[Latest Updates]: Soko la Madini Chunya laleta mapinduzi kwenye Sekta ya Madini

Tarehe : Dec. 2, 2019, 8:06 a.m.
left

Lengo la ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka 2019-2020 Chunya lafikia asilimia 91

Wanyabiashara wa Madini waipongeza Wizara ya Madini, Tume ya Madini

Greyson Mwase na Nuru Mwasampeta

Imeelezwa kuwa kuanzishwa kwa Soko la Madini Chunya lililopo mkoani Mbeya mapema Mei 02, 2019 kumepelekea mabadiliko makubwa kwenye ukusanyaji wa maduhuli kwenye Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Chunya ambapo kwa sasa wanakusanya wastani wa shilingi bilioni 1.09 kwenye biashara ya dhahabu  tofauti na awali ambapo walikuwa wanakusanya kiasi cha shilingi milioni 114.9 kenye biashara ya dhahabu.

Hayo yalielezwa leo tarehe 02 Desemba, 2019 na Afisa Madini Mkazi wa Chunya, Godson Kamihanda kupitia mahojiano maalum  kwenye maandalizi ya kipindi maalum chenye kuelezea mafaniko  ya Sekta ya Madini kupitia masoko ya madini yaliyoanzishwa kinachoandaliwa na Wizara ya Madini, Tume ya Madini kwa kushirikiana na Idara ya Habari MAELEZO.

Kamihanda alisema kuwa, kabla ya kuanzishwa kwa  Soko la Madini Chunya kulikuwepo na utoroshwaji mkubwa wa madini kutokana na wafanyabiashara wa madini hayo kuuza kwa kificho na kukwepa kulipa kodi mbalimbali serikalini.

Alisema kuwa, mara baada ya kuanzishwa kwa soko husika na kufanya uhamasishaji wa matumizi ya soko, wafanyabiashara wengi wa madini walianza kuomba leseni za biashara ya madini na kuanza kufanya biashara mara moja.

Alifafanua kuwa, uwepo wa soko la madini  umesaidia kwa kiwango kikubwa kwa  ofisi yake kufikia kwa asilimia 91.2 ya  lengo la ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka wa fedha 2019-2020 ambapo mpaka sasa wameshakusanya shilingi bilioni 17.33 kati ya lengo lililowekwa la shilingi bilioni 18.86.

Aliongeza kuwa, ili kuimarisha uendeshaji wa  Soko la Madini Chunya, kumefunguliwa vituo vitano vya ununuzi wa madini ambapo wafanyabiashara wadogo wa madini hununua na baadaye huyauza kwenye  Soko kubwa la Madini

"Hii tulifanya kama njia mojawapo ya kusogeza huduma kwa wafanyabiashara wadogo wa madini  na kuongeza ukusanyaji maduhuli huku Serikali ikidhibiti utoroshwaji wa madini," alisema Kamihanda.

Akielezea mikakati ya uboreshaji zaidi wa ukusanyaji wa maduhuli unaofanywa na ofisi yake, Kamihanda alisema kuwa ni pamoja na kufungua vituo zaidi vya ununuzi wa madini ya dhahabu pamoja na usajili wa mialo ya kuzalisha dhahabu kwa kushirikiana na watendaji wa vijiji.

Aliongeza kuwa mikakati mingine ni pamoja na kutoa elimu kwa wachimbaji na wafanyabiashara  wa madini  na kuwataka wafanyabiashara wa madini kutumia Soko la Madini Chunya pamoja na vituo vilivyoanzishwa ili kuuza madini yao kwa kufuata bei elekezi na kupata faida kubwa huku wakilipa kodi mbalimbali Serikalini.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Sophia Kumbuli akielezea mapinduzi makubwa yaliyofanywa na Soko la Madini Chunya, mbali na kumpongeza Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dkt. John Pombe Magufuli, Wizara ya Madini pamoja na Tume ya Madini alieleza kuwa uwepo wa soko hilo umeleta mabadiliko makubwa kwenye ukusanyaji wa maduhuli kwenye halmashauri husika.

Alieleza kuwa kabla ya kuanzishwa kwa soko hilo, halmashauri yake ilikuwa ikipanga kukusanya kiasi cha shilingi  milioni 22 kwa mwaka na kufanikiwa kukusanya wastani wa shilingi milioni 19 tu.

Alisisitiza kuwa tangu kuanzishwa kwa Soko la Madini Chunya hadi kufikia tarehe 21 Novemba, 2019 halmashauri ilikusanya kiasi cha shilingi milioni 278 ambazo zitatumika kuboresha huduma za jamii kama vile barabara, shule, maji, n.k

Wakati huohuo wakizungumza kwa nyakati tofauti wafanyabiashara wa madini katika Soko la Madini Chunya, walipongeza Serikali kupitia Wizara ya Madini na Tume ya Madini kwa uanzishwaji wa soko husika kwani biashara ya madini wilayani Chunya imekuwa ni ya uhakika huku wakineemeka na kulipa kodi mbalimbali Serikalini.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabishara wa madini wa Soko la Madini Chunya, Katibu wa Soko la Madini Chunya, Pius Madabuke alieleza kuwa uanzishwaji wa soko la madini umepelekea upatikanaji wa dhahabu wa uhakika kwani hapo awali wafanyabiashara wengi walikuwa wakitorosha madini hayo.

Alieleza kuwa manufaa mengine yaliyopatikana katika soko hilo ni pamoja na upatikanaji wa bei elekezi ambapo kwa sasa wanauza kwa faida kubwa hali iliyopelekea kufutika kwa masoko bubu yaliyokuwepo majumbani.

Katika hatua nyingine, Madabuke aliiomba Serikali kupitia Tume ya Madini kuongeza wataalam zaidi kwenye vituo vya kununulia madini na kuhamasisha Taasisi za Kifedha kutoa mikopo kwa wafanyabiashara wa madini.

Naye Katibu wa Kituo cha Ununuzi wa Dhahabu Chunya, Emmanuel Nilla aliongeza kuwa tangu kuanzishwa kwa kituo hicho wafanyabiashara wadogo wa madini wameondokana na dhana ya kuuzia madini ya dhahabu majumbani kutokana na faida kubwa inayopatikana kwenye uuzaji wa dhahabu kupitia katika kituo hicho.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals