Tarehe : June 27, 2025, 2:22 p.m.
Wachimbaji Wadogo Dodoma Wapatiwa Mafunzo ya Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira Migodini
Mafunzo yanalenga kukuza uchimbaji salama, endelevu na wenye tija katika sekta ya madini ya shaba
Dodoma, Juni 27 2025
Zaidi ya wachimbaji wadogo kutoka migodi ya shaba iliyopo katika mkoa wa Dodoma wamepatiwa mafunzo maalum kuhusu usalama mahali pa kazi, afya, utunzaji wa mazingira na usimamizi wa shughuli za uchimbaji. Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha uchimbaji salama na endelevu nchini.
Mafunzo hayo yamewahusisha wachimbaji kutoka Mgodi wa Shengde uliopo Nala, Mgodi wa Hussein Pilly uliopo Tambi (Wilaya ya Mpwapwa) na Mgodi wa Canada uliopo Chamkoroma (Wilaya ya Kongwa) ambapo yamewezeshwa na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kushirikiana na Tume ya Madini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhandisi Chacha Megewa kutoka Tume ya Madini ameeleza kuwa ni muhimu kwa wachimbaji kufanya kazi katika mazingira salama kwa kutumia vifaa kinga kama kofia ngumu, reflekta, buti, gloves na barakoa (maski).
"Ulipuaji wa baruti ni mojawapo ya shughuli hatarishi migodini. Hii ni kazi ya kitaalam na lazima ifanywe na mtu mwenye cheti maalum. Ni muhimu kuhakikisha vilipuzi vyote vimelipuka kikamilifu kabla ya kuruhusu watu kuingia mgodini tena," amesisitiza Mhandisi Megewa.
Kwa upande wake, Mkaguzi wa Migodi kutoka Tume ya Madini, Bw. Fahad Mkuu, amekumbusha kuwa usalama ni jukumu la pamoja na si la mtu mmoja. Amesisitiza umuhimu wa wachimbaji kujenga utamaduni wa kulinda afya zao na kuheshimu kanuni za kazi migodini.
"Mazingira ya mgodi ni hatarishi. Kutovaa vifaa kinga ni kuhatarisha maisha yako. Ni jukumu letu sote kulinda afya zetu na kuhifadhi mazingira," amesema.
Bw. Fahad ameongeza kuwa hatua za kurekebisha mazingira baada ya uchimbaji—ikiwemo kufukia mashimo na kupanda miti—ni muhimu kwa usalama wa jamii, hasa watoto na mifugo.
Wakati wa majadiliano, baadhi ya wachimbaji wameeleza kufurahishwa na mafunzo hayo na kuomba kupewa msaada wa vifaa vya kujikinga ili kusaidia kulinda afya ya uzazi na kupunguza maambukizi ya VVU katika maeneo ya migodi.
Mafunzo haya ni sehemu ya mikakati ya UNDP ya kuimarisha mchango wa Sekta ya Madini nchini kwa kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinakuwa salama, zenye tija na zinazozingatia masuala ya afya na mazingira.
Kwa mujibu wa waandaaji, mafunzo kama haya yataendelea kutolewa katika mikoa mingine ili kusaidia kuwawezesha wachimbaji wadogo kuendana na viwango vya kitaifa na kimataifa vya uchimbaji bora na salama.
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.