Tarehe : Feb. 28, 2018, 6:45 a.m.
Juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Madini za kuhakikisha rasilimali Madini inawanufaisha watanzania zimezaa matunda baada ya kupata shilingi Bilioni 1.614 kutokana na mgawo wa mwisho wa fedha za Mrabaha na Asilimia Moja ya ada ya ukaguzi katika mauzo ya Almasi.
Hayo yalielezwa na Waziri wa Madini, Angellah Kairuki tarehe 08 Novemba, 2017 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Wizara ya Madini zilizopo jijini Dar es Salaam. Mkutano huo pia ulimhusisha Katibu Mkuu wa Wizara, Profesa Simon Msanjila, Kamishna wa Madini Nchini, Mhandisi Benjamin Mchwampaka na Wataalam wa Madini.
Waziri Kairuki alisema kuwa mapato hayo yanatokana na mauzo ya mzigo wa Karati 39,567.96 za kampuni ya Williamson Diamond Limited katika soko la Almasi nchini Ubelgiji baada ya kuruhusiwa kuuza na Serikali.
Alisema kuwa, awali Wizara ya Madini ilizuia mzigo wa Almasi za Kampuni ya Williamson Diamonds Ltd zilizokuwa zinasafirishwa kwenda Antwerp-Ubelgiji hapo tarehe 31 Agosti 2017 ili kujiridhisha kuhusu thamani halisi ya Almasi hizo, mzigo huo bado upo na taratibu za kuthibitisha thamani halisi ya Almasi hizo zinaendelea.
Aliendelea kusema kuwa, hata hivyo, Serikali iliruhusu Williamson Diamond Limited kuendelea na uzalishaji wa Almasi na baada ya kuzalisha kiasi cha karati 39,567.96 waliomba waruhusiwe kuuza Almasi hizo.
Alisisitiza kuwa Serikali ilikubali na Wataalam wa Serikali walithaminisha Almasi hizo na kupata thamani ya awali kuwa Dola za Marekani 8,191,644.99 na mrabaha wa awali ukalipwa jumla ya Dola za Marekani 491,498.70 na ada ya ukaguzi Dola za Marekani 81,916.45 na hivyo Serikali kupata jumla ya Dola za Marekani 573,418.15 sawa na shilingi Bilioni 1.288.
Aliongeza kuwa, tarehe 20 Oktoba 2017 Almasi hizo zilisafirishwa kwenda Ubelgiji na Serikali ilituma Maafisa wake kusimamia uuzwaji wa Almasi hizo ambapo Almasi huuzwa kwa njia ya mnada.
“ Napenda kuufahamisha umma kuwa tarehe 07 Novemba, 2017 Almasi hizo ziliuzwa kwa Dola za Marekani 10,261,227.76. Thamani hii ni sawa na ongezeko la Dola za Marekani 2,069,582.77 sawa na asilimia 20.16% kulinganisha na thamani ya uthaminishaji wa awali,” alisema Kairuki
Waziri Kairuki aliendelea kufafanua kuwa kutokana na ongezeko hilo baada ya Almasi hizo kuuzwa, Serikali itapata mrabaha zaidi ambao ni wa mwisho (Final royalty) kiasi cha Dola za Marekani 124,174.97 na ada ya ukaguzi Dola za Marekani 20,695.83 ambayo jumla yake ni Dola za Marekani 144,870.80 sawa na Shilingi Milioni 325.525 na kufanya jumla ya mapato yote ya Serikali kutokana na mauzo ya Almasi hizi kuwa ni Dola za Marekani 718,288.95 sawa na Shilingi Bilioni 1.614.
Alieleza pia katika mzigo huo wa Almasi kulikuwa na Almasi moja yenye rangi adimu (Pink diamond) yenye uzito wa karati 5.92 (Gramu 1.184) ambayo yenyewe pekee iliuzwa kwa Dola za Marekani 2,005,555.00 sawa na Sh. 4.51 Bilioni .
Waziri Kairuki aliwahakikishia Watanzania kuwa Serikali itaendelea kusimamia kwa umakini Rasilimali Madini ili kuhakikisha kuwa Nchi inanufaika ipasavyo na kusisitiza kufanya maboresho zaidi katika uthaminishaji, ukaguzi na usimamizi wa madini ili kudhibiti mianya yote ya upotevu wa mapato ya Serikali.
Katika hatua nyingine Waziri Kairuki alisema kuwa usiku wa kuamkia tarehe 29 Oktoba, 2017 katika eneo la Kiabakari, Serikali ilikamata sampuli za miamba ya madini ya dhahabu takriban kilo 600 zilizokuwa zinasafirishwa na Kampuni ya wachina inayoitwa ZEM (T) Ltd bila vibali kutoka Wizara ya Madini.
Alisema Serikali imeamua kuwapeleka mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake kwa kosa la kusafirisha na kukutwa na sampuli hizo bila kibali.
Kairuki aliwataka wachimbaji madini wote kulipa kodi, mrabaha na ada zote za Serikali zinazohusika katika shughuli za uchimbaji na biashara ya madini na kufuata kanuni na sheria zote katika umiliki na usafirishaji wa sampuli au madini kutoka eneo moja kwenda eneo jingine.
Imeandaliwa na:
Greyson Mwase na Nuru Mwasampeta, Dar es Salaam,
Maafisa Habari,
Wizara ya Madini,
5 Barabara ya Samora Machel,
S.L.P 2000,
11474 Dar es Salaam,
Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,
Barua Pepe: info@madini.go.tz,
Tovuti: madini.go.tz
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.