Tarehe : Sept. 28, 2025, 11 a.m.
Geita,
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, amesema Serikali kupitia Wizara inajivunia hatua kubwa iliyopigwa kwa kuongezeka ushiriki wa wanawake kwenye mnyororo mzima wa madini, hatua inayodhihirisha dhamira ya Serikali ya kuendeleza usawa wa kijinsia katika sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.
Ameyasema hayo leo Septemba 28, 2025, katika Maonesho ya Teknolojia ya Madini Geita, wakati akizungumza na Chama cha Wanawake Wachimbaji wa Madini Tanzania (TAWOMA),
Mbibo amesema wanawake wanazidi kushiriki si tu kwenye uchimbaji mdogo, bali pia kwenye biashara, uongezaji thamani, teknolojia na kutoa huduma katika Sekta ya Madini.
“Kwa sasa tunaona mabadiliko makubwa. Wanawake wanashiriki kwenye nyanja zote za mnyororo wa madini, kutoka migodini hadi sokoni. Wizara ya Madini inajivunia kuwa mfano bora wa usawa wa kijinsia nchini,” amesema Mbibo.
Aidha, Mbibo ameongeza kuwa, Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi yanayojumuisha utoaji wa leseni, upatikanaji wa maeneo ya uchimbaji na mafunzo ya kitaalamu, hatua zinazowezesha wanawake kushiriki kwa ufanisi sambamba na wanaume.
“Hatuwezi kuacha kundi kubwa la wananchi nyuma. Wanawake wana mchango mkubwa wa kuleta mageuzi katika sekta ya madini na Wizara itaendelea kusimama bega kwa bega nao,” amesisitiza Mbibo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TAWOMA Salma Ernest amesema hatua zinazozoendelea kuchukuliwa Serikali zimekuwa chachu ya mafanikio kwa wanawake wengi waliokuwa wakikosa nafasi katika sekta hiyo.
Amesisitiza kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini imeendelea kutoa kipaumbele kwa wanawake kwa kuwapatia vitalu vya uchimbaji na kuwasaidia kupata elimu ya kitaalamu.
“Kuongezeka kwa idadi ya wanawake sekta ya madini si tu kunawanufaisha wao binafsi, bali pia kunachangia ustawi wa familia na jamii kwa ujumla” amesema Salma.
Kwa kuongezeka kwa idadi ya wanawake katika Sekta ya Madini, Tanzania inajiweka katika nafasi bora zaidi ya kuendeleza uchumi jumuishi unaozingatia usawa, huku dhana ya “Madini ni Maisha na Utajiri” ikipata tafsiri ya vitendo.
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.