[Latest Updates]: Waziri Mkuu Majaliwa ataka kanuni za uanzishwaji masoko ya madini kukamilishwa haraka

Tarehe : Jan. 28, 2019, 11 a.m.
left

  • Aitaka Wizara ya Madini kutoa Mwongozo wa Usafirishaji Madini Nje.
  • Waziri Biteko asema, Rasimu ya Kwanza imekamilika,
  • Asisitiza Masoko yaanze mwezi Februari

 Asteria Muhozya na Samwel Mtuwa, Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Madini kuharakisha ukamilishaji wa Kanuni za Uanzishwaji Masoko ya Madini nchini, ikiwemo kuhakikisha masoko hayo yaanza haraka.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo Januari 26, wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha Mawaziri kutoka wizara mbalimbali, Wakuu wa Mikoa yote nchini, Wizara ya madini, Makatibu Tawala wa Mikoa, Taasisi mbalimbali zikiwemo Tume ya Madini, Benki Kuu ya Tanzania na Kituo cha Uwekezaji Nchini, (TIC).

Amesema kikao hicho ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli aliyayotoa Januari 22 wakati akifungua Mkutano wa Kisekta uliowashirikisha wachimbaji na wadau wa madini nchini ambapo Rais Magufuli alisisitiza juu ya kuanzishwa kwa masoko ya madini.

Aidha, ameipongeza Wizara ya Madini kwa kikao hicho na kusema kwamba, kimelenga katika kujenga uelewa wa pamoja kwa Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Maafisa Madini wa Mikoa kuhusu kanuni na namna ya kuendesha Masoko hayo.

Akisisitiza kuhusu usimamizi wa masoko ya madini, Waziri Mkuu amesema kuwa, Wakuu wa Mikoa kwa kushirikiana na Maafisa Madini ndiyo watakuwa wasimamizi wakuu wa masoko hayo  na kuongeza kuwa, katika ngazi ya Wilaya, masoko hayo yatasimamiwa na wakuu wa wilaya na kueleza “kwenye wilaya msimamizi ni mkuu wa wilaya, wakuu wa wilaya mkaripoti kwa wakuu wa mikoa wawasaidie,”.

Pia, ametaka pindi kanuni hizo zitakapokamilika kuzifikisha kwa Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa na Halmashauri za Wilaya na  katika maeneo yote yenye machimbo wakiwemo wachimbaji na Wafanyabiashara ikilenga kuwezesha wadau hao kufikiwa na kanuni hizo na kuwa na uelewa wa kutosha na hatimaye ziweze kusimamiwa kikamilifu kwa kushirikiana  na Tume ya Madini.

Katika kuhakikisha kwamba masoko hayo yanaendeshwa  kwa usalama, ameitaka mikoa kuhakikisha kunakuwa na na hali ya ulinzi na usalama kwenye maeneo hayo ili  kuwahakikishia wafanyabiashara, wachimbaji na wananchi kwa ujumla usalama wa kutosha wakati wa kuuza madini hayo katika masoko yatakayoanzishwa.

Akizungumzia mwongozo wa usafirishaji madini nje ya nchi, ameitaka  wizara  ya madini kutoa mwongozo huo mapema na kueleza kuwa, baada ya serikali kutafakati kwa kina, imetoa mwongozo wa kusafirisha baadhi ya madini nje ya nchi na hivyo kuitaka wizara kutoa mwongozo huo kwa Wakuu wa Mikoa yote nchini.

 Kwa upande wake, Waziri wa Madini Doto Biteko amesema kuwa, tayari rasimu ya kwanza ya Kanuni hizo imekamilika na kueleza kuwa, kikao kazi kinalenga jambo ambalo halikuwahi kufanyika tangu nchi ya Tanzania ipate uhuru na hivyo kuwataka wakuu wa mikoa kulifanya kuwa jambo linalowahusu wote.

Amesema kwa sasa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini hawana maeneo maalum wanayoweza kufanyia biashara  ya madini  hali ambayo inachangia kuwepo utoroshaji wa madini na hivyo kuikosesha serikali mapato.

Ameongeza, ili  kukabiliana na changamoto ya masoko ya madini, Wizara iliunda kamati iliyojumuisha wajumbe kutoka katika taasisi mbalimbali za serikali zikiwemo Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Madini, Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara, Benki  Kuu na Tume ya Madini.

Amesema kuwa, Kamati hiyo iliundwa ili kuandaa rasimu ya Kanuni za kuanzisha na kusimamia Masoko ya Madini Nchini na kuongeza kuwa katika kuandaa kanuni hizo, jina la Kanuni linalondekezwa The Mining (Mineral and Gem House) Regulations, 2019," amesema Waziri Biteko.

Ameongeza kuwa, Marekebisho ya sheria yaliyofanyika mwaka 2017 katika sheria ya Madini ya Mwaka 2010 yalilenga kulinda maslahi ya taifa na kuhakikisha sekta ya madini inachangia ipasavyo katika kukuza na kuimarisha mchango wa sekta katika pato la Taifa na kuongeza kwamba, si kweli kwamba marekebisho hayo yamefukuza wawekezaji bali yameongeza idadi ya wanaotaka kuwekeza katika sekta ya madini.

Katika hatua nyingine, Waziri Biteko amewataka Wakuu wa Mikoa kuhakikisha masoko ya madini yanaanza mara moja wakati kanuni hizo zinaendelea kuboreshwa na kusisitiza wakuu hao wahakikishe yaanza ifikapo mwezi Februari mwaka huu.

“Lazima Wakuu wa Mikoa tuanze. Wakuu wa Mikoa tutaanza na Kanuni hizi, hizi. Tutaendelea kuziboresha lakini lazima tuanze. Na kanuni hizi zikipita, lazima kila anayehusika atafanya biashara kupitia kanuni hizi,” amesisitiza Waziri Biteko.

Halikadhalika, amewataka washiriki wa kikao hicho kuhakikisha wanazipitia kanuni hizo kwa lengo la kufanya maboresho na kutoa mapendekezo yatakayowezesha kuwa na kanuni zitakazowezesha taifa kunufaika na rasilimali hiyo na kuongeza, “ hizi kanuni zikiwa mbovu itakuwa yetu wote,”.

Pia, amewaomba Wakuu wa Mikoa, Maafisa Tawala wa Mikoa, Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa na Wadau kwa ujumla kufanya kazi kwa pamoja ili kuweza kutimiza ndoto za muda mrefu za Wachimbaji wadogo Wafanyabiashara wa Madini, Wadau na Watanzania wote kwa ujumla za kuhakikisha kwamba sekta ya madini inachangia zaidi katika taifa na inalinufaisha.

Naye, Waziri , Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman Jafo amesema kuwa, Waziri Biteko ameanza vizuri na  kueleza kuwa,  kikao hicho kitasaidia kupata mambo mbalimbali yatakayosaidia katika uanzishwaji wa masoko hayo na kueleza kuwa, timu yake ya mikoa iko tayari.

“Mhe. Waziri nimefurahi sana namna wakuu wa mikoa walivyozungumza wakati wa majadiliano ya kuboresha Kanuni hizi. Tunakwenda kuona namna ya kuanzisha masoko haya,”.

Aidha, amewataka wakuu wa mikoa kulichukulia jambo hilo kama matarajio ya Rais Magufuli anavyotaka kuona kwamba madini yanalinufaisha taifa.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals