[Latest Updates]: Viongozi wasiokwenda na kasi ya Tume ya Madini kutenguliwa

Tarehe : Aug. 6, 2018, 6:01 a.m.
left

Greyson Mwase na Asteria Muhozya, Morogoro

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amesema kuwa viongozi pamoja na maafisa waandamizi walioteuliwa kufanya kazi katika Tume ya Madini teuzi zao zinaweza kutenguliwa iwapo watafanya kazi kinyume na taratibu za utumishi wa umma.

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (katikati waliokaa mbele) Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa tatu waliokaa mbele) Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila ( kushoto waliokaa mbele), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi, (wa pili kushoto waliokaa mbele) na , Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga (wa pili kulia waliokaa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na watendaji kutoka Tume ya Madini

Waziri Kairuki ameyasema hayo leo tarehe 06 Agosti, 2018 wakati wa ufunguzi wa mafunzo  ya kazi kwa viongozi  na maafisa waandamizi wa Tume ya Madini  iliyofanyika mjini Morogoro na kuhudhuriwa na watendaji na watumishi kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. delardus Kilangi.

Alisema kuwa, Serikali imewateua kufanya kufanya kazi na Tume ya Madini  huku ikiwa na matarajio makubwa ikiwa ni pamoja na kuondoa kabisa urasimu kwenye utoaji wa leseni kwa kuhakikisha kuwa wanatoa leseni kwa wakati, kutatua mogogoro ya wachimbaji wadogo na kuwa wabunifu kwenye ukusanyaji wa mapato yanayotokana na madini.

Aidha, Waziri Kairuki aliongeza kuwa watendaji wapya wanatakiwa kuwa makini kwenye zoezi zima la utoaji wa leseni kwa kuhakikisha kuwa wanahakiki historia za waombaji wa leseni kwenye uchimbaji madini kabla ya kutoa leseni mpya.

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (kulia) akibadilishana mawazo na Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto) kwenye mafunzo hayo.

“Ni vyema mkahakikisha kuwa mnafahamu kwa kina historia za waombaji wa leseni za madini hususan kwenye mapato na matumizi kwa mwaka, ulipiaji wa leseni, ushiriki katika utoaji wa huduma za jamii, uzingatiaji wa kanuni za uhifadhi na mazingira na kuwapatia leseni waombaji  wale tu watakaokidhi vigezo,” alisisitiza Waziri Kairuki.

Katika hatua nyingine,Waziri Kairuki alitoa onyo kwa watumishi watakaothubutu kuhujumu mfumo wa huduma za leseni za madini kwa njia ya mtandao ujulikanao kama online mining cadastre transactional portal na kuongeza kuwa Wizara haitasita kuwachukulia hatua za kisheria watakaohujumu mfumo.

Waziri Kairuki aliwataka maafisa madini wa mikoa kuhakikisha wanaainisha maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini na kumpatia taarifa mapema na kuhakikisha wanafanya mikutano ya mara kwa mara na wachimbaji wadogo ili kubaini changamoto zao.

Awali akielezea mafunzo hayo, Waziri Kairuki alisema mafunzo hayo ya siku sita yatalenga kutoa elimu kuhusu historia ya mabadiliko ya sheria ya madini, sheria ya madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017, muundo wa tume ya madini na mawasiliano ya ndani na nje ya tume.

Kutoka kushoto, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Prof. Shukrani Manya, Kamishna wa Tume ya Madini, Dk. Athanas Macheyeki wakifuatilia ufafanuzi uliokuwa unatolewa na Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (hayupo pichani) kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo.

Aliendelea kueleza maeneo mengine kuwa ni pamoja na muundo na mfumo wa mawasiliano wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), taratibu za ofisi na makusanyo na maduhuli ya Serikali kwa njia ya kieletroniki (GEPG), usimamizi na utunzaji wa mali za umma, taratibu za utoaji wa leseni za shughuli za madini na ushirikishwaji wa wananchi/wazawa katika shughuli za madini.

Maeneo mengine ni pamoja na ukaguzi wa madini na biashara, utatuzi wa migogoro katika sekta ya madini, taratibu za uwasilishaji wa taarifa makao makuu ya Tume na kwenye mamlaka nyingine zinazohusika, utunzaji wa siri katika utumishi wa umma, masuala ya utawala na rasilimaliwatu, sheria, kanuni na taratibu za fedha, usimamizi wa mifumo ya udhibiti wa ndani, maadili katika utumishi wa umma na mfumo wa uwazi wa upimaji utendaji kazi (OPRAS).

Alisema kuwa  kwa kuwa tume imepata watumishi wa kutosha inatakiwa kuunda kamati mbalimbali za kisheria na kitendaji kama vile kamati ya maadili, kamati ya ukaguzi, kamati ya ajira za kigeni na baraza la wafanyakazi ili kuifanya tume iweze kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

Kaimu Mhasibu Mkuu wa Tume ya Madini, Avodia Lukonge (kushoto) akibadilishana mawazo na Mkaguzi wa Ndani kutoka Tume ya Madini, Happiness Shirima kabla ya kuanza kwa ufunguzi wa mafunzo hayo.

Naye Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza katika mafunzo hayo alimshukuru Waziri Kairuki kwa uteuzi wa watendaji wapya wa Tume ya Madini na kuwataka washiriki wa mafunzo hayo kuyafanyia kazi yote watakayojifunza.

Wakati huohuo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi alisema kuwa mabadiliko ya sheria ya madini yaliyofanyika Tanzania ni hatua ya ushujaa na kuongeza kuwa mataifa mengine yameanza kujifunza.

Alisema kutokana na muhimu wa Sekta ya Madini kwenye mchango wa ukuaji wa uchumi wa nchi ameamua kufika mwenyewe kuja kutoa mafunzo kwa viongozi na maafisa waandamizi wa Tume ya Madini ili waweze kusimamia ipasavyo sekta hiyo kwa kutumia sheria na kanuni za madini.

 

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals