[Latest Updates]: Wachimbaji madini watakiwa kuwa na Mpango wa Ufungaji Mgodi

Tarehe : Feb. 21, 2019, 1:47 p.m.
left

Na Greyson Mwase, Pwani

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amewataka wachimbaji wa madini  ya ujenzi  aina ya kokoto katika mkoa wa Pwani kuwa na Mpango wa Ufungaji Mgodi utakaotumika kama mwongozo wa kuhakikisha mazingira yanaachwa yakiwa katika hali salama mara baada ya kumalizika kwa shughuli za uchimbaji wa madini hayo.

Profesa Kikula aliyasema hayo leo tarehe 21 Februari, 2019 katika nyakati tofauti alipofanya ziara yake katika migodi  inayojishughulisha na shughuli za uchimbaji wa madini ujenzi aina ya kokoto iliyopo katika Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani yenye lengo la kutembelea wachimbaji wa madini hayo pamoja na kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.

Profesa Kikula katika ziara hiyo akiwa ameambatana na Kamishna - Tume ya Madini, Dkt. Athanas Macheyeki, wataalam kutoka Makao Makuu ya Tume ya Madini jijini Dodoma, Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ofisi ya Afisa Migodi Mkazi wa Lugoba pamoja na waandishi wa habari, Profesa Kikula alitembelea migodi ya Sisti Mganga, Gulf Concrete Company Limited na  Yaate Company Limited iliyopo katika Wilaya ya Bagamoyo.

Akizungumza katika nyakati tofauti mara baada ya kutembelea migodi hiyo, Profesa Kikula aliwataka wamiliki wa migodi kuhakikisha wanakuwa na mipango ya ufungaji migodi mapema badala ya kusubiri mpaka shughuli za uchimbaji madini zinapomalizika hivyo kufanya zoezi la ufungaji wa migodi kuwa gumu huku wakiacha mazingira yakiwa hatarishi.

“Ninapenda kuwakumbusha kuwa suala la kuwa na Mpango wa Ufungaji wa Migodi ni la lazima kulingana na Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake, hivyo ninawataka kuhakikisha mnakuwa na mpango ili kuhakikisha mashimo hayaachwi wazi,” alisema Profesa Kikula.

Awali akiwa katika mgodi unaomilikiwa na Sisti Mganga Profesa Kikula  alielezwa mafanikio ya mgodi huo ikiwa ni pamoja na  kokoto za mgodi huo kutumika katika ujenzi wa daraja la Mto Wami uliopo mkoani Pwani,  reli ya kisasa ya standard gauge na utengenezaji wa marumaru kwa ajili ya soko la ndani ya nchi.

Katika hatua nyingine Mganga alitaja changamoto zinazoukumba mgodi huo kuwa ni pamoja na tozo kubwa kutoka katika halmashauri na tozo nyingine zinazotozwa na kijiji cha Kihangaiko  pasipo kuwa na risiti pamoja na ukosefu wa vifaa vya kisasa.

Profesa Kikula alisema kuwa, suala la tozo litafanyiwa kazi kwa kuliwasilisha mamlaka za juu kwa ajili ya kufanyiwa kazi na kusisitiza kuwa nia ya Serikali kupitia Tume ya Madini, ni kuhakikisha wachimbaji wa madini hususan wadogo wanafanya kazi katika mazingira mazuri yenye faida kubwa huku wakilipa kodi mbalimbali Serikalini pasipo vikwazo vyovyote.

Wakati huo huo, akiwa katika mgodi wa uzalishaji wa kokoto wa Gulf  Concrete Limited Profesa Kikula alitoa mwezi mmoja kwa uongozi wa mgodi huo kuhakikisha wanarekebisha kasoro ya mazingira kwa kuhakikisha vumbi linalotoka wakati wa shughuli za uchimbaji wa kokoto halisambai kwani linaathiri wananchi  wa vijiji vya jirani katika mgodi huo.

Alisema ni vyema wakazingatia Sheria ya Mazingira kwani vumbi mbali na kuathiri wananchi wanaoishi katika vijiji vya jirani linaweza kuathiri wafanyakazi wa mgodi huo.

Aidha, alituaka mgodi huo kuendelea kuhakikisha unatoa huduma kwa jamii inayozunguka mgodi huo na kutumia huduma za ndani ya nchi kama vile bidhaa pamoja na ajira kwa wazawa.

Katika hatua nyingine, Profesa Kikula akiwa katika mgodi wa kuzalisha kokoto wa Yaate Co. Limited, mbali na kuupongeza mgodi kwa kuaminiwa na kupewa kazi ya kusambaza kokoto kwenye mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya standard gauge unaotelekezwa na kampuni ya Yapi  Merkezi na kutoa huduma mbalimbali kwa jamii inayouzunguka mgodi huo pamoja na ajira, aliutaka mgodi huo kuendelea kununua bidhaa/huduma kutoka kwa wananchi.

“Kutoa huduma bora kwa wananchi wanaozunguka mgodi kunaboresha mahusiano na kupunguza migogoro ya mara kwa mara inayoweza kujitokeza.

Awali akielezea mafanikio ya mgodi, Mkurugenzi Mtendaji wa Yaate Co. Limited, Eugen Mikongoti alisema  mradi umenufaisha watanzania wengi kwa kuchangia maendeleo ikiwa ni pamoja na ulipaji  wa zaidi ya shilingi bilioni 1.31 ambazo zimelipwa kama ushuru wa madini  kati ya kipindi cha mwezi Juni, 2018 hadi Januari, 2019 na shilingi milioni 338.8 zilizolipwa kama mrabaha.

Alieleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja na utoaji wa fursa za ajira kwa watanzania hususan vijana wanaozunguka mgodi na kuziwezesha kampuni zinazomilikiwa na wazawa kushiriki katika miradi mikubwa  hivyo kuzijengea uwezo wa kitaalam na kupata fursa.

Mikongoti alitaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kuwezesha maendeleo ya wanachi wanoishi karibu na mgodi kupitia huduma za jamii ambapo mpaka  sasa mgodi huo  unaendelea na ujenzi wa nyumba za watumishi na kuhudumia wananchi katika zahanati iliyopo mgodini.

Katika hatua nyingine Mikongoti alipongeza kazi kubwa zinazofanywa na Tume ya Madini chini ya Mwenyekiti wake Profesa Kikula ikiwa ni pamoja na kuwatembelea, kuwapa elimu na kutatua changamoto mbalimbali.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals