[Latest Updates]: STAMICO Yakabithiwa Leseni Kubwa ya Utafiti na Uchimbaji Madini Adimu Vilima vya Wigu, Morogoro

Tarehe : July 24, 2025, 11:38 a.m.
left

Ni maelekezo ya Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan

Lengo ni kukuza uwekezaji wa STAMICO kwenye madini mkakati

Waziri Mavunde akabidhi Leseni na kuelekeza uendelezaji wa Leseni kuanza mara moja

Mradi utachochea ukuaji wa Uchumi Morogoro

Morogoro

Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amekabidhi Leseni ya Utafiti na Uchimbaji Mkubwa wa Madini Adimu na Muhimu ambayo ni ya kimkakati ya Rare Earth Elements (REE) kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), ikiwa ni hatua muhimu ya kuliwezesha shirika kuingia kwenye shughuli za uchimbaji mkubwa kwa lengo la kuwanufaisha wananchi wote wa Tanzania.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo Julai 24, 2025 katika viwanja vya Shule ya Msingi Sesenga kijiji cha Sesenga Kata ya Mgazi Wilaya ya Morogoro, kufuatia uamuzi wa Serikali wa kuirejesha leseni hiyo kutoka kwa kampuni ya Wigu Hill Mining Company Limited baada ya kumalizika kwa shauri la madai kwenye Baraza la Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji(ICSID).

Akizungumza mbele ya mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara kwenye hafla ya makabidhiano ya leseni hiyo, Waziri Mavunde amesema kuwa madini ya Rare Earth Elements ni miongoni mwa madini ya kimkakati ambayo kwa sasa yanahitajika kwa kiwango kikubwa duniani  kutokana na umuhimu wake katika sekta ya teknolojia ya kisasa.

"Madini haya yanatumika katika vifaa vya kivita, kutengeneza simu janja, kompyuta, betri za magari ya umeme, vifaa vya matibabu na mashine mbalimbali. Hii ni fursa adhimu kwa kijiji cha Sesenga, Wilaya ya Morogoro, Mkoa na Taifa kwa ujumla kunufaika na rasilimali hii muhimu," amesisitiza Waziri Mavunde.

Pia, Waziri Mavunde amebainisha kuwa mradi huo utafungua fursa nyingi za ajira kwa wakazi wa maeneo ya jirani na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kupewa kipaumbele kwa wananchi wanaozunguka mgodi kuuza bidhaa zao mgodini (Local content) na kupitia uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR).

Vilevile, ameeleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro itaongeza mapato yake kupita tozo za huduma ambazo hutozwa kwenye shughuli za madini.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde ameitaka STAMICO kuanza mara moja mchakato wa uendelezaji wa leseni hiyo ili shughuli za uzalishaji madini hayo ziweze kuanza  kwa wakati.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mussa Kilakala amempongeza Waziri Mavunde kwa kuisimamia vizuri Sekta ya Madini na kumuahidi Waziri huyo kuendelea kusimamia sekta hiyo kwa karibu kwa ajili ya masilahi ya taifa.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Eng. Yahya Samamba amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira rafiki na salama kwenye maeneo ya uchimbaji madini nchini ambapo kwa sasa wachimbaji wananufaika na rasilimali hiyo.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse, ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kuendelea kuwaamini na kulikabidhi shirika hilo leseni hiyo muhimu na kumhakikishia Waziri Mavunde kuwa STAMICO iko tayari kuanza kazi kwa wakati na kuhakikisha kuwa mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi, kwa muda uliopangwa na kwa kuzingatia manufaa mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

"Tunatambua wajibu wetu mkubwa kwa taifa, STAMICO iko tayari kusimamia mradi huu kwa weledi wa hali ya juu ili kuleta tija na kuongeza mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa," amesema Dkt. Mwasse.

Uamuzi wa Serikali kukabidhi leseni hiyo kwa STAMICO ni sehemu ya jitihada za kulinda maslahi ya Taifa katika Sekta ya Madini kwa kuhakikisha maeneo yenye rasilimali hayakai bila kuendelezwa na kwamba rasilimali hizo zinachangia moja kwa moja katika ustawi wa wananchi na uchumi wa nchi.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals