[Latest Updates]: Taarifa za utafiti wa madini zitolewe kwa wananchi-Biteko

Tarehe : Nov. 16, 2018, 8:56 a.m.
left

Na Greyson Mwase, Singida

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ameuagiza Mgodi wa Dhahabu wa Shanta uliopo katika wilaya ya Ikungi mkoani Singida kuhakikisha unatoa taarifa za tafiti zake zilizofanyika katika maeneo mbalimbali ili wachimbaji wadogo waweze kuzitumia katika kubaini madini yaliyopo na kuanza kuchimba kwa kufuata sheria na kanuni za madini.

Naibu Waziri Biteko alitoa agizo hilo leo tarehe 19 Novemba 2018 kwenye mkutano wa hadhara na wachimbaji wadogo wa madini uliofanyika katika tarafa ya Mang’onyi wilayani Ikungi mkoani Singida kama sehemu ya ziara yake katika mkoa huo yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wachimbaji wa madini.

Aliongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini imeweka mazingira bora ya uchimbaji  wa madini kwa wachimbaji wadogo ikiwa ni pamoja na kuwapatia taarifa mbalimbali  za utafiti zilizofanywa na Wakala wa Utafiti na Jiolojia Tanzania (GST) na kampuni za utafiti wa madini lengo  likiwa  ni  kuhakikisha kuwa uchimbaji wao unakuwa wa uhakika na sio wa kubahatisha.

Akielezea maboresho mengine yaliyofanywa katika sekta ya madini, Biteko alisema Serikali imeboresha  Sheria ya Madini inayotambua madini kama mali ya watanzania  yanayosimamiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.

Aliendelea kusema kuwa, Serikali imeweka mkakati wa kurasimisha wachimbaji wadogo wa madini wasio rasmi na kuwapatia  leseni za madini ili uchimbaji wao ulete tija kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Biteko aliwataka wachimbaji wadogo wa madini kuunda vikundi na kupewa leseni ili waanze kuchimba   na kulipa kodi serikalini.

“Sisi kama Serikali kupitia Wizara ya Madini lengo letu ni kuhakikisha kuwa tunaweka mazingira bora kwa wachimbaji wadogo wa madini ili uchimbaji uongeze kasi ya ukuaji wa uchumi kupitia kodi na tozo mbalimbali,” alisema Biteko.

Wakati huohuo Biteko aliwataka wananchi wanaoishi karibu na Mgodi wa Dhahabu wa Shanta kutokuharibu miundombinu  ya maji iliyowekwa ili iweze kunufaisha wananchi wote.

Awali wakiwasilisha kero mbalimbali wakazi hao waliiomba Wizara ya Madini kuwapatia maeneo kwa ajili ya uchimbaji wa madini ili waweze kujiingizia kipato na kulipa kodi serikalini.

Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji wadogo wa madini katika tarafa ya Mang’onyi iliyopo wilayani Ikungi mkoani Singida, Consolata Joseph alisema kuwa uchimbaji wao  umekuwa ni wa kubahatisha na hata kuvamia maeneo yenye leseni kubwa ya madini inayomilikiwa na Kampuni ya Dhahabu ya Shanta.

Aliongeza kuwa, kama wachimbaji wadogo wapo tayari kulipa kodi stahiki serikalini mara baada ya kupatiwa maeneo na kuanza kuendesha shughuli za uchimbaji wa madini.

Awali akizungumza katika ziara hiyo, Meneja Mkuu  wa Mgodi wa Dhahabu wa Shanta uliopo wilayani Ikungi mkoani Singida, Philbert Rweyemamu alisema mgodi umeshaanza kutoa fidia na kuongeza kuwa mpaka sasa umeshatoa shilingi bilioni 2.6 pamoja na ujenzi wa makazi mbadala ambapo mpaka sasa wameshajenga nyumba sita.

Aliongeza kuwa mpaka ifikapo mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka huu, mgodi unatarajia kukamilisha ujenzi wa nyumba nyingine sita na kufanya idadi ya nyumba kuwa 12 kama sehemu ya kuhakikisha wananchi wanaolipwa fidia wanaishi katika mazingira mazuri.

Akizungumzia changamoto za mgodi wake, Rweyemamu alieleza kuwa ni pamoja na wachimbaji wadogo haramu kuvamia eneo la mgodi  na kuchimba madini, miundombinu kuhujumiwa na baadhi ya wananchi kugomea fidia inayotolewa na kampuni hiyo.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals