[Latest Updates]: Wizara ya Madini Yawasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Kamati ya Bunge

Tarehe : March 28, 2022, 11:56 a.m.
left

Taasisi Zaainisha Vipaumbele, Mikakati ya Makusanyo

Wajumbe wa Kamati Wataka Mradi wa Makaa Ya Mawe ya Kupikia wa Stamico Uharakishwe*

Kamati Yataka Wizara Kutupia Jicho Madini ya Kimkakati

Dodoma

Wizara ya Madini na Taasisi zilizo chini yake zimewasilisha kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 katika vikao vya kamati za bunge vinavyoendelea jijini Dodoma.

Akiainisha maeneo ya kipaumble  kwa  Mwaka wa Fedha 2022/2023, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Bw. Adolf Ndunguru amesema kuwa ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli na kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa; kuwaendeleza wachimbaji wadogo na kuwawezesha wananchi kushiriki katika uchumi wa madini; na kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini.

Ameyataja maeneo mengine kuwa ni pamoja na  kuhamasisha biashara na uwekezaji katika Sekta ya Madini;  kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya Wizara ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi; kusimamia mfumo wa ukaguzi wa shughuli za migodi; na  kuendeleza rasilimali watu na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi.

Pia, Katibu Mkuu Ndunguru ameieleza kamati hiyo  kuhusu misingi ya Makadirio ya makusanyo katika Mwaka wa Fedha 2022/23 kwa kusema kuwa ni pamoja na kuongeza mapato yatokanayo na madini ya ujenzi na viwandani kwa kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa maduhuli katika madini hayo;  kuimarisha ufuatiliaji, usimamizi na ukaguzi wa shughuli za Sekta ya Madini;  kudhibiti kikamilifu biashara haramu ya madini inayohusisha utoroshaji wa madini;  kuimarisha na kusimamia biashara ya madini ikihusisha masoko na vituo vya madini yaliyoanzishwa na yatakayoanzishwa ili kuongeza ufanisi na kuvutia wafanyabiashara wengi wa ndani na nje ya nchi kununua na kuuza madini katika masoko hayo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Dunstan Kitandula ameishauri wizara kuweka mfumo wenye mwelekeo mpya wa madini ya kimkakati unaoendana na mahitaji ya sasa ya dunia ili hatimaye ziweze kulinufaisha taifa ipasavyo.

 “Tusipojipanga tutajikuta tumebaki na rasilimali zisizokuwa na manufaa kwetu. Mathalan kwa hivi sasa dunia imeanza kuhama katika matumizi ya makaa ya mawe, kwa kipindi hiki kifupi kilichobaki sisi tumejipangaje kuhakikisha tunaitumia rasilimali hii haraka? Vipi kwa madini yanayohitajika hivi sasa ikiwemo ya viwandani?,” amehoji Kitandula.

Aidha, Kitandula ameishauri wizara kuangalia ikiwa Sera ya Madini ya Mwaka 2009 inayotumika hivi sasa inaakisi mwelekeo wa sasa wa mahitaji ya rasilimali madini zinazohitajika zaidi duniani kwa wakati huu na hivyo kuitaka wizara kuiwezesha kikamilifu taasisi yake ya Jilolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ili iendelee kufanya tafiti za kina ikiwemo kutafiti maeneo mapya ili kuibua zaidi madini ya kimkakati  yanayohitajika kwa sasa duniani.

Awali, wakichangia  taarifa ya wizara na taasisi, wajumbe wa kamati  hiyo wameitaka wizara kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuharakisha utekelezaji wa mradi wa makaa ya mawe kwa ajili ya kupikia kutokana na umuhimu wake katika kukabiliana na athari za ukataji  miti  ikiwemo urahisi wa makaa hayo katika matumizi ya majumbani.

Kwa mujibu wa taarifa ya STAMICO, shirika hilo hivi sasa linasubiri matokeo ya sampuli zilizowasilishwa kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa ajili ya uthibitisho wa viwango kabla ya kusambazwa kwa walaji.

Vilevile, wajumbe  wa kamati wameendelea kuipongeza wizara  na taasisi zake kutokana na namna inavyosimamia sekta hiyo ikiwemo kasi ya ukuaji wa sekta, maendeleo yake pamoja na namna inavyochangia katika ukuaji wa uchumi, Hata hivyo, wajumbe wameshauri kuhusu kuhakikisha kwamba mchango wa sekta hiyo unawagusa  moja kwa moja wananchi hususan wanaozungukwa na shughuli za miradi ya madini ikiwemo kuhakikisha wizara inaendeleza usimamizi na utekelezaji wa madini mengine ambayo yana tija kwa taifa ikiwemo madini ya ujenzi na chumvi.

Wizara ya Madini inatarajia kukutana tena na kamati hiyo tarehe 29 Machi, 2022.

 Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Madini

 

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals