[Latest Updates]: Wachimbaji Madini Songwe waruhusiwa kuendelea na shughuli za uchimbaji madini

Tarehe : Oct. 18, 2018, 8:20 a.m.
left

Na Greyson Mwase, Songwe

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amewataka wachimbaji wa madini  wanaoendesha shughuli zao za uchimbaji wa madini ya chokaa na ujenzi katika  kijiji cha Nanyala kilichopo katika Wilaya ya Mbozi iliyopo mkoani Songwe kuendelea na shughuli zao wakati wakisubiri  suluhu ya  mgogoro baina yao na kiwanda cha saruji cha Mbeya.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia mbele) na Meneja wa Kiwanda cha chokaa cha Lime Africa kilichopo katika Kata ya Nanyala Wilayani Mbozi Mkoani Songwe, Fredy Msindo (kushoto mbele) pamoja na msafara wakiendelea na ziara katika eneo la kiwanda hicho ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili katika mkoa wa Songwe yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini tarehe 17 Oktoba, 2018.[/caption]

Naibu Waziri Nyongo aliyasema hayo leo tarehe 17 Oktoba, 2018 alipokuwa akizungumza katika mkutano na wachimbaji wadogo  uliofanyika katika kata ya Nanyala wilayani Mbozi mkoani Songwe ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili katika  mkoa huo  yenye lengo la  kukagua shughuli za uchimbaji wa madini,  kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.

Katika ziara yake Nyongo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Songwe, John Palingo, Afisa Madini Mkazi katika Mkoa wa Mbeya, Sabai Nyansiri, Afisa Madini anayesimamia wilaya za Songwe na Chunya, Athuman Kwariko, Afisa Madini kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mbeya, Ndege Bilagi, vyombo vya ulinzi na usalama vya wilaya pamoja na waandishi wa habari.

Nyongo alifafanua kuwa, awali maelekezo yalitolewa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ya kutaka viongozi kutoka katika mikoa ya Mbeya na Songwe kukaa pamoja na kuhakikisha wanamaliza mgogoro wa ardhi kati ya  wakazi wa Songwe na Mbeya na kiwanda cha kuzalisha saruji nje ya mahakama jambo ambalo linafanyiwa kazi kwa sasa.

Alielekeza viongozi kutoka katika mikoa husika kuhakikisha wanashughulikia mgogoro wa ardhi kati ya mikoa miwili na kiwanda cha saruji cha Mbeya kwa wakati huku wananchi wanaojishughulisha na shughuli za uchimbaji madini wakiendelea na shughuli zao kama kawaida katika maeneo husika.

Aliendelea kusema kuwa, jukumu kuu la Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini ni kuhakikisha wanatoa leseni za uchimbaji wa madini kwa kuzingatia sheria na kanuni za madini na kusisitiza kuwa leseni ya uchimbaji wa madini ni tofauti na  hati ya ardhi kwa kuwa inahusisha madini yaliyopo chini ya ardhi.

“Ningependa ieleweke kuwa, leseni ya madini inampa mtu kibali cha kuchimba madini yaliyopo chini ya ardhi ambayo ni tofauti na hati ya ardhi, hivyo wachimbaji wa madini wana haki ya kuendelea na shughuli za uchimbaji wa madini wakati suala la mgogoro wa ardhi likiendelea kushughulikiwa na mamlaka husika,” alisisitiza Nyongo.

Akielezea taratibu za kuchimba madini mara baada ya kupata leseni, Naibu Waziri Nyongo alisema mara baada ya mchimbaji kupata leseni ya uchimbaji wa madini anatakiwa kufika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na baadaye kutambulishwa katika Ofisi ya Kijiji ili kukutanishwa na wananchi na kufanya makubaliano ya ulipaji fidia kabla ya kuanza shughuli rasmi za uchimbaji wa madini.

Alisisitiza kuwa, ni lazima wawekezaji wote katika shughuli za uchimbaji wa madini kuhakikisha kuwa wanajitambulisha na kufanya makubaliano na wananchi kabla ya kuanza rasmi kwa uchimbaji wa madini ili kuepuka migogoro ya mara kwa mara.

Diwani wa Viti Maalum kutoka Tarafa ya Iyula iliyopo Wilayani Mbozi mkoani Songwe, Messiah Swella akiwasilisha kero yake kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) katika mkutano huo.[/caption]

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Nyongo aliwataka maafisa madini katika mikoa ya Mbeya na Songwe kuendelea na zoezi la kuainisha maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini ikiwa ni pamoja na utoaji wa leseni ili uchimbaji wao uweze kuleta tija kwenye uchumi wa nchi.

Aidha, aliongeza kuwa katika maeneo ambayo ni ya hifadhi au vivutio vya utalii leseni zake zifutwe ili kuhakikisha rasilimali za maliasili zinalindwa na kuongeza pato kwenye uchumi wa taifa.

Wakati huohuo Nyongo aliwataka wachimbaji wa madini kuhakikisha kuwa wanalipa kodi mbalimbali  ili fedha hizo ziweze kutumika katika  uboreshaji wa huduma nyingine za jamii kama vile elimu, afya, miundombunu ya barabara.

Pia, Nyongo aliwataka wachimbaji wa madini kuorodhesha kodi na tozo mbalimbali ambazo wanaona ni nyingi na kuziwasilisha katika Wizara ya Madini, ili Wizara iangalie namna ya kuzipunguza na wapate faida zaidi kwenye uchimbaji wa madini.

Awali wakizungumza katika nyakati tofauti wachimbaji hao walieleza changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na mgogoro wa ardhi baina yao na  kiwanda cha saruji cha Mbeya, uharibifu wa mazingira unaofanywa na baadhi  ya wachimbaji na ukosefu wa maeneo kwa ajili ya uchimbaji wa madini.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals