[Latest Updates]: STAMICO Sasa Imefanya Kitu-Kamati ya Bunge

Tarehe : Nov. 24, 2019, 12:59 p.m.
left

Na Asteria Muhozya, Dodoma

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeonesha kuwatia moyo Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini baada ya kuwasilisha taarifa yake kwa kamati hiyo iliyoonesha kuwepo mafanikio kutokana na kuendeleza mgodi wake wa Kiwira, kuendeleza uchimbaji na uuzaji makaa ya mawe kupitia mgodi wake wa Kabulo na uzalishaji dhahabu katika mgodi wa STAMIGOLD.

Wakichangia hoja baada ya kuwasilishwa kwa taarifa kuhusu hatua zilizofikiwa katika kuendeleza migodi ya Kiwira, Stamigold, Buhemba na Backreef, na taarifa ya utekelezaji wa majukumu kwa kipindi cha nusu mwaka 2018/19, kuanzia mwezi Julai hadi Desemba, 2018, wajumbe hao wamesifu jitihada zinazofanywa na shirika hilo kwa kufufua mgodi wake wa Kiwira na uzalishaji unaofanywa Stamigold na Kabulo na kueleza kuwa, hivi sasa kuna mambo yanafanyika na yanakamilika.

Pamoja na mafanikio hayo, kamati imeitaka wizara kuendelea kuzifanyia kazi changamoto za uchimbaji mdogo wa madini nchini huku ikitakiwa kufanyia kazi ushauri uliotokana na mkutano wa Kisekta kati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli na wadau wa madini uliofanyika Januari 22, 2019.

Aidha, wameitaka wizara kutumia mkutano huo kupanga mipango itakayowezesha Tanzania Ijayo kunufaika na rasilimali madini ikiwemo kuhakikisha inawawezesha wachimbaji wadogo kukua kutoka uchimbaji mdogo, kwenda wa kati na hatimaye kuwa wachimbaji wakubwa.

Vilevile, wajumbe wa kamati wameishauri wizara kulifanyia kazi suala la mitobozano huku ikitakiwa kuweka mazingira mazuri ya kuepusha ajali za wachimbaji wadogo migodini.

Akitoa taarifa kwa kamati hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Deusdedith Magala, amesema kuwa, katika kipindi cha nusu mwaka wa utekelezaji wa bajeti ya Mwaka wa Fedha 2018/19, kuanzia mwezi Julai hadi Disemba, 2018, mgodi wa Kabulo umezalisha tani 4,052 na kuuza tani 1,302 za makaa yenye thamani ya shilingi 96.2 milioni ambapo kutokana na mauzo hayo, serikali imepokea mrabaha na ada ya ukaguzi wa shilingi 8,062,961.31 na ushuru wa huduma shilingi 738,597.94.

Magala ameeleza kuwa, mgodi wa STAMIGOLD umezalisha wakia 7581.55 za dhahabu na wakia 1,014.33 za madini ya fedha yenye jumla ya thamani ya shilingi bilioni 21.3, na kuongeza kwamba, mauzo hayo yameuwezesha mgodi huo kulipa mrabaha wa shilingi bilioni 1.27 katika kipindi hicho.

Akitaja mafanikio mengine, Magala amesema kuwa, shirika hilo limekamilisha ukarabati wa kinu cha kusagia makaa ya mawe kwa lengo la kuongeza thamani ya makaa yanayochimbwa katika mgodi wa Kabulo ili kukidhi mahitaji ya soko.

Aidha, amesema ukarabati mwingine ni pamoja na matengenezo ya njia za kusafirisha makaa ya mawe ikiwemo reli na mikanda; matengenezo ya mashine za kusaga na kuchekecha makaa, uhunzi na uchongaji vipoli na kusema kuwa, ukarabati huo ulitumia gharama ya shilingi 31,471,010.  

 “ Mhe. Mwenyekiti vilevile, shirika linaendelea na tathmini ya kufufua mgodi wa chini wa Kiwira ili nao ujumuishwe katika uzalishaji wa makaa,” amesema Magala.

Akitoa ufafanuzi kuhusu akiba ya uwepo wa makaa ya makaa katika mgodi wa Kiwira, Magala amesema kuwa, unakadiriwa kuwa na wastani wa tani milioni 35.14 za mashapo ya makaa, ambapo kati ya mashapo hayo, yaliyothibitishwa yanafikia tani milioni 22.14 na mashapo yanayoweza kuvunwa kwa faida yanafikia tani milioni 14.64.

Akieleza mikakati ya shirika hilo, Magala amesema kuwa, ni pamoja na kutafuta mbia wa kuendeleza mradi wa visusu vya dhahabu wa Buhemba, kutafuta mkandarasi wa uchimbaji ili kutekeleza sehemu ya uchimbaji wa kokoto katika mradi wa Ubena Zomozi, kuendelea kutafuta mkandarasi mwingine wa uchimbaji ili aweze kuongeza uzalishaji wa makaa ya mawe katika mgodi wa Kabulo na kuendelea kufuatilia vibali vya kuajiri kutoka mamlaka ya ajira za utumishi wa Umma ili kuongeza nguvu kazi ya shirika.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akizungumzia mafanikio ya mgodi wa Stamigold amesema kwamba mgodi huo unafufuka tofauti na ilivyokuwa awali ambapo sasa unazalisha ikiwemo kulipa madai ya wafanyakazi.

Akizungumzia changamoto ya mitobozano, amesema kuwa, wizara inashirikiana na mamlaka za mikoa na wilaya kuhakikisha inatatua migogoro hiyo na kuongeza kuwa, wizara inafanya jitihada za kuwaendeleza wachimbaji wadogo kwa kuwa endapo wataendelezwa, watawezesha kuwepo na mapato ya uhakika kwa serikali kutokana na idadi yao nchini.

Wizara ya Madini na taasisi zake ilianza kukutana na Kamati hiyo kuanzia Januari 21 hadi 23, ambapo taarifa ya utekelezaji kwa wizara na taasisi zake kwa kipindi cha Nusu Mwaka, (2018/19) ziliwasilishwa kwa kamati hiyo.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals