[Latest Updates]: UDSM yaridhia kukilea Chuo cha Madini

Tarehe : March 22, 2018, 8:52 a.m.
left

Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) umeridhia kukilea Chuo cha Madini Dodoma (MRI) baada ya kuombwa na Wizara ya Madini ambayo ndiyo inamiliki Chuo hicho.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayeshughulikia Taaluma, Profesa Bonaventure Rutinwa akielezea utayari wa UDSM kukilea Chuo cha Madini, kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini (hawapo pichani), walipotembelea Kampasi ya Nzega ya Chuo hicho wakiwa katika ziara ya kazi, Machi 17 mwaka huu.[/caption]

Dhamira hiyo iliwekwa wazi mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, ilipotembelea na kukagua Kampasi ya Chuo cha Madini iliyopo Nzega mkoani Tabora, Machi 17 mwaka huu.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayeshughulikia Taaluma, Profesa Bonaventure Rutinwa alisema kuwa UDSM ina uzoefu wa kutosha katika kulea vyuo mbalimbali hivyo iko tayari kufanya kazi hiyo.

“Sisi tunataka kuthibitisha kwamba tuko tayari kukilea hiki Chuo, kama tutapewa jukumu hilo. Hii ni kwa sababu tunao uzoefu wa kutosha uliotokana na kulea vyuo vingine mbalimbali vikiwemo SUA, Muhimbili, Mzumbe na vingine kadhaa,” alisema.

Aidha, aliongeza kuwa, katika Mpango-Kazi walioundaa na kuuwasilisha wizarani, umebainisha kuwa udahili wa wanafunzi utaanza mapema mwakani.

“Mwaka huu tumepanga uwe wa maandalizi lakini mwakani tunapanga kuanza udahili wa wanafunzi wa UDSM wanaosomea Kampasi ya Nzega na Dodoma.”

Awali, akiwasilisha taarifa ya Chuo cha Madini kwa Kamati hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila alisema kuwa Mpango wa Serikali ni kuifanya MRI kuwa kitovu cha mafunzo ya kozi mbalimbali za madini hapa nchini.

“Wizara iliunda kamati  kwa ajili ya kupitia kitaalam miundombinu yote iliyoko kampasi ya Nzega na Dodoma pamoja na kuangalia uwezekano wa kuimarisha taaluma katika Chuo hiki; kuimarisha uendeshaji wa Chuo; uanzishaji wa kozi mpya na hasa kukiwezesha Chuo kuwa cha mfano na kitovu cha mafunzo ya kozi zote za madini nchini,” alifafanua.

Alisema kuwa, Wizara imeshapokea taarifa ya Kamati husika na inaifanyia kazi ili kuangalia uwezekano wa UDSM kukilea Chuo hicho.

Aidha, Profesa Msanjila alieleza kuwa lengo kuu la kuanzishwa kwa Kampasi ya Nzega ni kuongeza wataalam wa kada ya kati katika sekta ya madini. Hivyo, pamoja na shughuli nyingine za taaluma, Kampasi hiyo ni mahsusi kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa vitendo katika fani za jiolojia na utafutaji wa madini, uhandisi wa uchimbaji madini, uhandisi wa uchenjuaji madini, usimamizi wa mazingira migodini na upimaji wa ardhi na migodi.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakikagua majengo mbalimbali ya Chuo cha Madini Kampasi ya Nzega, walipokuwa katika ziara ya kazi Machi 17 mwaka huu.[/caption]

Vilevile, alieleza lengo jingine kuwa ni kukipanua Chuo hicho kiweze kuendesha shughuli zake kwa ufanisi zaidi, mathalani Kampasi ya Nzega ambayo ina migodi itakayowezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo.

Chuo cha Madini kilianzishwa rasmi mwaka 1982 kwa lengo la kutoa mafunzo ya kada ya kati katika sekta ya madini. Chimbuko la wazo hilo lilitokana na mahitaji ya watendaji wa kada hiyo.

Jumla ya wanafunzi 542 wamedahiliwa na Chuo kufanya mafunzo ya muda mrefu kwa nadharia na vitendo katika fani mbalimbali za madini.

Imeandaliwa na:

Veronica Simba, Nzega

Afisa Habari,

Wizara ya Madini,

Kikuyu Avenue,

P.O Box 422,

40474 Dodoma,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,

BaruaPepe: info@madini.go.tz,                                             

Tovuti: madini.go.tz

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals