[Latest Updates]: Wanaodai fidia Nyamongo wahakikishiwa kulipwa

Tarehe : March 28, 2018, 10:45 a.m.
left

Serikali imewahakikishia Wananchi wa Tarime wanaostahili kulipwa fidia na Mgodi wa North Mara uliopo wilayani humo ambao walifanyiwa tathmini kuwa watalipwa.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo alisema hayo Desemba 28, 2017 wakati wa ziara yake katika Kijiji cha Nyabichune, Kata ya Matongo Wilayani Tarime kwenye mkutano na wananchi na wachimbaji wadogo.

Mwananchi wa Kijiji cha Kewanja, Kata ya Kemamba Wilayani Tarime, Samuel Peter akimueleza Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) kuhusu suala la ulipaji fidia kwenye maeneo waliyopisha Mgodi wa Dhahabu wa North Mara ili kuendeleza uchimbaji. Nyuma yake ni Eliza Malembela ambaye pia ni mwananchi wa eneo hilo akisubiri kumueleza Naibu Waziri kero yake.[/caption]

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wa maeneo hayo walimueleza Naibu Waziri malalamiko mbalimbali ikiwemo suala la ulipaji wa fidia, ajira, mahusiano duni na mgodi na mgodi kushindwa kununua bidhaa zinazozalishwa na wananchi wa maeneo hayo.

Akijibu hoja hizo, Naibu Waziri Nyongo aliuagiza mgodi huo wa North Mara kuhakikisha unawalipa wananchi fidia wanayostahili. “Haiwezekani mmefanya tathmini halafu baadaye mnageuka kwamba hamtolipa, ubabaishaji wa aina hiyo haupo maana mlikua mmekwisha waandaa wananchi kisaikolojia kwamba mtawalipa,” alisema.

Kwa upande mwingine aliwaonya wananchi wanaofanya udanganyifu kuacha tabia hiyo mara moja kwani kufanya hivyo kunasababisha malipo ya fidia kuchelewa kwa wananchi wanaostahili.

“Hapa nimeelezwa tathmini ya kwanza ilikua na kiasi kidogo cha fidia kilichokuwa kinadaiwa tofauti na tathmini ya mara ya pili na hapa inaonekana kuna baadhi yenu wamefanya udanganyifu,” alisema.

Aliwataka wananchi hao kuwatambua waliofanya udanganyifu ili kuharakisha zoezi la ulipaji wa fidia kwa mujibu wa sheria na makubaliano.

“Tathmini ya mara ya pili imeonekana ina kiwango kikubwa, tunaomba ushirikiano wenu kuwabaini waliojiongeza ili zoezi la ulipaji fidia likamilike kwa wakati bila kuwepo udanganyifu,” aliagiza Naibu Waziri Nyongo.

Akizungumzia suala la ajira, Naibu Waziri Nyongo aliuagiza mgodi huo kuhakikisha unatoa kipaumbele kwa wananchi wa maeneo yanayozunguka mgodi na hapohapo aliwaasa wananchi watakaonufaika na ajira hizo kufanya kazi kwa uadilifu.

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Kewanja, Kata ya Kemamba Wilayani Tarime wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) akizungumzia masuala yanayohusu Mgodi wa Dhahabu wa North Mara ikiwemo ulipaji wa fidia na suala la ajira kwenye mgodi huo.[/caption]

“Ajira zitolewe kwa wenyeji wenye sifa na nyie ndugu zangu mkipewa kazi fanyeni kwa uadilifu, msiwaharibie wengine wenye nia ya kufanya kazi,” alisema Nyongo.

Kuhusu suala la manunuzi ya bidhaa na huduma kutoka kwa wenyeji, Nyongo alisisitiza mgodi kutumia huduma na bidhaa zinazozalishwa na wenyeji wa hapo jambo ambalo alisema likifanyika kwa weledi litachangia katika uboreshaji wa mahusiano baina ya pande hizo mbili.

Aidha, alitoa rai kwa Halmashauri kuwa fedha wanazopokea za ushuru wa huduma (service levy) kutoka mgodini hapo ambazo zinatakiwa kuleta maendeleo hapo Nyamongo zirudishwe hapo kufanya maendeleo.

“Halmashauri isimamie vema ili kupata ushuru wa huduma kwa kiasi kinachostahili kutoka kwenye mgodi kwa ajili ya maendeleo,” aliagiza Nyongo.

Naibu Waziri Nyongo alisisitiza suala la uboreshaji wa mahusiano, umuhimu wa kutii na kufuata sheria, kuepuka vurugu, amani, usalama na upendo na vilevile mgodi kuachia maeneo ambayo hayafanyiwi kazi kwa ajili ya uchimbaji mdogo.

Imeandaliwa na:

Mohamed Saif,

Afisa Habari,

Wizara ya Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,

Barua Pepe: info@madini.go.tz,                                                                               

Tovuti: madini.go.tz

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals