[Latest Updates]: Taasisi zinazohusika na Mradi wa Magadi Soda - Engaruka zatakiwa kushirikiana kuwezesha mradi huo kuanza

Tarehe : Dec. 22, 2023, 10:21 a.m.
left


Katibu Mkuu Madini  asema utaokoa matumizi makubwa ya Fedha za Kigeni

Arusha

Serikali imewataka Viongozi wa Taasisi zinazohusika na Mradi wa Kimkakati wa Magadi Soda ulioko Engaruka Wilayani Monduli Mkoa wa Arusha kushirikiana kwa karibu katika kukamilisha taratibu zote zinazohitajika ili Mradi huo unaotarajiwa kuongeza ajira, malighafi za viwandani, kukuza biashara na uchumi wa Taifa uanze kutekelezwa kwa wakati.

Hayo yalibainishwa Desemba 21, 2023 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Bw. Elijah Mwandubya na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Bw. Kheri Mahimbali walipotembelea Mradi huo wa Kimkakati wa Magadi kwa lengo la kuona utekelezaji wake na kutatua changamoto mbalimbali zitakazowezesha kuanza kutekelezwa rasmi kwa mradi huo.

Akizungumza mara baada ya kufanya ziara katika Mradi huo Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah alisema ziara ya Makatibu Wakuu katika kuutembelea mradi huo ni ishara tosha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuona kuwa mradi huo unaanza kutekelezwa mara moja.

“Ziara hii imeshirikisha wizara tatu na jumla ya Taasisi nne na itafanya kazi kwa kushirikiana na vijiji vinne katika kujadili mambo mbalimbali yanayohusu mradi na kuanza kutekelezwa kwa mradi huu ni dhahiri kuwa utasaidia katika kuboresha maisha ya wakazi wa Engaruka na Taifa kwa ujumla, kuongeza mapato kwa Serikali na ipo tayari kuhakikisha utekelezaji wake unaanza mara moja,’’ alibainisha Dkt. Abdallah.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Bw. Kheri Mahimbali alibainisha  kuwa kuanza kuchimbwa kwa madini ya Magadi soda nchini kutaokoa kiasi kikubwa cha fedha za kigeni  ambacho kimekuwa kikitumika kuagiza Magadi soda kutoka nje ya nchi kwa ajili ya matumizi ya malighafi hiyo  viwandani.

“Sisi kama wasimamizi wa Sekta ya Madini hapa nchini tunahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kuwa Magadi soda ni madini muhimu sana kwa ajili ya ustawi wa viwanda vingi hapa nchini kwa kuwa yanatumika kama malighafi na tuna viwanda ambavyo tayari vinategemea malighafi hii muhimu” alifafanua  Mahimbali.

Katika hatua nyingine, Mahimbali aliwataka wakazi wa Engaruka na Watanzania kiujumla kuhakikisha wanachangamkia fursa mbalimbali zitakazojitokeza pale ambapo mradi huu utakapoanza kutekelezwa hapa nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo, (NDC) Dkt Nicolaus Shombe alibainisha kuwa NDC kama mwekezaji kwa niaba ya Serikali tayari imekamilisha hatua mabalimbali za kuelekea kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo ikiwemo kufanyika kwa upembuzi yakinifu pamoja na tathmini ya mazingira huku akiishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa namna inavyouchukulia mradi huu kwa uzito wa kipekee na nia ya dhati iliyonayo ya kutaka kutekelezwa kwa mradi huu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Mwl. Happyness Laizer pamoja na Katibu Tawala wa Wilaya ya Monduli Muhsin Kassim walisema wapo tayari kupokea mradi huo huku wakitoa rai kwa wananchi kuchangamkia fursa zitakazotokana na utekelezwaji wa Mradi huo.

Wakizungumza kwa niaba ya wananchi wa Engaruka Viongozi wa eneo hilo wakiwemo Diwani na Mtendaji wa Kata ya Engaruka pamoja na Wenyeviti wa Vijiji vya Engaruka juu, Engaruka chini, Irerendeni pamoja na Oldonyo Lengai walionesha kufurahishwa na hatua ya Serikali kuamua kutekeleza mradi huo utawakaowaletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii hususani katika upatikanaji wa ajira, ukuaji wa biashara na uchumi kwa ujumla.

Mradi wa Magadi soda wa Engaruka ni moja kati ya miradi kumi na saba ya kimkakati ya Serikali ambao upo chini ya Shirika la Taifa la Maendeo (NDC) ambao unaelezwa kuwa utekelezwaji wake utakuwa na manufaa makubwa kiuchumi kwa Taifa kwa kuwa utasaidia katika kutoa malighafi mbalimbali za Magadi soda kwa viwanda ndani na nje ya nchi, kutoa ajira elfu moja za moja kwa moja kwa wananachi ambapo uwekezaji wake unatarajia kugharimu kiasi cha Dola za Marekani Milioni Mia Nne.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals