[Latest Updates]: Lazima Kuwa Wabunifu Kwenye Ukusanyaji wa Maduhuli-Prof. Kikula

Tarehe : Feb. 16, 2020, 9:32 a.m.
left

Na Greyson Mwase, Iringa

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa nchini kuwa wabunifu kwenye ukusanyaji wa maduhuli ili Tume ya Madini iweze kuvuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka wa fedha 2019/2020 la shilingi bilioni 470.

Profesa Kikula alitoa kauli yake  jana tarehe 15 Februari, 2020 mkoani Iringa kwenye ziara yake ya kikazi katika mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini, kuzungumza na wachimbaji wa madini pamoja na kutatua kero mbalimbali.

Katika ziara yake Profesa Kikula aliambatana na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Iringa, Mhandisi Abdulrahman Milandu, pamoja na timu ya wataalam kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Iringa na kutoka Makao Makuu ya Tume ya Madini.

Alisema kuwa, mchango wa Sekta ya Madini unategemewa sana kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi hivyo wataalam kwenye Sekta hawana budi kuwa wabunifu katika kuhakikisha wanakusanya maduhuli huku wakidhibiti utoroshwaji wa madini.

Akielezea mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa Tume ya Madini, Profesa Kikula alifafanua kuwa ni pamoja na kuvuka  lengo la ukusanyaji wa maduhuli ambapo katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali ilikusanya jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 346 ikiwa imevuka lengo lililopangwa la kukusanya shilingi bilioni 310.

Alieleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja uanzishwaji wa Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa pamoja na Maafisa Migodi Wakazi kwenye maeneo yenye migodi mikubwa ya madini, uanzishwaji wa masoko ya madini pamoja na vituo vya ununuzi wa madini.

Aliendelea kusema kuwa ili kuhakikisha huduma katika shughuli za utafiti, uchimbaji na biashara ya madini zinaimarika nchini, Serikali imeongeza wataalam kwenye Ofisi za Madini, vitendea kazi ikiwa ni pamoja na magari na mashine za kupima madini kwenye masoko ya madini yaliyoanzishwa.

Aidha, Profesa Kikula aliwataka wamiliki wa leseni za madini kuhakikisha wanaandaa na kutekeleza mipango ya ufungaji wa migodi ili kuepusha athari za uharibifu wa mazingira zinazoweza kujitokeza mara baada ya kumalizika kwa shughuli za uchimbaji wa madini.

Vilevile aliwataka wachimbaji wa madini kuendesha shughuli zao kwa kufuata Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake.

Profesa Kikula alitembelea machimbo ya mchanga yaliyopo katika Kambi ya Jeshi la Magereza la Mlolo yaliyopo Wilayani Iringa, Machimbo ya mchanga ya Ifingo Wilayani Mufindi na Machimbo ya Dhahabu ya Sinai, Ugenza Wilayani Mufindi, mkoani Iringa.

Akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika eneo la Sinai Wilayani Mufindi Mkoani Iringa, Profesa Kikula aliwataka wachimbaji hao kutumia masoko ya madini yaliyoanzishwa na kuongeza kuwa upo utaratibu wa kusogeza huduma kwa kuweka vituo vya ununuzi wa madini ili waweze kunufaika.

Aidha aliwataka wachimbaji hao kujiepusha na migogoro na kuwahakikishia kuwa Serikali ipo tayari kuwasaidia katika kuhakikisha kuwa uchimbaji wao na unakuwa na faida.

Aidha, Profesa Kikula alimpongeza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Iringa kwa utekelezaji wa  mikakati aliyojiwekea kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini katika Mkoa wa Iringa.

Wakati huohuo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Iringa, Mhandisi Abdulrahman Milandu akielezea namna wanavyosimamia shughuli za madini katika mkoa huo, alisema kuwa wachimbaji wengi  hususan wa madini ya ujenzi wameanza kuchimba kulingana na Sheria ya Madini na Kanuni zake inavyotaka kutokana na elimu ambayo imekuwa ikitolewa mara kwa mara na ofisi yake.

Alisema tayari ofisi yake  imetoa elimu kwa wachimbaji wa madini na wananchi kuhusu mpango wa utoaji wa huduma kwa jamii katika migodi ya dhahabu ya  Nyakavangala, Ihanzutwa, Ulata, Uengulinyi, Lupembe Senga na katika maeneo ya uchimbaji wa mchanga, udongo na mawe katika vijiji vya Kibena, Muwimbi, Rungemba, Kikiombo, Saohill, Isakalilo na Kitelewasi vilivyopo katika Wilaya za Iringa na Mufindi.

Aliongeza kuwa Ofisi yake imeanza kuhamasisha wachimbaji wa madini ujenzi na watengenezaji wa tofali kuunda vikundi vidogo na kupewa leseni za madini.

"Tunaamini kuwepo kwa vikundi rasmi vya wachimbaji wa madini ujenzi na watengenezaji wa tofali kutachangia kwa kiasi kikubwa kwenye ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali", alisema Mhandisi Milandu.

Katika hatua nyingine Mhandisi Milandu alisema katika kuhakikisha hakuna utoroshaji wa madini ujenzi katika mkoa wa Iringa, Ofisi yake imekuwa ikishirikiana kwa karibu zaidi na vyombo  vya ulinzi na usalama kama vile jeshi la polisi.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals