICO); Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC); na Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI).

 

  1. Mheshimiwa Spika, baadhi ya majukumu yaliyotekelezwa na taasisi hizo ni: utoaji na usimamizi wa leseni za madini; Ukaguzi wa Masuala ya Usalama, Afya na Mazingira; kufanya utafiti wa Jiosayansi na Uboreshaji wa Kanzidata ya Taifa ya Taarifa za Miamba na Madini; usimamizi wa vituo vya mfano vya wachimbaji wadogo wa madini; kusimamia utekelezaji wa miradi ya ubia; udahili na utoaji wa mafunzo kuhusu uongezaji thamani madini; na uandaaji na uwekaji wazi ripoti ya ulinganifu wa mapato ya Serikali na mapato yaliyowasilishwa na kampuni  za uziduaji.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

  1. MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2026/2027

 

  1. Mheshimiwa Spika, katika kuandaa Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2026/2027, Wizara imezingatia miongozo ifuatayo: Mwongozo wa Kitaifa wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti wa Mwaka 2026/2027; Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025; Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027 – 2030/2031 (FYDP IV); DIRA 2050; Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Muda Mrefu (LTPP 2050); Makubaliano ya Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi; Agenda 2063 ya Maendeleo ya Afrika; Africa Mining Vision; Sera ya Madini ya Mwaka 2009; Mpango Mkakati wa Wizara; Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030; Kifungu cha 21 cha Sheria ya Bajeti, Sura 439; Maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na viongozi wengine wa kitaifa pamoja na Maelekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo yaliyotolewa kwa nyakati tofauti.

 

  1. Vipaumbele kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

 

  1. Kuimarisha Ukusanyaji wa Maduhuli

 

  1. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali, Wizara itaendelea kuimarisha ukaguzi na usimamizi wa uchimbaji wa madini ili uweze kunufaisha nchi na wawekezaji; kuimarisha  na kusimamia masoko na vituo vya ununuzi wa madini nchini; na kuendeleza mikakati ya kuimarisha usimamizi wa madini ujenzi na viwandani, soko la tanzanite na madini mengine ya vito hapa nchini ili kuongeza mapato yatokanayo na madini hayo.
  2. Mheshimiwa Spika, Wizara imepanga kutekeleza mikakati ya kuimarisha utekelezaji wa Sheria ya Madini, ikiwemo kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa madini kwenda nje ya nchi na biashara haramu ya madini nchini. Aidha, katika kuendelea kuimarisha udhibiti na kuzuia utoroshaji wa madini ya tanzanite, Wizara kupitia Tume ya Madini, itakamilisha ununuzi wa kofia zenye kamera maalum kwa ajili ya ukaguzi na itahakikisha wakaguzi na wathaminishaji wa madini hayo wanatumia kofia hizo ili kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa mwenendo wa uzalishaji na biashara ya madini kwenye Eneo Tengefu la Mirerani.

 

  1. Kuongeza Mchango wa Sekta ya Madini Kwenye Pato la Taifa

 

  1. Mheshimiwa Spika, katika kuongeza mchango wa wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa, Wizara imepanga kutekeleza mikakati ifuatayo: kuhamasisha shughuli za utafiti wa madini na uanzishaji wa migodi mipya, kuimarisha usimamizi  wa migodi ya uchimbaji; kuboresha mfumo wa usimamizi wa madini ya ujenzi na ya viwandani; kusimamia utekelezaji wa Sheria inayoitaka migodi mikubwa kuajiri, kununua huduma na bidhaa kutoka hapa nchini na kuhamasisha ushiriki wa  Watanzania katika mnyororo wa uchumi wa madini; na kuendelea kuimarisha mazingira wezeshi ya kisera na kisheria. Aidha, Wizara itahakikisha kuwa wawekezaji waliopewa leseni za uchimbaji wa madini wanaanza uzalishaji mara baada ya kukamilisha taratibu za matakwa ya kisheria.

 

 

 

  1. Kuendeleza Mnyororo wa Thamani Katika Madini Muhimu na Madini Mkakati

 

  1. Mheshimiwa Spika, madini muhimu na madini mkakati ni madini ambayo yana mahitaji makubwa kwenye maendeleo ya uchumi na ulinzi wa Taifa. Madini hayo ni pamoja na lithium, graphite, helium, nickel, cobalt, titanium, copper, aluminium, niobium na rare earth elements ambayo yanatumika kutengeneza vifaa vya teknolojia ya kisasa ikiwemo nishati safi.

 

  1. Mheshimiwa Spika, ili kuongeza manufaa yatokanayo na madini muhimu na madini mkakati kwa uchumi wa Taifa, Wizara imepanga kuendeleza mnyororo wa thamani katika madini hayo kwa kufanya yafuatayo: kuhamasisha uwekezaji katika utafutaji na uchimbaji wa madini muhimu na madini mkakati; kufanya utafiti wa mahitaji ya madini mkakati ili kuyafikia masoko mbalimbali duniani; kutoa leseni za utafutaji, uchimbaji na biashara ya madini muhimu na madini mkakati; na kukamilisha na kutekeleza mkakati wa uendelezaji na uvunaji wa madini hayo nchini. Naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba watanzania wananufaika ipasavyo na uwepo wa rasilimali za madini muhimu na madini mkakati hapa nchini.

 

  1. Kuhamasisha Uwekezaji katika Uongezaji Thamani Madini

 

  1. Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya uchenjuaji, uyeyushaji, usafishaji na utengenezaji wa bidhaa zitokanazo na madini; kuendelea kutoa ushirikiano kwa wamiliki wa viwanda vya usafishaji wa madini ya dhahabu nchini ili kupata ithibati ya LBMA; na kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya Kituo cha Jemolojia Tanzania ili kiweze kutoa mafunzo na huduma kwenye mnyororo wa uongezaji thamani madini kwa ufanisi.

 

  1. Mheshimiwa Spika, ili kuhamasisha uwekezaji katika uongezaji thamani madini, Serikali imetenga eneo la Buzwagi lililopo Wilaya ya Kahama kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani madini na viwanda vya uzalishaji bidhaa migodini.

 

  1. Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza kutangaza fursa za uwekezaji nchini, Wizara kwa kushirikiana na Chemba ya Migodi Tanzania (Tanzania Chamber of Mines) itafanya Mkutano wa saba (7) wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini. Mkutano huo unatarajiwa kufanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere kuanzia tarehe 19 hadi 21 Novemba, 2026 Jijini Dar es Salaam. Mkutano huu utawakutanisha kwa pamoja makundi mbalimbali ya wataalamu wa masuala ya madini, Wakurugenzi na Watendaji Wakuu wa kampuni za utafiti na uchimbaji wa madini, kampuni za utafiti na uchimbaji wa madini, watoa huduma, wafanyabiashara na wawekezaji katika Sekta ya Madini kutoka ndani na nje ya nchi yetu.

 

  1. Kuimarisha Uendeshaji wa Minada na Maonesho ya Madini ya Vito

 

  1. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza kipaumbele hiki Wizara itafanya yafuatayo: uendelezaji wa minada na maonesho ya madini ya vito ya Arusha (Arusha Gem Fair - AGF) na Minada ya madini ya vito ya kimataifa ili kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara ya madini ya vito (Gemstone Hub); na kuimarisha uendeshaji wa viwanda vya kuongeza thamani madini nchini.

 

  1. Kuongeza Uwekezaji kwenye Tafiti za Kina za Madini

 

  1. Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa shughuli hii, Wizara itafanya tafiti za kina za jiosayansi ikiwemo jiofizikia (High-resolution Airborne Geophysical Survey) ili kuainisha uwepo wa madini mbalimbali yakiwemo madini muhimu na madini mkakati. Aidha, Wizara kupitia GST itaendelea na ujenzi wa mfumo wa kusimamia taarifa za jiosayansi. Vilevile, Wizara itaendelea kushirikisha wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ili kufanya tafiti za madini katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuongeza wigo wa eneo la nchi lililofanyiwa utafiti wa kina wa madini.

 

  1. Kuwarasimisha na Kuwaendeleza Wachimbaji Wadogo

 

  1. Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea na taratibu za kuwarasimisha na kuwaendeleza wachimbaji wadogo kwa kuweka mazingira wezeshi yatakayowahamasisha kufanya uwekezaji; kuendelea kuhamasisha taasisi za kifedha kutoa mikopo ya fedha na vifaa kwa wachimbaji wadogo; kuandaa Mpango wa kuwatambua na kuwaendeleza wachimbaji wadogo nchini kupitia Mfuko wa Dhamana kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha; kuboresha utendaji wa vituo vya mfano ili kuimarisha utoaji wa huduma  na mafunzo kwa wachimbaji wadogo; na kuimarisha huduma za uchorongaji kwa wachimbaji wadogo.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kuimarisha utekelezaji wa mipango ya kuwawezesha wachimbaji wadogo ili waweze kufanya shughuli zao kwa tija kwa kuwatengea maeneo na kuwawezesha kupata leseni kwenye maeneo yenye taarifa za msingi za jiolojia kupitia Programu ya MBT; kuchukua hatua za ufutaji wa leseni za utafiti ambazo hazifanyiwi kazi na kuzirejesha Serikalini ili kupangwa vyema na kugaiwa kwa wachimbaji wadogo; kuhamasisha wachimbaji wadogo kushiriki mikutano, maonesho na makongamano mbalimbali  ndani na nje ya nchi  kwa lengo la kujifunza na kutangaza shughuli zao; kuendesha makongamano kwenye mikoa ya kimadini kwa ajili ya kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo na wananchi kwa ujumla kuhusu masuala ya sheria na kanuni mbalimbali za madini zikiwemo za Local Content, CSR, Haki Madini na Haki Ardhi; na kuhamasisha wachimbaji wadogo kushiriki kwenye minada na maonesho ya madini ya vito nchini ili kupanua wigo wa biashara.

 

  1. Mheshimiwa Spika, ili kuwawezesha wachimbaji wadogo waweze kunufaika na rasilimali madini, Serikali itaendelea kuitumia Timu ya Wataalamu wenye uzoefu na masuala ya fedha, madini na sheria kwa ajili ya kutoa mapendekezo ya namna ya kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata mitaji na msaada wa kiufundi. Hatua hii itawawezesha wachimbaji hao kufanya uchimbaji wenye tija na kunufaika zaidi kiuchumi. Aidha, Wizara kupitia STAMICO itaendelea kuwalea na kuwaendeleza wachimbaji wadogo kwa kuwajengea vituo vya mfano katika maeneo yenye uchimbaji mdogo.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi iweze kuanzisha vituo vya kuuza na kukodisha  vifaa na mashine mbalimbali za kufanyia shughuli za madini kwa lengo la kuwawezesha wachimbaji wadogo kutekeleza shughuli za madini kwa tija ili kuongeza mchango wao katika Pato la Taifa.

 

  1. Kuzijengea Uwezo Taasisi Zilizo Chini ya Wizara ya Madini

 

  1. Mheshimiwa Spika, ili kuzijengea uwezo taasisi, Wizara itafanya yafuatayo: kuiwezesha  Tume ya Madini  kupata rasilimali fedha na vifaa kwa ajili ya  kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi; kuendelea kuimarisha STAMICO ili ishiriki kikamilifu kwenye uwekezaji wa shughuli za madini.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kuimarisha GST ili iweze kufanya tafiti za jiosayansi kwa lengo la kubaini maeneo mapya yenye uwepo wa madini; kuimarisha TGC ili iweze kusimamia na kuhamasisha uwekezaji katika shughuli za uongezaji thamani madini ya vito na metali za thamani; na kuiwezesha TEITI kupata rasilimali mbalimbali ikiwemo vifaa na vitendea kazi ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

 

  1. Maeneo Mengine Yatakayotekelezwa na Wizara katika Mwaka wa Fedha 2026/2027

 

  1. Mining Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri

 

  1. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Madini itaendelea na utekelezaji wa “Mining Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri” inayoweka matamanio ya kuwa na usimamizi thabiti na endelevu wa rasilimali madini ili kukuza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa; na kuboresha maisha ya watanzania kupitia shughuli za madini.

 

  1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2026/2027 Wizara kupitia GST inatarajia kufanya tafiti za kina za jiosayansi ikiwemo utafiti wa kina wa jiofizikia (High Resolution Airborne Geophysical Survey). Utafiti huo unatarajia kuongeza taarifa za kina za jiofizikia kutoka asilimia 16 ya sasa hadi kufikia asilimia 34.  Aidha, katika utekelezaji wa Mining Vision 2030 Serikali itaendelea na jitihada za tafiti za kina ili angalau kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030. Taarifa hizi zitaongeza uelewa wa jiolojia ya nchi yetu na hivyo kuvutia na kuboresha mazingira ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuchochea ufungamanishaji na sekta nyingine za kiuchumi hususan Sekta za Viwanda, Kilimo, Ujenzi, Fedha na nyingine zinazotoa huduma kwenye Sekta ya Madini. Mheshimiwa Spika, binafsi nikushukuru wewe na Bunge lako Tukufu kwa kuniunga mkono katika kuhakikisha utafiti wa kina wa madini unafanyika katika nchi yetu kwa kiasi kikubwa.

 

  1. Programu ya Mining for a Brighter Tomorrow – MBT
  1. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Madini itaendelea kutekeleza Programu ya MBT kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2025/2026 hadi 2029/2030. Programu hii ni ya mageuzi katika Sekta ya Madini ambayo imeanzishwa kwa ajili ya kuboresha ushiriki wa wachimbaji wadogo ikiwemo wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum katika fursa zilizopo kwenye mnyororo wa thamani wa madini.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Programu ya MBT inatarajiwa kuongeza ushiriki wa vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum kwenye Uchumi jumuishi kupitia Sekta ya Madini na kuwawezesha kupata kipato na kuwaongezea fursa za ajira.

 

 

  1. Kuwajengea Uwezo Wataalam kwenye Maeneo Muhimu katika Sekta ya Madini
  1. Mheshimiwa Spika, ili kukidhi mahitaji ya rasilimali watu katika shughuli za madini na uhitaji wa teknolojia mahsusi katika mnyororo wa thamani wa madini nchini, Wizara imetenga fedha za kuwajengea uwezo wataalamu katika Sekta ya Madini kwa kuwasomesha ndani na nje ya nchi kupitia mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu. Mafunzo hayo yatajikita zaidi katika fani za ukadiriaji wa mashapo (resource estimation), modeli za kifedha (financial modelling), ukaguzi wa fedha na rasilimali madini, uthaminishaji wa madini na uongezaji thamani madini ikiwemo madini ya vito, madini muhimu na madini mkakati.

 

  1. Kuboresha Usimamizi wa Shughuli za Madini Kidijitali
  1. Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea na hatua za ukamilishaji wa ujenzi wa Mfumo wa Usimamizi wa Sekta ya Madini Kidijitali utakaojulikana kama “Mineral Sector Management Information System (MSMIS)”. Mfumo huu unalenga kuimarisha usimamizi, uratibu na upatikanaji wa taarifa za Sekta ya Madini kwa kutumia teknolojia za kidijitali, sambamba na jitihada za Serikali za kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma za umma. Mfumo huo utaunganishwa na mifumo mingine ya Serikali ili kuongeza ufanisi katika usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za madini na ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

 

 

 

  1. Usimamizi wa Mazingira na Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi
  1. Mheshimiwa Spika, Wizara itatekeleza Mpango Kazi wa Mazingira wa Sekta ya Madini 2025 – 2030 (Mineral Sector Environmental Action Plan – MSEAP) ambao unazingatia Mpango Kazi wa Taifa wa Usimamizi wa Mazingira (National Environmental Action Plan - NEAP) na DIRA 2050. Lengo kuu la Mpango huu ni kujumuisha kanuni za Mazingira, Jamii na Utawala Bora (Environmental, Social and Governance - ESG) katika upangaji, usimamizi na uangalizi wa udhibiti wa Sekta ya Madini nchini, ili kuhakikisha kuwa maendeleo ya rasilimali madini yanachangia ukuaji wa uchumi endelevu bila kuathiri usalama wa mazingira na ustawi wa jamii. Aidha, shughuli za usimamizi na utunzaji wa mazingira zitasimamiwa kwa kuzingatia Nguzo Na. 3 ya DIRA 2050, Sheria ya Madini Sura 123 na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191.

 

  1. Kazi Zitakazotekelezwa na Taasisi Zilizo Chini ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

 

  1. Tume ya Madini

 

  1. Utoaji na Ufuatiliaji wa Leseni za Madini
  1. Mheshimiwa Spika, Tume ya Madini itaendelea kutoa leseni kwa ajili ya shughuli mbalimbali za madini na kufuatilia uendelezaji wa leseni hizo. Tume ya Madini itaendelea kusimamia Sheria ya Madini, ikiwemo kusimamisha au kufuta leseni kwa wamiliki ambao watakiuka masharti ya kisheria. Aidha, Tume ya Madini itaendelea kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo.

 

  1. Kuimarisha Usimamizi wa Shughuli za Madini na Ukusanyaji wa Mapato ya Serikali
  1. Mheshimiwa Spika, Tume ya Madini itaendelea kuimarisha usimamizi ili kuhakikisha kwamba migodi mikubwa na ya kati ambayo imepewa leseni inaanza uzalishaji; kuimarisha usimamizi katika masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini nchini; kuendelea kudhibiti vitendo vya utoroshwaji wa madini nchini; kutanua wigo wa usimamizi wa uzalishaji wa madini ya ujenzi na madini ya viwandani; na kuendelea kufanya tafiti za kuibua vyanzo vipya vya mapato.

 

  1. Kuimarisha Ukaguzi wa Afya, Usalama, Mazingira na Uzalishaji wa Madini
  1. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kunakuwa na shughuli za uchimbaji madini endelevu, Tume ya Madini itaendelea kufanya kaguzi za usalama, afya na mazingira katika migodi midogo, ya kati na mikubwa. Aidha, kaguzi hizo zitahusisha mabwawa ya kuhifadhia topetaka (TSF), sehemu ya kuhifadhia miambataka (Waste Rock Dump - WRD) na maghala ya kuhifadhia baruti. Vilevile, Tume ya Madini itaendelea kusimamia uwasilishaji na utekelezaji wa mipango ya uendelezaji na ufungaji migodi. Serikali itaendelea kuchukua hatua stahiki kuhakikisha wachimbaji wanafuata taratibu za uchimbaji salama ili kuepuka ajali zisizo za lazima na ambazo zinaweza kuzuilika.

 

 

 

  1. Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (Local Content) na Wajibu wa Wamiliki wa Leseni za Madini kwa Jamii (CSR)
  1. Mheshimiwa Spika, katika kusimamia Ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini, Tume ya Madini itaendelea kutekeleza na kuhakikisha kuwa kampuni zinazomiliki leseni za madini zinanunua bidhaa na huduma zinazopatikana nchini. Aidha, Tume itaendelea kutangaza orodha ya huduma na bidhaa zinazotakiwa kutolewa na kampuni zinazomilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100. Vilevile, Tume itaendelea kusimamia wamiliki wa leseni za madini nchini kutimiza takwa la uwajibikaji kwa jamii (CSR). Ni marufuku kwa mtu ambaye si Mtanzania kusambaza bidhaa au kutoa huduma zilizotangazwa kufanywa na Watanzania kwa asilimia mia moja.

 

  1. Kuboresha Mazingira ya Utendaji Kazi na Kuwajengea Uwezo Watumishi
  1. Mheshimiwa Spika, Tume ya Madini imepanga kununua vitendea kazi na ujenzi wa majengo ya ofisi za Afisa Madini wakazi Mahenge, Rukwa na Songwe; Ukarabati wa majengo ya Ofisi za Afisa Madini Wakazi Morogoro, Mtwara na Mbeya; ununuzi wa vitendea kazi vikiwemo magari (25), kompyuta (300), pikipiki (100) na vifaa vya masoko ya madini ikijumuisha XRF 40 na mizani 20; ununuzi wa vifaa vya ukaguzi wa migodi na mazingira; pamoja na ujenzi wa mfumo wa Kanzidata ya Madini.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Ili kuhakikisha Tume ya Madini inatekeleza majukumu yake ipasavyo, itaendelea kuwajengea uwezo watumishi wake kwa kuwapatia mafunzo ya muda mrefu (70) na muda mfupi (170) katika kada mbalimbali kwa kuzingatia uhitaji uliopo.

 

  1. Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST)

 

  1. Kufanya Tafiti za Jiosayansi na Kuboresha Kanzidata ya Taifa ya Taarifa za Miamba na Madini 
  1. Mheshimiwa Spika, GST itafanya utafiti wa kina wa jiofizikia kwa njia ya kurusha ndege na ugani wa jiolojia na jiokemia katika QDS mbili (QDS 239 na 240) zilizopo Wilaya za Rufiji na Kilwa na kuchora ramani zake.

 

  1. Mheshimiwa Spika, GST itaendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa Mfumo wa Kanzidata ya Taifa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kukamilika kwa mfumo huo kutaongeza usalama wa taarifa za jiosayansi na utarahisisha uhifadhi na usambazaji wake kwa wadau.

 

  1. Mheshimiwa Spika, GST itakusanya, itahakiki na kutathmini uhalisia wa taarifa na takwimu za jiosayansi kutoka kwa wamiliki wa leseni 40 za utafutaji na uchimbaji madini nchini; kuhuisha Kanzidata ya Rasilimali Madini ya Taifa pamoja na Kitabu cha Madini Yapatikanayo Tanzania; kukusanya na kuchakata taarifa za miamba choronge mita 1,000 kutoka kwa wamiliki wa leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini.

 

 

  1. Kuwajengea Uwezo Wachimbaji Wadogo
  1. Mheshimiwa Spika, GST inalenga kufanya utafiti wa jiosayansi katika eneo litakalotengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo kwa kutumia vifaa vya kisasa ikiwemo ndege nyuki (drone) ili kupata taarifa za kina za jiofizikia kwa lengo la kubaini sehemu zenye viashiria vya uwepo wa madini katika eneo hilo. Aidha, GST itatoa mafunzo kuhusu kutambua ulalo, mwelekeo, tabia za mbale kwa uchenjuaji katika mikoa minne (4) ambayo ni Rukwa, Katavi, Kigoma na Kagera yenye shughuli hai za uchimbaji mdogo wa madini.

 

  1. Kuboresha Huduma za Maabara
  1. Mheshimiwa Spika, katika kuboresha huduma za maabara, GST itaendelea kufanya uchunguzi wa sampuli mbalimbali kwa kuzingatia vigezo vya ithibati (accreditation). Aidha, GST itaendelea na ujenzi wa maabara mpya ya kisasa ya uchunguzi wa madini (State of the Art Geoscientific Laboratory) katika eneo la Kizota Dodoma. Vilevile, GST itaendelea na ujenzi wa maabara za kanda katika mikoa ya kimadini ya Chunya na Geita ikiwa ni pamoja na ununuzi wa vifaa vyake kwa lengo la kusogeza karibu huduma kwa wananchi wanaojihusisha na shughuli za madini.

 

  1. Mheshimiwa Spika, GST itaendelea  kutengeneza vyungu vya kuyeyushia sampuli (crucibles and cupels) 250,000 kwa ajili ya kuwezesha uchunguzi wa sampuli za miamba na udongo hususani dhahabu. Aidha, GST itafanya uchunguzi wa sampuli 25,000 za udongo, miamba na madini na uandaaji wa sampuli rejea za ndani (internal certified reference materials) za dhahabu, shaba, fedha, zinki, chuma na cobalt.

 

  1.  Ufuatiliaji na Kuelimisha Umma Kuhusu Majanga ya Asili ya Jiolojia
  1. Mheshimiwa Spika, GST itakusanya na kuchakata taarifa kutoka vituo vinne (4) vya kudumu vya kunakili mienendo ya mitetemo vilivyopo katika mikoa ya Arusha, Dodoma, Geita na Mbeya. Aidha, ramani inayoonesha vitovu vya matetemeko ya ardhi nchini itahuishwa ikiwemo matengenezo kinga ya vifaa vya kunakili mitetemo. Vilevile, GST itaendelea kutoa elimu kwa umma kwa njia ya machapisho, semina na vyombo vya habari kuhusu namna bora ya kujikinga na kupunguza athari za majanga ya asili ya jiolojia.

 

  1. Kuwajengea Uwezo Watumishi wa GST katika Kutekeleza Majukumu
  1. Mheshimiwa Spika, GST itawajengea uwezo watumishi 30 kwa kuwapatia mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu katika fani mbalimbali ikiwemo masuala ya maabara.

 

  1. Mheshimiwa Spika, ili kuboresha mazingira ya utendaji kazi, GST itaendelea na taratibu za ununuzi wa vitendea kazi ikiwemo helikopta na ndege nyuki (drone) kwa lengo la kuongeza kasi ya kufanya utafiti wa kina wa madini nchini ikiwemo maeneo ya wachimbaji wadogo.

 

  1. Shirika la Madini la Taifa (STAMICO)
  1. Kuimarisha Ukusanyaji wa Mapato
  1. Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha mapato ya Shirika yanakua na kuimarika, Shirika limepanga kuongeza usimamizi kwenye uwekezaji uliopo katika miradi ya: uzalishaji wa Makaa ya Mawe na Nishati Safi ya Rafiki Briquettes; kuimarisha shughuli za uchorongaji; na uzalishaji wa kokoto – Chigongwe.

 

  1. Kuwezesha Shughuli za Uchimbaji Mdogo na Kuimarisha Vituo vya Mfano
  1. Mheshimiwa Spika, STAMICO itaendelea kuwezesha wachimbaji wadogo kwa kufanya yafuatayo: kuendelea kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa vituo vya mfano vya Itumbi, Lwamgasa na Katente pamoja na mitambo 15 ya uchorongaji; kuendelea na uzalishaji katika mgodi wa mfano Lwamgasa; kuanza uzalishaji katika kiwanda cha chumvi kilichopo Mkoa wa Lindi; kukamilisha upanuzi wa Kituo cha mfano cha Katente; na kusimika mitambo miwili (2) ya uchenjuaji yenye uwezo wa kuchakata tani 120 za mbale ya dhahabu kwa siku kwa kila mtambo katika eneo la wachimbaji wadogo la Mwakitolyo - Shinyanga na Buhemba - Mara.

 

  1. Kuendeleza Leseni za Madini za Shirika
  1. Mheshimiwa Spika, Shirika limepanga kuendelea na utafiti kwenye leseni moja (1) ya dhahabu iliyopo Wilaya ya Bukombe Mkoa wa Geita ambapo utafiti wake pamoja na taarifa ya upembuzi yakinifu utakamilika ifikapo Juni 2027. Vilevile, Shirika litaendelea na utafiti wa madini ya Kinywe katika leseni mbili (2) zilizopo Wilaya ya Ruangwa na Nachingwea, Mkoa wa Lindi pamoja na leseni tatu (3) za madini ya shaba zilizopo Katavi.

 

  1. Miradi ya Ubia na Kampuni Tanzu
  1. Mheshimiwa Spika, Shirika litaimarisha uendelezaji wa miradi ya ubia ambayo ni Mgodi wa Buckreef, Kiwanda cha Kusafisha Dhahabu Mwanza, Mgodi wa Uchimbaji wa Madini ya Nikeli wa Ntaka pamoja na Kampuni tanzu ya STAMIGOLD ili kuongeza ufanisi na kuwezesha ukusanyaji wa mapato kutoka kwenye miradi hiyo. Aidha, Shirika litaendelea kuiwezesha STAMIGOLD kufanya utafiti unaolenga kuongeza thamani ya matokeo ya utafiti wa awali pamoja na uhakiki wa uwepo wa mashapo katika leseni ya SML 157/2003 na PL 13075/2024 kwa lengo la kuongeza uhai wa mgodi huo.

 

  1. Kuendeleza Rasilimaliwatu na Kuboresha Mazingira ya Kufanyia Kazi
  1. Mheshimiwa Spika, Shirika linatarajia kujaza nafasi wazi 16 za watumishi kwa utaratibu wa uhamisho na ajira mpya. Aidha, watumishi 50 watapatiwa mafunzo ya muda mfupi na wanne (4) ya muda mrefu. Vilevile, Shirika litaendelea kusimamia na kuhakikisha maslahi na stahiki za watumishi zinapatikana kwa wakati. Kadhalika, Shirika litajenga jengo la Makao Makuu lenye ghorofa 10 jijini Dodoma.

 

  1. Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC)
  1. Utoaji Mafunzo ya Uongezaji Thamani Madini

 

  1. Mheshimiwa Spika, TGC itaendelea kutoa mafunzo katika programu tatu (3) kwa ngazi ya Stashahada katika teknolojia za madini ya vito na usonara; kutoa mafunzo ya muda mfupi katika fani za utambuzi wa madini ya vito, usonara, utengenezaji wa bidhaa za mapambo na urembo zinazotokana na miamba na vito na usanifu madini ya vito; na kufanya uhamasishaji kuhusu masuala ya uongezaji thamani madini ya vito katika shule za msingi na sekondari.

 

 

  1. Uzalishaji wa Bidhaa za Madini Zilizoongezwa Thamani

 

  1. Mheshimiwa Spika, TGC imepanga kuzalisha na kuuza bidhaa za usonara na ukataji wa madini ya vito 1300, bidhaa za usonara 1400, bidhaa za miamba 7200, bidhaa za urembo 7500. Bidhaa hizo zinatarajiwa kuwa na thamani ya shilingi milioni 135.

 

  1. Huduma za Upimaji wa Sampuli za Madini ya Vito

 

  1. Mheshimiwa Spika, Ili kuongeza ufanisi wa huduma za maabara TGC imepanga kuimarisha ufanisi wa maabara ambapo itaboresha huduma za upimaji wa madini ya vito hadi kufikia uwezo wa kupima sampuli 1200 kwa mwaka.

 

  1. Utafiti wa Madini ya Vito na Metali

 

  1. Mheshimiwa Spika, TGC kwa kushirikiana na Taasisi ya Jemolojia ya Nchini Thailand (GIT) imepanga kufanya utafiti wa ubora na viwango vya madini ya Tanzanite. Tafiti hizi zitaongeza ubunifu na tija katika shughuli mbalimbali za uongezaji thamani kwa madini ya vito na metali.

 

  1. Kuwajengea Uwezo Watumishi na Kuboresha Mazingira ya Kazi

 

  1. Mheshimiwa Spika, TGC itawawezesha watumishi saba (7) kuhudhuria mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi ndani na nje ya nchi. Lengo ni kuendelea kuwajengea uwezo katika maeneo yao ya utekelezaji wa majukumu. Aidha, TGC imepanga kununua mashine na vifaa mbalimbali kwa ajili ya karakana za mafunzo na uchakataji madini pamoja na ununuzi wa gari.
  2. Mheshimiwa Spika, TGC itaendelea na usimamizi wa ujenzi wa Jengo la ghorofa 8 (Twin Tower Building). Jengo hili litakuwa na miundombinu mbalimbali ikiwemo madarasa, karakana za uongezaji thamani madini, maabara ya kisasa ya madini ya vito na bidhaa za usonara, mineral gallery, ofisi, mabweni kwa ajili ya wanafunzi, kantini na maduka.

 

  1. Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI)

 

  1. Kuandaa na Kuweka Wazi Taarifa ya 17 ya TEITI ya Mwaka wa Fedha 2024/2025

 

  1. Mheshimiwa Spika, TEITI itaandaa na kuweka wazi taarifa ya 17 ya Mwaka wa Fedha 2024/2025 ya ulinganishi wa malipo ya kodi na tozo kutoka kampuni za madini, mafuta na gesi asilia na mapato yaliyopokelewa na Serikali. Uandaaji wa taarifa hiyo ni utekelezaji wa vigezo vya uwazi na uwajibikaji vya mwaka 2023 ambapo nchi wanachama wa EITI hutakiwa kuandaa na kuweka wazi taarifa husika kila mwaka.

 

  1. Kuweka Wazi Mikataba ya Kampuni za Madini, Mafuta na Gesi Asilia

 

  1. Mheshimiwa Spika, TEITI itaendelea kuweka wazi mikataba ambayo Serikali imeingia na Kampuni za Madini, Mafuta na Gesi Asilia hapa nchini ikiwa ni utekelezaji wa Sheria inayosimamia majukumu ya TEITI pamoja na utekelezaji wa Matakwa ya Kimataifa ya EITI.

 

 

  1. Kuweka Wazi Orodha ya Wamiliki wa Hisa katika Kampuni za Madini, Mafuta na Gesi Asilia

 

  1. Mheshimiwa Spika, TEITI itaendelea kuweka wazi majina ya wamiliki wa hisa katika kampuni za madini, mafuta na gesi asilia (Beneficial ownership disclosure) kupitia ripoti zake za kila mwaka.

 

  1. Kutoa Elimu kwa Umma Kuhusu Matumizi ya Takwimu Zinazotolewa Kwenye Ripoti za TEITI
  1. Mheshimiwa Spika, TEITI itaendelea kutoa elimu kwa umma kwa kuwafikia wadau ikiwa ni pamoja na kushiriki katika maonesho mbalimbali ndani na nje ya nchi, kufanya warsha katika maeneo ambapo shughuli za uchimbaji wa rasilimali madini, mafuta na gesi asilia zinatekelezwa, na kufanya vipindi vya redio na runinga ili kutangaza majukumu ya taasisi na kuhamasisha matumizi ya takwimu zinazotolewa.

 

  1. Kuwajengea Uwezo Watumishi

 

  1. Mheshimiwa Spika, Ili kuhakikisha TEITI inatekeleza majukumu yake ipasavyo, itaendelea kuwajengea uwezo watumishi wake kwa kuwapatia mafunzo ya muda mrefu watumishi wanne (4) na muda mfupi 12 katika kada mbalimbali kwa kuzingatia uhitaji uliopo.

 

  1. Kufanya Tafiti za Namna Wananchi Wanavyonufaika na Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia

 

  1. Mheshimiwa Spika, TEITI itaendelea kufanya utafiti kuhusu utekelezaji wa sheria  katika eneo la Ushirikishwaji wa Watanzania (Local Content) katika Sekta ya Uziduaji na Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (Corporate Social Responsibility - CSR) katika Sekta ya Madini, Mafuta na Gesi Asilia. Aidha, TEITI itaendelea kufanya tafiti katika Sekta ya Uziduaji  ili kuishauri Serikali namna bora ya kuboresha usimamizi wa Sekta ya Uziduaji.

 

  1. Utekelezaji wa Vigezo vya EITI  Nchini

 

  1. Mheshimiwa Spika, mwaka 2023 Tanzania ilifanyiwa tathmini ya utekelezaji wa vigezo vya EITI ambapo ilipata hadhi ya daraja la moderate kwa kiwango cha asilimia 77.  Taasisi hii ya EITI ndio taasisi yenye jukumu la Kimataifa la kufanya tathmini ya utekelezaji wa shughuli za Uziduaji kwa nchi wanachama ikiwemo Tanzania. Taasisi hiyo imepanga kufanya tathmini ya nne (4) kwa TEITI Mwezi Januari, 2027. Aidha, tathmini hiyo itapima utekelezaji wa vigezo vya EITI. Ili kukamilisha tathmini hiyo, TEITI itafanya maandalizi husika.

 

  1. SHUKRANI

 

  1. Mheshimiwa Spika, natambua wazi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea na juhudi kubwa za kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi yetu unaimarika. Kasi, juhudi na ubunifu mkubwa wa utendaji kazi anaoendelea nao Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vinachochea kukua kwa maendeleo ya nchi yetu.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kipekee nitumie fursa hii kumshukuru tena kwa dhati Mheshimiwa Rais kwa miongozo na maelekezo anayotupatia katika Sekta ya Madini ambayo yanaifanya sekta hii kuendelea kukua kwa kasi na kuvutia wawekezaji kwa manufaa ya Taifa.

 

  1. Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii pia kumshukuru Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa maelekezo na miongozo ambayo amekuwa akiitoa kwa Sekta ya Madini ili kuimarisha usimamizi na utendaji wa shughuli mbalimbali za sekta kwa manufaa ya Taifa.

 

  1. Mheshimiwa Spika, napenda pia nimshukuru Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa usimamizi wake makini wa shughuli za kila siku za Serikali.

 

  1. Mheshimiwa Spika, niwashukuru wadau wa Sekta ya Madini wakiwemo Chemba ya Migodi, FEMATA, TAWOMA, TAMIDA, CHAMMATA, WIMA, TWIMI, TAMISA na vyama vingine vya wachimbaji madini, watafutaji, wachimbaji, wamiliki wa mitambo ya uchenjuaji, uyeyushaji na usafishaji madini, wafanyabiashara wa madini na watoa huduma kwa kuendelea kutekeleza shughuli zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi. Hii imerahisisha usimamizi wa Sekta ya Madini.

 

  1. Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila endapo sitazishukuru taasisi za fedha hususan mabenki kwa kuendelea kuwapa mikopo wadau wa Sekta ya Madini wakiwemo wachimbaji wakubwa, wa kati na wadogo. Vilevile, nivishukuru Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kutuhakikishia usalama na kushirikiana nasi katika kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa madini kwenye maeneo yenye shughuli za madini bila kusahau vyombo vya habari kwa ushirikiano wanaotupatia katika kuitangaza Sekta ya Madini.

 

  1. Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka  migodi na watanzania wote kwa ujumla kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji katika maeneo yao. Hakika wamekuwa sehemu ya mafanikio ya Sekta ya Madini nchini.

 

 

  1. HITIMISHO
  1. Mheshimiwa Spika, ili Wizara iweze kutekeleza majukumu na malengo yaliyopangwa ikiwemo ukusanyaji wa maduhuli ya shilingi 1,406,006,031,000.00 naomba Bunge lako Tukufu liridhie na kupitisha makadirio ya shilingi 174,983,580,000.00 kwa ajili ya matumizi ya Wizara na Taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 kwa mchanganuo ufuatao:
  1. shilingi 71,507,708,000.00 sawa na asilimia 40.87 ya bajeti yote ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
  2. shilingi 103,475,872,000.00 sawa na asilimia 59.13 ya bajeti yote ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Kati ya fedha hizo, shilingi 27,365,095,000.00 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi (PE) na shilingi 76,110,777,000.00 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC) ya Wizara na Taasisi zake.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza. Majedwali na vielelezo mbalimbali kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa masuala na takwimu muhimu kuhusu Sekta ya Madini vimeambatishwa pamoja na hotuba hii.  Hotuba hii inapatikana katika tovuti ya Wizara ya Madini kwa kikoa cha https://www.madini.go.tz.
  2. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals