[Latest Updates]: Naibu Waziri Nyongo aagiza maafisa madini kuwasilisha kwake tafsiri sahihi ya mawe yanayokatwa kabla ya kutoa maamuzi ya usafirishwaji wake nje ya nchi

Tarehe : Oct. 8, 2018, 8:02 a.m.
left

Na Greyson Mwase, Dodoma

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amewataka maafisa madini nchini kuwasilisha kwake haraka maana halisi ya mawe yanayochimbwa na kukatwa kama ni madini ghafi au ni mali ghafi  kabla ya  kutoa maamuzi juu ya usafirishwaji wake nje ya nchi.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati mbele) akiendelea na ziara katika machimbo ya mawe yaliyopo katika eneo Itiso Wilayani Chamwino mkoani Dodoma.[/caption]

Aliyasema hayo jana tarehe 06 Oktoba, 2018 mara baada ya kukamilisha ziara yake katika Mgodi wa Mawe unaomilikiwa na Sisti Mganga uliopo katika eneo la Itiso mkoani Dodoma ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku moja katika Wilaya ya Chamwino yenye lengo la  kukagua shughuli za uchimbaji wa madini,  kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini pamoja na wananchi wanaozunguka migodi.

Katika ziara yake Nyongo aliambatana na Mkuu wa Wilaya  ya Chamwino, Vumilia Nyamoga, Mbunge wa Jimbo la  Chinolwa, Joel Makanyaga, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Joshua Nduche, vyombo vya  ulinzi na usalama vya Wilaya pamoja na waandishi wa habari.

Alifafanua kuwa Sheria Mpya ya Madini ilitoa zuio la usafirishwaji wa madini ghafi nje ya nchi ili kuzuia mianya ya utoroshwaji wa madini nje ya nchi.

“Kabla ya Sheria hii mpya ya Madini, kulikuwa na utoroshwaji mkubwa wa madini nje ya nchi hali ambayo iliikosesha  Serikali mapato yake, lakini mara baada ya utekelezaji wa Sheria Mpya ya Madini tumeshuhudia ongezeko kubwa la mapato kutokana na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini,” alisema Nyongo.

Naibu Waziri Nyongo aliendelea kusema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa mbali na wachimbaji wa madini hususan  wachimbaji wadogo kufanya shughuli zao katika mazingira mazuri, Serikali inataka kupata mapato stahiki kwa ajili ya uboreshaji wa sekta nyingine muhimu.

Alisema mara baada ya kupokea changamoto ya kuzuiwa kwa usafirishwaji wa mawe yaliyochimbwa na kukatwa na Mgodi wa Mawe unaomilikiwa na Sisti Mganga, aliridhishwa na juhudi zinazofanywa na mgodi huo na kusema kama Serikali inaangalia namna ya kumsaidia mmiliki wa mgodi huo lakini baada ya kujiridhisha kama ni malighafi badala ya madinighafi.

Mmiliki wa Mgodi wa Mawe uliopo katika eneo la Itiso Wilayani Chamwino mkoani Dodoma, Sisti Mganga kushoto akielezea shughuli zinazofanywa na mgodi huo kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa pili kutoka kushoto mbele)[/caption]

“Lazima tuhakikishe Sheria inasimamiwa ipasavyo, iwapo itabainika kuwa mawe yanayochimbwa na kukatwa ni malighafi basi tutatoa uamuzi wa kuyaruhusu kusafirishwa nje ya nchi na Serikali kupata mapato yake,” alisisitiza Naibu Waziri Nyongo.

Katika hatua nyingine akizungumza katika nyakati tofauti katika ziara hiyo, Nyongo aliwataka wachimbaji wadogo nchini wasio rasmi kuunda vikundi na kuomba leseni za uchimbaji madini ili waweze kuchimba kwa kufuata sheria  na kanuni za madini.

Aliendelea kusema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini imetenga maeneo maalum yaliyofanyiwa utafiti kwa ajili ya kugawiwa kwa wachimbaji wadogo.

Aidha, aliwataka wamiliki wote wa leseni kuendeleza maeneo yao kama Sheria ya Madini inavyowataka  na kusisitiza watakaoshindwa kuendeleza maeneo yao leseni zao zitafutwa na maeneo yao kugawanywa kwa ajili ya wachimbaji wadogo.

Naye Mbunge wa Chilonwa kupitia Chama cha Mapinduzi, Joel Makanyaga akizungumza katika ziara hiyo alimshukuru Naibu Waziri Nyongo kwa kutembelea machimbo hayo na kufafanua kuwa iwapo wachimbaji hao watawezeshwa na Serikali bidhaa za ujenzi zinazotokana na mawe zitaongezeka na kusaidia hususan katika ujenzi wa jiji jipya la Dodoma.

Alisema kuwa mahitaji ya vifaa vya ujenzi ni makubwa katika ujenzi wa jiji la Dodoma na kuendelea kusema kuwa mapato yatokanayo na uchimbaji na ukataji wa mawe yanatarajiwa kuongezeka hivi karibuni.

Awali akiwasilisha changamoto za Mgodi wa Mawe Mkurugenzi wa Mgodi huo, Sisti Mganga alisema kuwa uwepo wa  Sheria ya Madini inayokataza usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi umeathiri utendaji kazi wa kampuni kwani wamerundika mawe mengi wakisubiri maelekezo kutoka Serikalini.

Alisisitiza kuwa mawe yanayochimbwa kukatwa na kung’arishwa katika  machimbo hayo yanajulikana kama malighafi kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na barabara na kuiomba Serikali kuruhusu usafirishwaji wa mawe hayo ili waweze kuendesha shughuli za uchimbaji na ukataji wa mawe hayo na kulipa mrabaha na kodi mbalimbali Serikalini.

Aidha Mganga aliiomba Serikali kupitia Wizara ya Madini kuendelea kuhamasisha uwekezaji katika ujenzi wa viwanda kwa ajili ya kuchenjua na kuongeza thamani madini ili kuzalisha ajira na kukuza uchumi wa nchi.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals