[Latest Updates]: Serikali yaahidi kurekebisha mapungufu yatakayobainika katika sheria ya madini

Tarehe : April 28, 2018, noon
left

Serikali imesema iko tayari kurekebisha mapungufu yatakayobainika katika Sheria au Kanuni za Madini ili kuhakikisha wadau wote wa sekta hiyo wananufaika ipasavyo hivyo kukuza Pato la Taifa.

Baadhi ya wafanyabiashara na wachimbaji wa madini nchini, wakizungumza katika Mkutano baina ya Naibu Mawaziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Doto Biteko pamoja na viongozi wa Chama cha Wafanyabishara wa Madini Tanzania (TAMIDA) na Chama cha Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA). Mkutano ulifanyika Februari 14 mwaka huu Arusha.[/caption]

Hayo yalisemwa Februari 14 jijini Arusha na Naibu Mawaziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Doto Biteko wakati wa Mkutano wao na wadau wa sekta ya madini wakiwemo Chama cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA) na Chama cha Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA).

Akizungumzia suala hilo, Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini haitasita kufanya marekebisho katika sheria au kanuni za madini zitakazobainika kuwa kikwazo katika biashara ya madini nchini.

Akiunga mkono maneno hayo, Naibu Waziri Biteko alisema “Sheria au Kanuni siyo Msahafu ambao hauwezi kubadilishwa hivyo pale tutakapojiridhisha kuna mapungufu, tutarekebisha kusudi mambo yaende vizuri.”

Biteko na Nyongo walisema kuwa, dhamira ya Serikali ni kuona sekta ya madini inalinufaisha Taifa ipasavyo kwa kukuza vipato vya wananchi wanaojishughulisha na shughuli za madini lakini kubwa zaidi ni kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa.

“Mchango wa Madini katika Pato la Taifa bado kwa sasa ni asilimia 4.2 tu. Hii ni ndogo sana. Tunaamini kuwa ikiwa sekta hii itasimamiwa vizuri, mchango wake unaweza kufikia asilimia 10 na kuendelea,” alisema Nyongo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Biteko alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kwa dhati kuhakikisha madini yanayopatikana Tanzania, hususan Tanzanite, yanawanufaisha watanzania zaidi kuliko nchi nyingine yoyote kwani yanapatikana nchini tu. “Tumechoka kuona madini yetu wenyewe yananufaisha mataifa mengine zaidi yetu, nasi kuambulia kipato kidogo sana kisichostahili. Hili tutalisimamia kwa nguvu zetu zote na tunaamini inawezekana,” alisema.

Kauli hiyo ya Naibu Mawaziri ilikuja kufuatia vyama hivyo vya wachimbaji na wafanyabiashara ya madini kuwasilisha taarifa zao katika mkutano huo; ambapo walieleza kuwa moja ya changamoto kubwa wanayoomba Serikali ifanyie kazi ni kubadili kanuni katika Sheria ya Madini inayoelekeza kuongeza thamani ya madini hapa nchini kabla ya kuyasafirisha nje ya nchi.

Mbunge wa Simanjiro James Ole Millya, akizungumza katika Mkutano baina ya Naibu Mawaziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Doto Biteko pamoja na viongozi wa Chama cha Wafanyabishara wa Madini Tanzania (TAMIDA) na Chama cha Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA). Mkutano ulifanyika Februari 14 mwaka huu Arusha.[/caption]

Akiwasilisha taarifa husika kwa niaba ya wanachama wa TAMIDA, Mwenyekiti wake, Sammy Mollel alisema kuwa kumekuwa na mkanganyiko kuhusu maelezo ya kanuni hiyo inayohusu uongezaji thamani madini nchini.

“Sisi tunaamini Kanuni hiyo inalenga madini ya metali na ya viwanda lakini siyo madini ya vito. Madini ya vito yakikatwa, yanapungua thamani hivyo tunaomba Serikali itufikirie katika hili.”

Hata hivyo, Naibu Mawaziri Biteko na Nyongo, wakitolea ufafanuzi zaidi suala hilo, walisema kuwa Wizara iko katika hatua za mwisho kukamilisha Mwongozo maalum utakaobainisha kila aina ya madini yanapaswa kuwa katika hali gani au kuongezwa thamani kwa kiasi gani kabla hayajatolewa kibali cha kuyasafirisha nje ya nchi. “Mwongozo huo tutautoa hivi karibuni maana kwa sasa tunaukamilisha.”

Katika hatua nyingine, Nyongo na Biteko walisisitiza ushirikiano baina ya Serikali na wadau hao wa sekta ya madini katika kufanikisha udhibiti wa utoroshaji wa madini hivyo kuiwezesha Serikali kupata mapato stahiki kutokana na biashara hiyo.

“Tunaomba sana mtupe ushirikiano. Tukishirikiana tutafanikiwa. Tuleteeni majina ya wanaotorosha madini pamoja na taarifa nyingine mbalimbali zinazohusu sekta hii ambazo mnahisi zinaweza kutusaidia kudhibiti suala husika.”

Akizungumzia kuhusu mabadiliko yanayoendelea kufanywa katika sekta ya madini ili kudhibiti mianya ya wizi na utoroshwaji wa madini, Naibu Waziri Biteko aliwataka wafanyabiashara na wachimbaji wa madini kuachana na dhana potofu kuwa Serikali inawachukia.

Baadhi ya wafanyabiashara na wachimbaji wa madini nchini, wakizungumza katika Mkutano baina ya Naibu Mawaziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Doto Biteko pamoja na viongozi wa Chama cha Wafanyabishara wa Madini Tanzania (TAMIDA) na Chama cha Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA). Mkutano ulifanyika Februari 14 mwaka huu Arusha.[/caption]

“Mkiona tunashughulika katika kipindi hiki cha mpito msidhani Serikali inawachukia. Naomba niwahakikishie kuwa Rais John Magufuli anawapenda sana wachimbaji. Lakini anachukia sana anapoona wachimbaji wanasaidia kufanya haya madini yanufaishe nchi nyingine. Sasa mtusaidie.”

Aidha, Naibu Mawaziri Nyongo na Biteko waliwahakikishia wachimbaji na wafanyabiashara hao wa madini kuwa, hoja zote walizoziwasilisha zitafanyiwa kazi na Serikali.

“Tumesikia hoja zote mlizowasilisha. Ni nzuri. Tumezichukua. Hii ni pamoja na suala la ushirikishwaji ambalo mmeliongelea. Sisi tutaendelea kushirikiana nanyi.”

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini Gabriel Daqarro, Mbunge wa Simanjiro James Ole Millya, Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini Adam Juma pamoja na wataalam mbalimbali wa Wizara ya Madini.

Imeandaliwa na:

Veronica Simba, Arusha

Afisa Habari,

Wizara ya Madini,

Kikuyu Avenue,

P.O Box 422,

40474 Dodoma,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,

BaruaPepe: info@madini.go.tz,                                             

Tovuti: madini.go.tz

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals